2018-02-17 15:25:00

Ubatizo ni nguvu ya Kristo inayookoa na kutakasa!


Ni dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima; kipindi cha kumrudia Mungu kwa toba, mfungo mtakatifu, sala, matendo ya huruma na kuwasaidia wahitaji. Ni kipindi cha kujiandaa kukutana na Kristo Mfufuka ili kufufuka pamoja naye. Kutuongoza katika Kwaresima hii, Baba Mtakatifu Francisko ametupatia ujumbe wake wa Kwaresma wenye kauli mbiu “na kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa” (Mt. 24:12), anatualika tujihadhari na manabii wa uongo, ubaridi katika maisha ya kiroho na kijamii, kukuza moyo wa sala, matendo ya huruma na kufunga. Nalo Baraza la Maaskofu wa Tanzania katika Ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2018, sambamba na Baba Mtakatifu Francisko wanatualika tuutafakari upya utume wetu ambao ni agizo la Kristo kwetu “Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu”. Utekelezaji wa utume huu ni kutimiza wajibu mpana unaomgusa mwanadamu katika kila nyanja ya maisha: imani, jamii, siasa, uchumi na kadhalika na katika hizo zote kumwezesha kuishi kama alivyokusudia Mungu muumba wake.

Masomo kwa Ufupi

Somo la Kwanza (Mwa. 9:8-15) Baada ya gharika kuu Mungu anaweka agano na Nuhu. Ni agano ambalo linaambatana na ahadi ya Mungu kwamba hataangamiza tena viumbe kwa njia ya maji ya gharika. Anathibitisha agano hilo na anaweka upinde wa mvua kama ishara ya agano kati yake na ulimwengu na kuwa alama ya uaminifu wa Mungu kwa agano hilo. Agano hili linao upekee wake pia. Mungu haliweki kati yake na binadamu tu bali anaviunganisha ndani yake viumbe vingine vyote ambavyo pia vina uhai.

Somo la Pili (1Pet. 3:18 - 22) Katika ujumla wake, waraka huu Petro aliwaandikia wakristo wapya, yaani wale waliokuwa wamebatizwa siku za karibuni, kwa lengo la kuimarisha imani yao dhidi ya mateso waliyokuwa wakiyapata toka katika serikali ya kirumi. Katika somo la leo, Mtume Petro anawaambia wakristo hao kuwa ubatizo walioupokea ni alama ya wokuvu. Kama wakati wa Nuhu watu walivyookoka kwa maji ndivyo nao sasa kwa maji ya ubatizo wanaokolewa. Na tena maji ya ubatizo si tu alama ya juu juu bali yana nguvu ya ndani (ni sakramenti) ya kumleta mtu katika muungano na Mungu. Injili (Mk. 1:12 - 15) Injili ya leo inaleta kwetu vitu vitatu: Yesu kujaribiwa jangwani, kutiwa gerezani kwa Yohane Mbatizaji na mwaliko wa kutubu na kuiamini Injili, mwaliko anaoutoa Yesu anapoanza kuhubiri Habari Njema.

Yesu anajaribiwa jangwani kwa siku 40 kama ambavyo pia waisraeli walijaribiwa jangwani kwa miaka 40. Tofauti nao, Yesu anayashinda majaribu hayo ya ibilisi. Kutiwa gerezani kwa Yohane Mbatizaji kunaashiria mwisho wa utume wake maana baada ya hapo alikatwa kichwa. Hapo hapo Yesu naye anaanza rasmi utume wake wa hadhara. Yohane Mbatizaji ambaye alikuwa mtangulizi wa Yesu na aliyemwandalia njia hapa pia anaashiria kwa Yesu kuwa kama utume wake ulivoishia kutiwa nguvuni na kuuawa ndivyo pia utume wa Yesu utakavyoishia nguvuni na kuuawa. Kifo cha Yesu lakini kinakuwa ni ushindi dhidi ya ibilisi na utawala wake na kinakuwa ni mwanzo wa utawala wa Mungu, utawala ambao mwanadamu anaalikwa kuuingia kwa kutubu, kuongoka na kuiamini Injili.

Tafakari

Tangu kale, kipindi cha Kwaresma kimekuwa pia ni kipindi ambamo ndani yake Kanisa huwaandaa kwa ukaribu zaidi wale wanaotegemea kubatizwa wakati wa Paska. Na kwa wale waliokwisha batizwa, maandalizi haya yalilenga kufufua ndani yao “motomoto” wa ubatizo waliokwisha upokea. Ni kwa sababu hii, liturujia ya leo inaleta masomo yanayofafanua baadhi ya vipengele muhimu kuhusu ubatizo. Maji ya Ubatizo, katika Agano la Kale, yanafananishwa na maji katika gharika kuu wakati wa Nuhu na katika Agano Jipya, yanafananishwa na kifo cha Kristo. Ufanano huu unaashiria nguvu ya kuokoa inayopatikana katika ubatizo: kama vile maji ya gharika yalivokuwa na nguvu ya kuwaangamiza waovu na kuwaokoa waaminifu wa Mungu ndivyo hivyo maji ya ubatizo yanavyoweza kuangamiza dhambi na uovu ndani ya wanaoyapokea na kuwapatia wokovu. Hali kadhalika kwa maji ya ubatizo, mbatizwa anashiriki kifo cha Kristo, ili kama Kristo alivyofufuka ndivyo na huyo aliyekufa pamoja naye kwa ubatizo atakavyofufuliwa, ndiyo kupewa hadhi mpya, kuishi maisha mapya na kupata amana ya uzima wa milele. Kumbe ubatizo si kama jando la kumwingiza mtu katika rika au ukoo fulani tu, ubatizo unaenda zaidi ya hapo. Ni nguvu ya Kristo inayookoa.

Ujumbe wa Kwaresima kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania umetualika pia kuiangalia Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, Jubilei tunayoadhimisha mwaka huu 2018. Katika kuitafakari historia ya uinjilishaji hasa kipindi cha mwanzo cha wamisionari maaskofu wetu wanakiri “uinjilisha ulifanikiwa, ijapokuwa kwa kukabiliwa na changamoto nyingi” na hapo hapo wanahoji “Uinjilishaji mpya leo hii unalenga kuwasaidia wakristo kuishi ukristo kadiri ya mazingira ya leo na hivyo kuwa kielelezo cha kweli cha imani?”(Rej. Ujumbe wa Kwaresima 2018, uk.5 toleo la PDF). Kujibu swali hili kunaalika tafakari pana juu ya namna yetu sasa ya kuwaandaa waamini na namna waamini wanavyojiandaa kwa sakramenti za awali (Ubatizo, Ekaristi na Kipaimara) vigangoni, parokiani na majimboni. Kwa mwanga wa masomo ya leo tunaalikwa kuepuka kukurupusha maandalizi na hapo hapo kufufua mara kwa mara ule “motomoto” wa imani tunayoikiri ubatizo ili maisha yetu yaendelee kuwa kielelezo cha kweli cha imani hiyo daima.

Vishawishi vya yule mwovu shetani havituachi hata baada ya kupokea ubatizo na huturudisha nyuma daima tusitoe kielelezo cha imani katika maisha yetu. Vishawishi/majaribu hayo ni mengi katika maisha yetu. Yapo mepesi lakini pia yapo magumu; yapo ya muda mfupi lakini yapo yanayodumu; yapo yanayotoka ndani yetu wenyewe lakini yapo pia yanayotoka nje; yapo kila sehemu. Masomo yetu ya leo yanatuonesha kuwa sio sisi tu, bali Kristo naye alijaribiwa. Majaribu ya Yesu yanaletwa kwetu kutuonesha kuwa inawezekana kuyashinda majaribu. Inawezekana. Inawezekana kwa msaada wa Mungu.

Katika kipindi hiki cha Kwaresima Kanisa linatualika kuchota nguvu ya kushinda majaribu kutoka katika kufunga na kujikatalia. Kufunga na kujikatalia kunatiisha vilema vyetu ambavyo ndiyo chanzo kikubwa cha Majaribu yetu (Yak 1:13) na kunatujengea nidhamu ya ndani tunayoihitaji sana ili kuvishinda vishawishi. Kufunga na kujitakalia kunaruhusu nguvu yetu ya ndani tuliyojaliwa na Mungu kuongoza maisha yetu na si kuongozwa na vionjo na mivuto ya nje kama chakula, vileo, burudani ambavyo kwa siku hizi 40 tunajifunza kuviwekea nidhamu. Mtakatifu Alfonsi Maria Liguori kuhusu vishawishi anafundisha kuwa kuna aina ya vishawishi ili uvishinde lazima uvikimbie. Kristo aliyeshawishiwa na kuvishinda vishawishi awe daima tumaini letu katika kupambana na nguvu za yule mwovu.

Kwako msomaji ninakutakia Kwaresma njema.

Pd. William Bahitwa

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.