2018-02-17 06:40:00

Kwaresima ni kipindi cha upendo na mshikamano; toba na wongofu!


Kwaresima ni kipindi cha mapambano ya “Jangwa la maisha ya kiroho” kwa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha. Kwa kufunga na kusali; kwa njia ya matendo ya huruma sanjari na kujikita katika maisha ya kisakramenti ili kupata: neema na baraka, toba na wongofu wa ndani. Kwaresima ni muda uliokubalika kwa waamini kujizatiti katika maisha ya kiroho kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kwa njia hii, waamini wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Kristo Mfufuka kwa watu wa Mataifa!

Hiki ndicho kiini cha Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima, ambacho, kwa wao kinaanza rasmi tarehe 19 Februari, 2018. Huu ni mwaliko wa kuishi kikamilifu kazi ya ukombozi inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma na upendo wa Mwenyezi Mungu unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kiroho na kikanisa! Wakristo wanahamasishwa kuondokana na chachu ya unafiki wa Mafarisayo, waliodhani kwamba wanaweza kujiokoa wenyewe kwa kuwa na sheria ngumu.

Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani kwa kuondoa moyo wa jiwe kama ilivyokuwa kwa Mwana Mpotevu, ili kuonja tena huruma na upendo wa Mungu. Waamini waguswe na mahangaiko ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, ukame wa kutisha; upweke na utupu wa maisha; magonjwa na athari za majanga asilia. Waamini watumie kipindi cha Kwaresima kujiwekea msingi utakaowasaidia kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wawe na unyenyekevu kama ule wa Mtoza ushuru na Mwana mpotevu aliyethubutu kurejea tena nyumbani kwa Baba mwenye huruma baada ya kutapanya mali ya Baba yake kwa makahaba!

Mifano ya watakatifu waliojisadaka kwa ajili ya huduma, sala na ushuhuda wa Fumbo la Msalaba wawe ni mifano bora ya kuigwa katika maandalizi ya kukutana na Kristo Yesu, Mfufuka kwa wafu, chemchemi ya maisha mapya! Kwaresima ni muda wa kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa, udugu na mshikamano katika maisha ya kiroho na kijamii, ili kushiriki na kuwashirikisha wengine Fumbo la maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati wa kushikamana katika mapambano dhidi ya ubaguzi kwa kukazia fadhila ya umoja, upendo na udugu. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ambalo ni kazi ya mikono ya wanadamu iwe ni changamoto ya kusimama kidete: kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote, ili kuitengeneza dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2018 anakaza kusema, waamini wajifunze kushikamana katika mchakato wa kumwilisha fadhila, kusimama kidete katika kutafuta na kudumisha mafao ya wengi pamoja na kutii Sheria za Kanisa. Waamini wafunge na kusali kadiri ya mafundisho ya Kanisa, ili kujenga na kuimarisha umoja na mafungamano ya kijamii mintarafu mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Kanisa liwe ni chemchemi ya uhai ili waamini waweze “kuishi katika ukweli na upendo”. Maisha ya waamini wa Kanisa la Kiorthodox yanajikita haswa katika Liturujia ya maisha na utume wa Kanisa unaopata hitimisho lake katika adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, ibada inayorutubisha ufahamu wa Kanisa.

Tasaufi ya maisha ya Kanisa la Kiorthodox inawawezesha waamini kuthamini mwili na roho; kwa kuhakikisha kwamba, mwili unapata mahitaji yake msingi na roho inashibishwa kwa Neno la “Utamu wa ngano na asali kutoka mwambani”. Waamini wakumbuke kwamba, miili yao ni Hekalu na makao ya Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, wao wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa kazi ya Roho Mtakatifu, ili kushirikiana kwa dhati na Roho Mtakatifu kwa njia ya ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa.

Matunda ya maisha ya kiroho yanamwilishwa kwa namna ya pekee kwa njia ya upendo kwa Mungu na jirani na kwamba, mambo yote yatapita, lakini upendo haupungui neno wakati wowote. Upendo wa dhati ni matunda ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na kielelezo cha utimilifu wa maisha ili hatimaye, kuonja ukweli wa mambo ya nyakati! Imani ya Kanisa ni chemchemi ya neema katika mapambano ya maisha ya kiroho sanjari na kumwilisha upendo kwa Mungu na jirani. Huu ni upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu unaowawajibisha waamini: kufunga, kusali, kujisadaka na kufanya matendo ya huruma.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kufafanua kwamba, Mwenyezi Mungu ameahidi kuwa pamoja na waja wake hadi utimilifu wa dahali. Kipindi cha Kwaresima, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kujikita kikamilifu katika mapambano dhidi ya uchoyo na ubinafsi kwa kutumaini, kufurahi na kudumu katika kusali. Fadhila ya unyenyekevu iwawezeshe waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu; kwa kujenga na kudumisha ibada, moyo wa toba na msamaha; daima Mwenyezi Mungu akipewa sifa, utukufu na shukrani kwani Yeye ndiye muweza wa yote! Tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama siku ya wokovu ndiyo sasa ndivyo Maandiko Matakatifu yanavyokazia. Anahitimisha ujumbe wake wa Kwaresima kwa kusema, Kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa ya kufunga na kusali pamoja na kumwilisha matendo ya huruma, kielelezo cha imani na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.