Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Kenya: Huu ni wakati wa ukweli, haki, majadiliano na upatanisho!

Maaskofu Katoliki Kenya: Kwaresima ni wakati muafaka wa kujikita katika ukweli na haki kwa wote ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha majadiliano na upatanisho wa kitaifa! - REUTERS

17/02/2018 08:10

Dhamana na wajibu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya ni kuhakikisha kwamba: umoja, amani na uhuru wa kweli vinatawala katika maisha ya familia ya Mungu nchini humo. Kanisa linapenda kujikita katika mchakato mzima wa majadiliano katika ukweli na uwazi; ustawi na maendeleo ya wengi, ili  kudumisha misingi ya upatanisho wa amani, utulivu na mafungamano ya kitaifa ili hatimaye, kudumisha haki kwa wote! Haya ndiyo mambo msingi yanayovaliwa njuga na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2018.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, matatizo, changamoto na kinzani zinazojitokeza miongoni mwa familia ya Mungu nchini Kenya, zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya majadiliano katika ukweli, uwazi na haki kwa wote, ili amani ya kudumu iweze kupatikana. Ikumbukwe kwamba, hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani dumifu! Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka huu imezinduliwa kwenye Jimbo kuu la Kisumu, tarehe 10 Februari 2018 na inaongozwa na kauli mbiu “upatanisho wa amani, utulivu na mafungamano ya kitaifa ili kudumisha haki kwa wote”! Kwa ufupi haya ndiyo mambo makuu yanayopewa kipaumbele cha pekee na viongozi wa Kanisa nchini Kenya wakati huu wa kipindi cha Kwaresima.

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, CJPC, katika mahubiri yake, anaitaka familia ya Mungu nchini Kenya kujikita katika mchakato wa upatanisho na msamaha, ili kuganga na kuponya madonda ya chuki, uhasama, kinzani na utengano unaoweza kuhatarisha mafungamano ya kitaifa. Kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa ya kumwilisha Sala Kuu ya Baba Yetu, ambayo kimsingi ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu, kwa kupiga moyo konde na kuanza kujipatanisha na jirani zao.

Watu wengi wametikiswa na kuguswa na mpasuko wa kisiasa uliojitokeza nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu na marudio yake yaliyofanyika mwaka 2017. Upatanisho ni mchakato wa lazima na muhimu sana kwa familia ya Mungu nchini Kenya, ili kuanza na hatimaye, kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi! Msamaha wa kweli unafumbatwa katika misingi ya haki na usawa. Hii ni changamoto kwa Serikali ya Kenya chini ya Rais Uhuru Kenyatta pamoja na wapinzani wanaongozwa na Bwana Raila Odinga.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya uzinduzi wa Kampeni ya Kwaresima Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya iliongozwa na Askofu mkuu Zacchaeus Okoth wa Jimbo kuu la Kisumu aliyeitaka familia ya Mungu nchini Kenya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Anakiri kwamba, kwa sasa Kenya inawaka moto wa chuki unaoweza kuzimwa kwa ushuhuda wa Injili ya upendo na mshikamano. Wakenya wajiulize maswali msingi, wanaelekea wapi kama taifa? Wanatendeanaje kama ndugu? Hayo wanayoyafanya wanayafanya kwa sababu gani? Umefika wakati kwa familia ya Mungu nchini Kenya kupandikiza na kukuza mbegu ya haki kwa kutambua kwamba, kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa, kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2018. Upendo unaendelea kupoa kutokana na kuongezeka kwa kukosekana usawa katika vyombo vya sheria; hali ya kukata tamaa; ukosefu wa demokrasia na utawala wa sheria na kwamba, wananchi wa Kenya watubu na kumrudia tena Mwenyezi Mungu.

Jimbo kuu la Kisumu nchini Kenya lina historia ya nyanyaso na dhuluma tangu mwaka 1969 kulipotokea mauaji ya kinyama na kwamba, watetezi wa wanyonge wanaendelea kushikishwa adabu na kunyamaziwa kwa mtutu wa bunduki. Kati yao ni: Thomas Joseph Mboya aliyeuwawa kikatili kunako mwaka 1969, Argwings Kodhek aliyeuwawa na watu wasiojulikana kunako mwaka 1969 bila kumsahau Hayati Chris Chege  Msando aliyekuwa mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya, (IEBC) kitengo cha teknolojia aliyeuwawa kunako mwaka 2017.

Kwa upande wake Kanon Peter Karanja, Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Kenya, NCCK, anasema, kuna mpasuko mkubwa nchini Kenya unahitaji mchakato wa majadiliano ya kitamaduni na kikabila, ili kujenga umoja na mafungamano ya kitaifa nchini Kenya. Shida kubwa kwa sasa ni uchu wa mali na madaraka unaolisambaratisha taifa badala ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa. Hali ya uchumi inaendelea kuwa mbaya na utawala wa sheria unaanza kufutika taratibu sanjari na uhuru wa vyombo vya habari kiasi cha kutishia usalama na maisha ya wengi. Wadau mbali mbali wanapaswa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu wa Mwaka 2017 ili uchaguzi wa mwaka 2022 uweze kuwa: huru, wa kweli na wa haki kwa wote. Ni vyema pia kuipitia Katiba ya Nchi ya Kenya ili kuangalia mianya inayoweza kusababisha mipasuko ya kitaifa ili iweze kurekebishwa mapema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

 

 

 

17/02/2018 08:10