2018-02-16 10:48:00

Papa Francisko awataka Maaskofu "Kujifunza kustaafu"


Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi “Imparare a congedarsi” yaani “Kujifunza Kustaafu” anatoa wosia na sala kwa viongozi wa Kanisa kujiandaa vyema kung’atuka kutoka madarakani, kwa kutambua kwamba, hii pia ni sehemu ya huduma inayohitaji mfumo mpya wa uwepo na uwajibikaji. Haya ni maandalizi muhimu sana ya maisha ya ndani, kwani inawezekana kabisa kung’atuka kutoka madarakani kwa kigezo cha umri au pale ambapo Askofu anaombwa kuendelea na utume wake kwa muda mrefu kidogo, hata kama atakuwa ametimiza umri wa miaka 75, ambao kisheria: Maaskofu pamoja na wale walioteuliwa na Papa wanapaswa kuachia madaraka!

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kujiandaa kikamilifu mbele ya Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, ili kuachana na kishawishi cha uchu wa madaraka kwa kudhani kwamba, wao ni watu muhimu sana na wala hakuna mbadala. Mwelekeo huu wa maisha ya ndani unaojikita katika sala utawasaidia viongozi wa Kanisa kuvuka kipindi hiki kigumu kwa: amani, utulivu wa ndani na matumaini, vinginevyo, kinaweza kugeuka na kuwa wakati wa kinzani na machungu katika maisha. Kiongozi wa Kanisa anayetambua ukweli wa kujiandaa, anapaswa kuwa na mang’amuzi yanayofumbatwa katika sala namna ya kufungua ukurasa mpya wa maisha yake baada ya kung’atuka kutoka madarakani, kwa kuanza kuweka mikakati mipya ya maisha inayofumbatwa katika sadaka, unyenyekevu, sala pamoja na kujisomea zaidi! Pale inapowezekana, kiongozi wa Kanisa awe tayari kutoa huduma za kichungaji kadiri ya uwezo na nafasi yake.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, pale inapotokea kwamba, kiongozi wa Kanisa anaombwa kuendelea na utume wake kwa muda mrefu kidogo, ina maanisha kwamba, sasa anapaswa kuweka kando mipango yake binafsi kwa moyo wa ukarimu na kwamba, fursa hii ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na wala kamwe isichukuliwe kama kielelezo cha mafanikio ya mtu binafsi, urafiki au zawadi kutokana na utendaji makini wa shughuli za kichungaji! Maamuzi yanayotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni sehemu ya wajibu wake wa kuongoza unaofumbatwa katika hekima na busara inayomwezesha kufanya mang’amuzi na hatimaye, kutoa uamuzi sahihi.

Baba Mtakatifu anasema, maamuzi haya yanaweza kutolewa ili kumpatia kiongozi wa Kanisa kumalizia mradi fulani ambao ni kwa ajili ya ustawi wa Kanisa; kuwa na uhakika wa mwendelezo wa utume fulani ndani ya Kanisa au wakati wa mabadiliko ya watendaji wakuu kwenye Sekretarieti kuu; mchango unaoweza kutolewa na kiongozi huyu wa Kanisa katika utekelezaji wa sera na maamuzi yaliyotolewa na Kiti kitakatifu au mwongozo katika mafundisho ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, tayari mada hii ilikwisha kujadiliwa kwenye mwongozo wa “Rescriptum ex audientia” yaani mazungumzo kati yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican kunako tarehe 3 Novemba 2014, kwa kubainisha Sheria za Kanisa, kufanya mabadiliko kwa baadhi ya Sheria hizi pamoja na kuziwekea mkazo. Ushuhuda na mang’amuzi yaliyotolewa na viongozi waliojisadaka kwa ajili ya utume na huduma mbali mbali katika Kanisa kama: Maaskofu mahalia, viongozi wakuu wa Mabaraza ya Kipapa au Mabalozi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia umemwezesha Baba Mtakatifu Francisko kutambua umuhimu wa kutekeleza: Sheria, Kanuni na Taratibu mintarafu muda na jinsi ya kuweza kung’atuka kutokana na umri.

Baada ya kupata ushauri makini, Baba Mtakatifu Francisko anasema viongozi wa Kanisa wataweza kung’atuka madarakani pale ombi lao linaporidhiwa na viongozi wakuu wanaohusika. Papa Francisko kwa Barua hii Binafsi “Imparare a congedarsi” yaani “Kujifunza Kustaafu”  anatamka kwamba: Maaskofu Jimbo, Waandamizi na Wasaidizi wanatakiwa kuwasilisha barua za kung’atuka kutoka madarakani kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wanapogota umri wa miaka 75.

Kwa viongozi wa Sekretarieti kuu ya Vatican wasiokuwa Makardinali, Mabalozi wa Vatican licha ya kugota umri huo, hawatang’atuka madarakani moja kwa moja, lakini watapaswa hata wao kuwasilisha barua ya kuomba kung’atuka kutoka madarakani; naye Khalifa wa Mtakatifu Petro, baada ya tafakari ya kina, atatoa maamuzi yake na mhusika kuhabarishwa kama ameridhia au bado amepewa muda kidogo wa kuendelea na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha kwa kusema kwamba yale yote aliyokusudia katika Barua hii Binafsi “Imparare a congedarsi” yaani “Kujifunza Kustaafu”  yanapaswa kutekelezwa mara moja baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano na Gazeti rasmi la “Acta Apostolicae Sedis”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.