2018-02-15 13:06:00

Bwana Jacob Zuma abwaga manyanga ya Urais Afrika ya Kusini!


Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya kusini (SACBC) lilimshauri Rais Jacob Zuma mwenye umri wa miaka 75 kutafakari na kufanya maamuzi sahihi kama mtu mzima mwenye busara na kwa ajili ya mafao ya taifa lake. Mwaliko huu wa Maaskofu nchini humo ulitolewa kufuatia shinikizo alilowekewa Rais Zuma kutoka ndani ya chama chake mwenyewe ili ajiudhuru kabla ya muda wake kuisha, ambao ungekuwa mwishoni mwa mwaka 2019. Katika uongozi wake kama Rais Jacob Zuma ameandamwa sana na kashfa ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma pamoja na kudorora kwa uchumi wa Afrika ya Kusini, ambayo miaka kadhaa iliyopita, uchumi wake ulikuwa unakua kwa kasi ya ajabu! Bwana Jacob Zuma daima amekanusha shutuma zote hizi dhidi yake.

Bunge la Afrika ya Kusini, Alhamisi, tarehe 15 Februari 2018 limepokea rasmi barua ya Jacob Zuma ya kujiuzuru kutoka madarakani kama Rais wa Afrika ya Kusini kwa ajili ya mafao umma. Tayari Bunge limeanza mchakato wa kumtafuta mrithi wake na kwamba, kwa sasa Makamu wa Rais, Bwana Cyril Ramaphosa ndiye anayeiongoza Afrika ya Kusini na anatarajiwa kuthibitishwa na kuongoza nchi hadi kufikia mwaka 2019, Afrika ya Kusini itakapofanya uchaguzi mkuu.

Bwana Cyril Ramaphosa anasema, atasimama kidete kupambana na rushwa pamoja na ufisadi ambao umekichafua sana Chama cha A.N.C huko Afrika ya Kusini. Wachunguzi wa mambo wanasema, Rais mpya lazima ajikite katika mchakato wa kupambana na “Mtandao wa uhalifu” ambao umeitikisa sana Afrika ya Kusini kwa miaka ya hivi karibuni. Bwana Jacob Zuma katika hotuba yake ya kung’atuka kutoka madarakani kwa ajili ya mafao ya umma amesema kwamba, hasingependa kuona damu ya watu wasiokuwa na hatia Afrika ya Kusini inamwagika kwa sababu ya jina lake wala A.N.C kugawanyika na kumeguka.

Huu ni uamuzi ambayo ameufanya kwa uchungu na shinikizo kutoka katika Chama cha A.N.C ambacho kilimpatia muda wa saa 48 kuwa ameng’atuka kutoka madarakani vinginevyo wabunge wa Chama chake wangempigia kura ya kutomwamini, hali ambayo ingepelekea kushitakiwa na hatimaye kukosa marupurupu yake yote kama Rais wa Afrika ya Kusini. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, kuna upepo wa nguvu ya umma unaoendelea kuvuma Kusini mwa Afrika, kwa viongozi kung’atuka kutoka madarakani kwa mafao ya umma. Kumba kumba hii ilimpitia Mzee Robert Mugabe wa Zimbabwe hivi karibuni na sasa Bwana Jacob Zuma ametumbukia huko! Moto unaendelea kuwaka huko nchini DRC, wananchi wakitaka Rais Joseph Kabila kung’atuka madarakani ili kupisha mchakato wa uchaguzi mkuu kuanza mara moja! Baada ya Jacob Zuma kung’oka madarakani kwa nguvu ya umma, nani tena Barani Afrika akafuatia na hatimaye, kuangukiwa na mkuyu?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News

 








All the contents on this site are copyrighted ©.