Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Ujumbe wa Kwaresima Tanzania: Uinjilishaji, maendeleo na demokrasia

Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Ustawi, Maendeleo na Mafao ya wengi sanjari na demokrasia kama utekelezaji wa haki msingi za binadamu ni kiini cha Ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2018 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. - RV

13/02/2018 08:44

Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa mwaka 2018. Ni ujumbe unaozingatia matukio makuu matatu: Jubilei ya Miaka 150 ya Ukristo Tanzania Bara, Miaka 50 ya Tamko la Maaskofu kuhusu Mwelekeo na Hatima ya Tanzania na Maandalizi ya Uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2019. Wapendwa Familia ya Mungu, Na Watu Wote wenye Mapenzi Mema, “Neema na iwe kwenu, na amani zitokazo kwa Mungu, Baba yetu” (Kol 1:2).

Kama ilivyo ada ya Wakristo pote ulimwenguni, kwa kipindi cha siku arobaini kabla ya kuadhimisha Jumapili ya Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo, Wakristo hutumia muda huo kufunga, kufanya toba na kufanya matendo ya huruma kwa wote wenye mahitaji huku wakijitafakari kuhusu uhalisia wa hali yao ya kuwa ni wenye dhambi mbele ya Mungu, ili waweze kufanya toba ya kweli na yenye mageuzi na wongofu katika maisha. Mwaka huu kipindi hiki, kijulikanacho kama kipindi cha Kwaresima, kinaanzia tarehe 14 Februari Jumatano, siku ambayo inajulikana kwa jina la Jumatano ya Majivu, mpaka tarehe 29 Machi, ambayo itakuwa ni siku ya Alhamisi Kuu.

Kwa mwaka huu wa 2018 kipindi hiki, cha kujitafakari mbele ya Mungu na kufanya toba hususan uhai wa imani yetu kwa njia ya matendo ya huruma, haki, upendo na amani kwa jirani zetu, ni kipindi chenye upekee wa aina yake kwa sababu kuu tatu: 1) Ni katika mwaka huu ambapo Kanisa Katoliki Tanzania  linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, na kilele chake kitakuwa tarehe 2 Oktoba; 2) Mwaka huu pia utakuwa ni mwaka wa 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko rasmi kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi yetu; na 3) Mwaka huu ni mwaka wa maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji  hapo mwakani 2019. Kwa sababu kuu hizo tatu, ni vema tafakari yetu ya Kwaresima ikalenga katika swali ambalo, kwa namna moja au nyingine, linahusu sababu hizo tatu. Kwa njia ya swali hilo mwanadamu hudiriki kumhoji na kumuuliza Mungu na Muumba wake kuhusu hali ya binadamu mwenzake. Swali hilo ni “Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mw. 4:9).

Hali halisi ya nchi yetu, kwa yeyote anayesoma ishara za nyakati kwa makini, inalifanya swali hilo liwe na uzito wake kuendana na sababu hizo kuu tatu zilizotolewa. Lakini pia, tukumbuke kuwa mwaka 2018 ni mwaka wa sabini (70) tangu Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa walipotamka rasmi na kujifunga kuhakikisha kuwa Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 linatekelezwa. Na sasa tuone ni kwa namna gani swali hilo linatuhusu kwa kuangalia misingi ya sababu hizo kuu tatu.

Kuhusu sababu ya kwanza, ni lazima tunapoadhimisha miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara tujiulize hilo swali kwa namna ifuatayo: “Je, sisi Wakatoliki katika kipindi hicho cha miaka 150 tumekuwa walinzi wa binadamu wenzetu, ambao tumefanywa kuwa ndugu zao kama Familia ya Mungu kupitia Mwanae Yesu Kristo na Mama yetu Bikira Maria?”. Kuhusu sababu ya pili, tujiulize swali hilo hilo kama ifuatavyo: “Je, katika kipindi hicho cha miaka hamsini, kuanzia 1968 mpaka mwaka huu 2018, sisi Wakatoliki tumekuza roho na moyo wa kuwajali binadamu kama ndugu zetu, kuendana na barua ya kichungaji ya mwaka huo, yenye kichwa cha habari The Church and Developing Society of Tanzania,  iliyotuasa kuwa falsafa na imani ya Azimio la Arusha, Azimio ambalo lilitoa mwelekeo na hatima ya nchi yetu, inakubaliana kwa karibu kabisa na ( kwa kunukuu sehemu ya ujumbe huo) “roho ya kweli ya Kristo na Kanisa, roho ambayo ni ya udugu, ya kumegeana, ya kuhudumiana na ya kufanya kazi kwa bidii?” Kwa kusisitiza ukaribu huo kati ya Azimio la Arusha na roho ya kweli ya Kikristo, barua hiyo ya kichungaji ilizingatia barua ya Yakobo, 2:14-17 inayosema kuwa imani bila matendo ni imani mfu!

Kuhusu sababu ya tatu, baada ya kufanya toba na kusherehekea Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo, tukiwa na ari na mwelekeo mpya wa maisha ya Kikristo yanayodhirishwa na imani hai, swali hilo tulihusishe na dhamira ya kweli ya viongozi wetu watarajiwa wa serikali za mitaa, kwa kujiuliza, “Mwaka huu wa maandalizi ya kuchagua viongozi wa serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji, tufanye nini ili maandalizi yetu ya uchaguzi yatupe viongozi wetu wa karibu ambao hawatakwepa wajibu wao kwa kujitetea kwa mtazamo wa swali kama hilo?”

Hivyo basi, ili kuhakisha kuwa tuna pata majibu ya kweli na yenye kuleta mabadiliko katika nafsi zetu na mahusiano na ushirikiano katika jamii yetu, ujumbe huu wa Kwaresima una lengo la kuwahimiza, kuwahamasisha na hata kuwadai waumini Wakatoliki wote kuuitikia kwa moyo wa toba, mageuzi na kushiriki kwa kujitoa zaidi katika uinjilishaji wa nchi yetu kama mwanga na chumvi ya ulimwengu wa Tanzania. Kufikia lengo hilo, tunahimiza Jumuiya Ndogondogo katika kila parokia ziutafakari kwa makini ujumbe huu, zipange namna ya kuutekeleza kwa kuzingatia hayo maswali matatu. Ili kufanikisha hilo, tunatoa mwongozo ufuatao katika hatua tatu: 1) Kusoma ishara za nyakati za Tanzania na kuzichambua; 2) Kuzitathmini ishara hizo kwa misingi ya Injili na tunu za Ufalme wa Mungu kuendana na masomo na Injili ya Jumatano ya Majivu; na 3) Kufanya maamuzi yatokanayo na tathmini hiyo na kupanga utekelezaji wa maamuzi hayo. Tunawaalika basi, tutembee pamoja katika kulitafakari fumbo la imani yetu, huku tukiomba neema ya Mungu ifanye kazi ndani yetu na kutujalia kukua katika kumpenda, kumjua na kumtumikia Mungu na vivyo hivyo kumpenda jirani huku tukitumikiana sisi kwa sisi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

 

 

13/02/2018 08:44