2018-02-13 10:34:00

Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Mt. Egidio: Amani, Afya na Elimu!


Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, yenye makao yake makuu mjini Roma, inasherehekea Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake hapo tarehe 7 Februari 1968 kwa kujikita katika Sala, Maskini na Amani duniani. Kwa kipindi chote hiki, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imekuwa mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha, faraja na matumaini kwa watu wanaoishi pembezoni mwa jamii; kwa kuthamini na kudumisha utu wao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni Jumuiya ambayo imeendelea kujizatiti katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano katika jamii.

Shukrani za pekee zimwendee Professa Andrea Riccardi, muasisi wa Jumuiya hii aliyejisadaka katika ujana wake na hivyo kuwa ni chachu ya mageuzi ya kijamii, ambayo yamekuwa ni endelevu hadi wakati huu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu! Changamoto hii inaendelezwa pia na Professa Marco Impagliazzo, Rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ambaye pia anapongezwa sana Chancellor Angela Merkel wa Ujerumani katika barua yake kwa viongozi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inayoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Professa Andrea Riccardi akiwa na umri wa miaka 18 akiwa na vijana wenzake, waliamua kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maboresho ya wananchi wengi ndani na nje ya Roma; kwa kuzivalia njuga changamoto mamboleo zilizoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yaani: majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mataifa. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ikajikita pia katika majadiliano ya kitamaduni na maboresho ya sekta ya elimu ili kupambana na ujinga, magonjwa na umaskini unaonyanyasa ut una heshima ya binadamu!

Chancellor Angela Merkel anasema, kwa njia ya mradi wa “The DREAM na BRAVO” kwa nchi zinazoendelea imesaidia sana katika mchakato wa maboresho ya afya ya mama na mtoto kwa kudhibiti maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto, mradi ambao unaendelea kupata mafanikio makubwa Barani Afrika. Mradi wa BRAVO unapania kuwalinda watoto wadogo kwa kuwaandikisha na kuwapatia nafasi ya kupata masomo katika “shule za amani” ili hatimaye, waweze kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita anasema Chancellor Angela Merkel Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imejipatia umaarufu mkubwa katika Jumuiya ya Kimataifa; kwa watu wa dini na imani mbali mbali bila kuwasahau  maskini na watu wa kawaida ambao wameonja huduma ya upendo kutoka katika Jumuiya hii. Anahitimisha ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 kwa kusema, kwamba, ataendelea kushirikiana nao katika kutekeleza dhamana, wajibu na utume wao kati ya maskini pamoja na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.