Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Shirika la Madonda Matakatifu kuzeni: Udugu, ibada na huduma!

Papa Francisko analitaka Shirika la Madonda Matakatifu kudumisha maisha ya kijumuiya, ibada kwa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu na Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

12/02/2018 09:17

Baba Mtakatifu Baba Mtakatifu Francisko analitaka Shirika la Madonda Matakatifu lililoanzishwa kunako mwaka 1816 na Mtakatifu Gaspar Bertoni, huko Verona, Kaskazini mwa Italia, kuhakikisha kwamba, linawasha ndani mwake moto wa Neno la Mungu, ili uweze kuwafikia na kuwagusa wale wote wanaoishi pembezoni mwa jamii na ulimweguni katika ujumla wake. Huu uwe ni moto mzuri unaofumbatwa katika utakatifu wa maisha; uwe ni moto wa upendo, unaogusa nyoyo za watu, kwa kuheshimu uhuru pamoja na kuwapatia watu muda wa kuweza kumwongokea Mwenyezi Mungu na wala si moto wa ghasia na vurugu.

Baba Mtakatifu katika hotuba aliyoitoa mubashara, Jumamosi, tarehe 10 Februari 2018 alipokutana na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Madonda Matakatifu, aliwataka kukuza na kudumisha udugu katika maisha ya kijumuia, sala, uhuru na ukweli pasi na unafiki; Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, iwe ni chemchemi ya huruma na upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu. Anasema, Mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu uwasaidie kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa!

Baba Mtakatifu anasema, maisha ya kijumuiya ni toba ya hali ya juu kabisa kama anavyokaza kusema Mtakatifu John Berchmans kwa lugha ya Kilatini kwamba,  “mea maxima poenitentia, vita communis”. Si rahisi sana kwani huu ni uhalisia wa maisha ya watu unaogusa matatizo, fursa na changamoto mbali mbali za maisha. Kuna wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko; mashindano ambayo watu wanataka kujikuza na kujiona bora zaidi kuliko wanajumuiya wengine; hali ya kutoelewana, kinzani na misigano ya kibinadamu. Yote haya yanaendelea kujengeka taratibu katika nyoyo za watu, kiasi hata cha wanashirika kushindwa hata kusalimiana kama ndugu katika Kristo Yesu.

Maisha ya kidugu katika jumuiya yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika sala, kwa kuombeana, kusaidiana na kutegemezana kwa hali na mali kwani, hakuna maisha pasi na mikwaruzano, kama haya yanaweza kutokea katika familia na maisha ya watu wa ndoa, sembuse watawa wanaokutanishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Daraja takatifu, ili kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani? Baba Mtakatifu anakaza kusema, kukosa na kukoseana ni jambo la kawaida katika maisha ya pamoja, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu wa maisha, pasi na kubaki na kinyongo moyoni. Watawa wajifunze kusema na kushuhudia ukweli wa mambo bila woga, kielelezo makini cha ukomavu na uhuru kamili!

Masengenyo na unafiki ni sumu mbaya inayopekenyua hata kuua maisha ya kijumuiya. Watawa wawe na ujasiri wa kushirikishana shida, mang’amuzi, uzuri na changamoto wanazokumbana nazo katika nadhiri zao, yaani: ufukara, useja na utii, kama kielelezo cha ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu! Watawa wawe ni nidhamu ya kuheshimu utu na heshima ya ndugu zao katika utawa na kamwe wasimpatie Shetani nafasi ya kuchafua utu na heshima ya ndugu zao katika Kristo!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, iwe ni chemchemi ya huruma na upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu wanaowahudumia, kama alivyothubutu kusema Mtakatifu Bernardo. Watawa wawe na ujasiri wa kukimbilia na kujificha katika Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, kwa njia ya toba, wongofu wa  ndani, maisha ya sala na Sakramenti za Kanisa. Watawa wasikubali kupigishwa magoti na dhambi zao, bali wawe na ujasiri wa kusimama tena na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, daima wakiongozwa na Neno la Mungu linalowakumbusha kwamba, Kristo Yesu aliteswa na kufa Msalabani, ili kuzichukua dhambi za walimwengu, ili wafuasi wake wawe hai kwa mambo ya haki kwani kwa kupigwa kwake wao wameponywa!

Watawa wajenge na kukuza Ibada kwa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, kimbilio na faraja yao wakati wa shida na magumu ya maisha! Wajifiche huko dhidi ya hasira ya Mungu kutokana na dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu! Madonda Matakatifu yawe ni chemchemi ya Ibada kwa huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, Mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu uwasaidie kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa katika huduma ya upendo kama alivyofanya Bikira Maria kwa binamu yake Elizabeth.

Mtakatifu Yosefu alijipambanua kuwa ni mtendaji hata katika ukimya wake; mtu mwenye haki asipenda makuu; aliyemfundisha Yesu stadi za maisha; kwa hakika alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti, mchaji wa Mungu na daima alionesha hofu ya Mungu katika maisha yake. Baba Mtakatifu anawaalika watawa kujenga na kudumisha Ibada kwa Mtakatifu Yosefu na kwa Bikira Maria katika safari ya maisha yao hapa duniani. Katika shida, hofu na mashaka ya maisha na utume, watawa daima wakimbilie ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa kutambua kwamba, kwa pamoja wanaunda na kujenga Jumuiya ambayo ni sehemu ya familia ya Mungu. Ibada kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu si kwa ajili ya watoto wadogo parokiani, bali ni Ibada inayopaswa kudumishwa na waamini wote, watawa wakiwa mstari wa mbele!

Baba Mtakatifu anasema, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kwa: ari, unyenyekevu na furaha kama alivyofanya Mtakatifu Gaspar Bertoni na kwamba, huu ndio mtindo wa uinjilishaji uliotekelezwa na Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu. Daima aliwaendea na kuwakaribia watu; akawaonjesha wema na huruma ya Mungu kwa njia ya ukweli wa Neno la Mungu. Hii ndiyo changamoto kwa Wamissionari wa Shirika la Madonda Matakatifu kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kuandamana na kumwambata Kristo Yesu na kwa njia ya ushuhuda wa furaha ya Injili inayomwilishwa katika maisha. Ili kudumu katika dhamana na utume huu, kuna haja ya kujikita katika uvumilivu na ushuhuda wa ukweli wa Injili. Waendelee kubatiza kwa moto wa Roho Mtakatifu unaofumbata upendo unaobubujika kutoka katika Msalaba wa Kristo Yesu ili kutakasa nyoyo za watu. Kwa sasa Shirika la Madonda Matakatifu lina jumla ya wanashirika 400 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi 15 duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/02/2018 09:17