2018-02-12 09:36:00

Mt. Bakhita ni kielelezo cha mapambano dhidi ya utumwa mamboleo!


Kila mwaka ifikapo tarehe 8 Februari Mama Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya Mt. Josephina Bakhita. Huyu binti alizaliwa mnamo mwaka 1869 huko maeneo ya Darfur nchini Sudan. Akiwa angali na umri wa miaka 7 alitekwa nyara na kuuzwa kama mtumwa. Jospehina Bakhita aliuzwa mara kadhaa katika biashara ya utumwa chini ya waarabu katika masoko ya  El Obeid na Khartoum. Baadae alinunuliwa na Bwana Callisto Legnani, mwanadiplomasia wa Italia aliyekuwa akiishi Khartoum. Bwana Callisto Legnani alikuwa ananunua watoto waliokuwa wakiuzwa kama watumwa, ili awaweke huru na kuwarudisha katika familia zao. Hata hivyo kwa Josephina Bhakita haikuwa rahisi kumrudisha kwa familia yake, kwani binti huyu alikuwa hakumbuki jina lake, familia yake wala kijiji alikotoka, kufuatia mshtuko, trauma, alioupata kutokana na nyanyaso za kimwili na kiakili. Jina Bakhita alipewa na waarabu wafanyabiara wa utumwa, neno linalomaanisha “Bahati”.

Baadae Bwana Callisto Legnani aliporudi nchini Italia mnamo mwaka 1884, alilazimika kwenda naye, ambako Josephina Bakhita alijiunga na Shirika la Mabinti wa Upendo maarufu kama Masista Wakanosa na kuwa mtawa. Josephina Bakhita alifariki tarehe 8 Februari 1947. Tarehe 17 Mei 1992 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimtangaza kuwa Mwenye heri na mnamo tarehe 1 Oktoba 2000 akamtangaza kuwa Mtakatifu, ambapo kumbukumbu yake huadhimshwa tarehe 8 Februari kila mwaka. Lengo la kuadhimisha kumbukumbu hii ni pamoja na kuombea harakati za kutetea haki za wale wote wanaotendewa kama watumwa na kupiga vita biashara haramu ya binadamu. Utumwa mamboleo unavuka mipaka na haujali umri, hadhi wala jinsia. Utumwa mamboleo unajumuisha biashara ya ngono, nyanyaso za kijinsia, kazi za shuruti kwa watoto wadogo, watoto kutumika kama askari wa silaha, ndoa za kulazimisha pamoja na bisahra ya viungo vya binadamu. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha takribani milioni 43 ya utumwa wa namna hii, wakati kwa miaka mitano iliyopita takwimu zinaonesha walioathirika na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni 89 milioni.

Vita dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo inagusa nchi zote duniani na kuathiri kwa kasi nchi maskini zaidi. Kati ya mahali ambako janga hili linatisha kwa kuchukua kasi zaidi ni pamoja na nchi ya Libya ambako Kamera za kituo cha Luninga cha CNN mwaka 2017 zilishuhudia hayo ambapo wahamiaji walilazimshwa kulipa fedha ili kusafirishwa kuelekea barani Ulaya; mwaka huo huo Shirika la Habari la Reuters lilitoa taarifa kwamba askari wa ulinzi na usalama wa mipaka nchini Thailand wanashirikiana na wafanyabiashara haramu ya binadamu kwa kuuza Wakimbizi na Wahamiaji wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar. Wakiisha kufika Thailand, wanawake huozeshwa kwa wenye tabia ya ngono holela, wakati wanaume hutumikishwa bure kwenye mashamba au viwanda vya uvuvi. Takwimu za Jumuiya ya kimataifa zinaonesha hata Amerika ya kusini kuna takribani watu milioni 2 wanaoshurutishwa kazi za suluba, na kati ya nchi zenye sifa hiyo mbaya ya utumwa mamboleo barani humo ni Haiti na Jamhuri ya Wadominikani. Kwa maeneo haya, sababu kubwa ya utumwa mamboleo ni biashara haramu ya dawa za kulevya.

Na Padre Celestine Nyanda.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.