Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inajikita katika Neno, Maskini na Amani

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1968.

12/02/2018 09:59

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, yenye makao yake makuu mjini Roma, ilianzishwa rasmi tarehe 7 Februari 1968 kwa kujikita katika Sala, Maskini na Amani duniani; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 10 Februri 2018 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano,  kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio.

Hili ni tukio ambalo limehudhuriwa na idadi kubwa ya Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, mabalozi na viongozi wa Serikali ya Italia ambayo inashirikiana kwa karibu sana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio hasa kwa huduma ya maskini, wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” ambao ndio walengwa wakuu wa Jumuiya hii. Kardinali Pietro Parolin katika mahubiri yake amesema, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yaliyoiwezesha Jumuiya hii kukita maisha na utume wake katika Neno la Mungu, linalosomwa na kutafakariwa kila siku kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria wa Trastevere na sehemu mbali mbali za dunia!

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imeendeleza huduma ya uponyaji iliyoanzishwa na Kristo Yesu kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kuwarejeshea tena: utu na heshima yao kama binadamu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu alipomponya yule mgonjwa wa Ukoma, aliyekuwa ametengwa na jamii yake. Neno la Mungu linalomwilishwa katika Injili ya huduma kwa maskini limeendelea kushuhudiwa Barani Afrika kwa njia ya Mradi wa “The DREAM” kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto, huduma ambayo imeanza kuzaa matunda ya matumaini.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio anasema, Kardinali Parolin, imekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kutafuta, kujenga na kudumisha amani duniani, kwa kuwasaidia watu wa Mungu kujenga imani na matumaini katika amani na utulivu kama kikolezo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya hii imekuwa ni msaada mkubwa kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Siria na Pembe ya Afrika pamoja na kuwasaidia kuganga na kutibu majeraha yao, kielelezo makini cha huruma na upendo wa Kristo kwa maskini, changamoto endelevu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imeendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa, huduma inayotekelezwa katika hali ya unyenyekevu mkubwa, sanjari na mchakato wa kupambana na umaskini duniani. Kardinali Parolin anakaza kusema, katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya wengine, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ni zawadi kubwa kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto na mwaliko wa kupokea zawadi hii na kuimwilisha katika umoja, mshikamano na udugu, daima wakijitahidi kumwiga Kristo Yesu katika maisha na utume wake, ili kazi ya ukombozi iweze kuwafikia watu wengi zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/02/2018 09:59