2018-02-10 16:23:00

Wamissionari washeni moto wa imani na huduma kwa maskini duniani


Shirika la Madonda Matakatifu lilianzishwa kunako mwaka 1816 na Mtakatifu Gaspar Bertoni, huko Verona, Kaskazini mwa Italia. Kwa sasa lina jumla ya wanashirika 400 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi 15 duniani. Jumamosi, tarehe 10 Februari 2018, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na washiriki wa mkutano mkuu wa Shirika la Madonda Matakatifu na kuwashukuru kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbali mbali za dunia sanjari, na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vijana wa kizazi kipya, utume wanaoutekeleza kwa kushirikiana pia na wakleri wa majimbo.

Baba Mtakatifu anawataka wanashirika hawa kuhakikisha kwamba, wanawasha ndani mwao moto wa Neno la Mungu, ili uweze kuwafikia na kuwagusa wale wote wanaoishi pembezoni mwa jamii na ulimweguni katika ujumla wake. Huu uwe ni moto mzuri unaofumbatwa katika utakatifu wa maisha. Si kama ule moto ambao Yakobo na Yohane walikuwa wanamwomba Kristo Yesu, ili ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize Wasamaria ambao hawakuwa tayari kupokea Habari Njema ya Wokovu. Moto anaotaka Mwenyezi Mungu uwashukie watu ni moto wa upendo, unaogusa nyoyo za watu, kwa kuheshimu uhuru pamoja na kuwapatia watu muda wa kuweza kumwongokea Mwenyezi Mungu na wala si moto wa ghasia na vurugu

Baba Mtakatifu anasema, Injili inatangazwa na kushuhudiwa kwa: ari, unyenyekevu na furaha kama alivyofanya Mtakatifu Gaspar Bertoni na kwamba, huu ndio mtindo wa uinjilishaji uliotekelezwa na Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu. Daima aliwaendea na kuwakaribia watu; akawaonjesha wema na huruma ya Mungu kwa njia ya ukweli wa Neno la Mungu. Hii ndiyo changamoto kwa Wamissionari wa Shirika la Madonda Matakatifu kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa kuandamana na kumwambata Kristo Yesu na kwa njia ya ushuhuda wa furaha ya Injili inayomwilishwa katika maisha. Wanashirika wakumbuke daima kwamba, si kila wakati Habari Njema ya Wokovu itaweza kupokelewa kwa mikono miwili, kwani wakati mwingine, inakataliwa, inazuiliwa, kudhulumiwa na hata wakati mwingine kuuwawa. Ili kudumu katika dhamana na utume huu, kuna haja ya kujikita katika uvumilivu na ushuhuda wa ukweli wa Injili. Waendelee kubatiza kwa moto wa Roho Mtakatifu unaofumbata upendo unaobubujika kutoka katika Msalaba wa Kristo Yesu ili kutakasa nyoyo za watu.

Huu ndio moto wa Roho Mtakatifu ulioshuka wakati wa Siku kuu ya Pentekoste na kwamba, kila mtu atatiwa chumvi kwa moto; huu ndio moto wa majaribu; moto wa upendo wa kidugu unaounda na kujenga Jumuiya inayotumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati yao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia sana ushuhuda wa upendo wa kidugu unaotolewa na wamissionari, kama kielelezo cha moto wa Roho Mtakatifu. Vinginevyo, Jumuiya za wamissionari zitapigwa na ubaridi, kuandamwa na giza pamoja na upweke hasi. Moto wa upendo wa kidugu ni mwanga unaowawezesha wamissionari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu na hivyo kuwa ni kivutio cha miito miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili kushiriki katika utume wa uinjilishaji. Watambue kwamba, kuna watu wanahitaji kuwashiwa tena moto wa imani, ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kama Shirika wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa maskini, wasiopendwa wala kuthaminiwa; wanaoteseka na kujikatia tamaa; wafungwa na watu wasiokuwa na makazi maalum; wakimbizi na wahamiaji hasa wale wanaokimbia vita.

Wanashirika wawe tayari kushirikiana na waamini walei ili kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo, kwa kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa Injili ya familia; kwa kuwajengea matumaini vijana wa kizazi kipya, ili waweze kuthamini maisha. Wawe ni wamissionari wenye furaha, wema na watakatifu ambao wako tayari kukutana na watu mbali mbali katika utume na maisha yao, tayari kuwasaidia Maaskofu mahalia kutangaza na kushuhudia Injili. Umissionari ni utambulisho wao unaowataka kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, kwa kutafakari uso wake katika sala, kwa kumtambua na kumhudumia kwa upendo miongoni mwa wale wote wanaokutana nao katika maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawatakia heri na baraka ili kwamba, Roho Mtakatifu awashe moto wa huduma na mshikamano wa uaminifu kwa Kristo na Injili yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.