Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Rushwa na ufisadi vinawapekenya sana wananchi wa Afrika ya Kusini

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini lina mshauri rais Jacob Zuma kufanya maamuzi magumu ya kung'atuka kutoka madarakani kwa ajili ya mafao ya umma kwani kwa sasa hali ni tete sana nchini Afrika ya Kusini. - REUTERS

10/02/2018 17:26

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya kusini (SACBC) linamwaalika Rais Jacob Zuma kutafakari na kufanya maamuzi sahihi kama mtu mzima mwenye busara na kwa ajili ya mafao ya taifa lake. Mwaliko huu wa Maaskofu nchini humo unatolewa kufuatia shinikizo analowekewa Rais Zuma kutoka ndani ya chama chake mwenyewe ili ajiudhuru kabla ya muda wake kuisha, ambayo ingekuwa mwishoni mwa mwaka 2019. Wakati huo huo, maaskofu katika ujumbe wao wanawaalika wale wote wanaohusika kufanya maamuzi kiserikali, kisiasa, au kijamiii kufanya hivyo kwa umakini, utulivu na uvumilivu mkubwa.

Kamati tendaji ya Chama cha African National Congress (ANC), ambacho ni chama tawala cha Rais Zuma, Siku ya Jumatano tarehe 7 Februari imeitisha kikao cha dharura na kunuia kumshinikiza Rais Jacob Zuma kujiudhuru na kupisha taratibu zingine za mchakato wa uchaguzi mkuu kabla ya muda wake. Shinikizo hilo linakuja kufuatia uozo wa rushwa na kashfa zinazomkumba Rais Zuma na serikali yake, na hivyo kupelekea kushuka vibaya sana kwa hali ya uchumi nchini humo. Asilimia 30 ya wananchi hawana kazi na wanaishi katika hali isiyo na uwiano kijamii; na wakati huo huo ni asilimia 10 tu ya mafisadi fulani inayotumia asilimia 66 ya utajiri wa nchi hiyo. Heshima na nguvu ya Rais Zuma vimeyumba tangu mwezi Desemba 2017 ambapo nafasi yake kama Mwenyekiti wa chama chake cha African National Congress (ANC), ilichukuliwa na aliyekuwa msaidizi na mpinzani wake mkubwa ndani ya chama, Bwana Cyril Ramaphosa, ambaye katika kinyang’anyilo hicho alimbwaga vibaya Bi Nkosazana Dlamini-Zuma, mke wa Rais Zuma. 

Askofu Abel Gabuza wa Jimbo Katoliki la Kimberly ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Maaskofu ya haki na amani nchini humo anasema, Jamii ya Afrika ya kusini inahitaji utamaduni wa kweli wa kitaifa na huduma kwa jamii unaojikita katika mafao ya wengi. Askofu Gabuza anasisitiza kwamba, ANC ni chama tawala, hivyo chochote kinachotokea ndani ya chama hicho, kinaathiri moja kwa moja serikali na taifa hilo kwa ujumla. Kuna watendaji wengi wa serikali na umma ambao hawana vigezo wala uwezo na bado wanashika nafasi za muhimu nchini humo, eti kwa sababu tu ni wanachama wa ANC. Askofu Abel Gabuza anasema umefika wakati zichukuliwe hatua madhubuti na za uungwana kwa uchungu wa taifa hilo, ili kuhakikisha wanapatikana watendaji wenye vigezo na uwezo wa kuitoa nchi yao kwenye myumbo wa maadili na maendeleo, kisha kuanza safari mpya ya ukombozi wa taifa lao.

Hali tete iliyomo ndani ya chama cha ANC, imepelekea misukosuko na sintofahamu kutoka kwa wapinzani kiasi cha kuanzisha maandamano katika miji mbali mbali nchini Afrika ya kusini. Miondoko hii inaashiria harufu mbaya ya kuchafuka kwa amani nchini humo. Hivyo maaaskofu wanasema, iwapo hali hiyo haitapatiwa ufumbuzi wa haraka wenye kuzingatia haki na amani, itakuwa ni sumu ya hatari itakayoitesa nchi ya Afrika kusini kwa vizazi vingi siku za usoni. Kwa ufupi, hali tete ya wananchi wa Afrika ya kusini inatokana na myumbo wa kisiasa; ukosefu wa uwiano katika matumizi ya rasilimali ambayo ni haki ya raia wote; kuongezeka kwa matabaka katika jamii; na umaskini unaokithiri. Maaskofu wa Afrika kusini wanawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuombea haki na amani nchini humo, wakati chama tawala kikitafuta suluhu ya haraka kwa ajili ya mafao wengi.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

10/02/2018 17:26