2018-02-10 08:26:00

Iweni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa


Amri kuu ni kumpenda Mungu kwa moyo na kumpenda jirani kama ujipendavyo – Mt. 22:37-40. Yesu aliifanya amri hii mali yake kabisa na akaiboresha. Alitaka kujifananisha kabisa au kuwa yule jirani aliposema kile umtendeacho mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, wanitendea mimi – Mt. 25:40. Historia ya maisha ya Mt. Martin wa Tours yaweza kutupa changamoto kubwa leo na pengine kurahisisha tafakari yetu ya neno la Mungu siku ya leo. Akiwa askari kijana alimsaidia maskini mkoma. Alipomwona huyu maskini tena mgonjwa na mwenye baridi kali na kwamba alihitaji msaada, alipasua koti lake la kijeshi vipande viwili. Ushujaa huu ulimtia matatani kama askari, kuharibu mali ya jeshi, lakini ulibadilisha maisha yake. Katika ndoto usiku ule alimwona Kristo akiwa amejifunika nusu koti huku akimwambia malaika aliyekuwa karibu yake, leo Martin amenifunika na koti lake. Tendo hili likabadilisha maisha yake na leo hii tunazungumza juu ya Mtakatifu Martin wa Tours.

Katika Hes. 12 tunasoma habari ya Miriam dada yake Musa, juu ya habari ya ukoma wake kwa sababu ya tabia yake mbaya ya kulalamika dhidi ya Musa kwa kumchukua yule mwanamke Mkushi. Yeye na Haruni wakawa na wasiwasi kama kweli Bwana anaongea na Musa. Wakaadhibiwa na Mungu. Musa anamuombea msamaha kwa Mungu na anapona.  Pia katika kitabu cha Ayubu, tunasikia anapoteza mali yake yote lakini imani yake kwa Mungu ilibaki imara. Katika macho ya watu yaonekana kwamba wenye dhambi na waliadhibiwa.  Katika sura 13 ya kitabu cha Walawi na ambapo somo la kwanza la leo latoka, hali ya ukoma yaonekana kama mapenzi ya Mungu.

Katika Agano Jipya na hasa katika injili hali ni tofauti kabisa. Jinsi Yesu anavyolikabili jambo hili ni tofauti kabisa na mitazamo ya watu. Yesu anamkaribia mgonjwa na kule kuwa naye karibu kunampa yule mgonjwa nafasi ya kusema shida yake – ukitaka waweza kuniponya. Naye Yesu anasema nataka – Mk. 1:40-41. Kwanza anamponya na ukoma na pili anaonesha kuwa ukoma siyo adhabu toka kwa Mungu. Kwa tendo hili Yesu anaweka mwisho dhana iliyotawala kuwa mwenye ukoma na pia aina yo yote ile ya ugonjwa ilikuwa ni adhabu toka kwa Mungu. Katika tendo hili ukoma unabaki kuwa kama aina yo yote ile ya ugonjwa ambayo inamzuia mtu kuwa mzima kama ambavyo Mungu anapenda. Kama ukoma au ugonjwa ungekuwa ni adhabu toka kwa Mungu, basi Yesu angekuwa ameenda kinyume na utendaji wa Baba yake.

Kwetu sisi iwe changamoto – mfano wa Yesu ni changamoto kubwa kwetu – kwanza kuwa karibu na watu, kuondoa dhana potofu na chafu zinazoendekeza magonjwa mbalimbali – kama vile unyanyapaa n.k. Ipo miongoni mwetu tabia ya kujitenga na watu tunaodhani au tunaowasema kuwa wana dhambi au aina fulani ya magonjwa. Tunajitenga nao na kwa sababu hiyo tunawaongezea maumivu zaidi. Tendo la Yesu kunyosha mkono na kumgusa yule mkoma linatoa changamoto iliyopo kati ya dhana ya mtakatifu na mdhambi. Ni upi ukoma wetu na katika mazingira yetu leo?  Hakika bado upo na kwa namna nyingi na tofauti.

Mahatma Ghandi angekuwa mkristo. Alisoma Biblia na kuielewa vizuri sana. Akafanya maamuzi kwenda kanisani siku moja huko Afrika Kusini. Alipofika eneo la Kanisa akakuta kuna Kanisa la wazungu, waafrika na watu mchanganyiko. Bila kujua utaratibu huo akataka kuingia Kanisa la wazungu. Alizuiliwa mlangoni na askari mzungu na kuoneshwa kanisa la waafrika. Huo ukawa mwisho wa mapenzi yake kwa ukristo na akarudi nyumbani.  Mtakatifu Teresa wa Avila anasema kuwa ingawa hatuna Bwana wetu kati yetu katika hali ya kimwili, tunaye jirani, ambaye kwa ajili ya upendo na matendo mema, ni mzuri kama angekuwa Bwana wetu mwenyewe.

Ile habari ya Msamaria mwema inatupatia swali kubwa – jirani yako ni nani. Ingefaa leo kuongeza ufahamu huu bila kuharibu maana ya biblia na kujiuliza mimi ni jirani ya nani? Lakini hii isibaki tu kutaja jirani zako ila iwe katika kujiuliza umefanya nini kwa ajili ya jirani yako.  Mhubiri maarufu Padre Munachi anatumia mfano huu ambao binafsi unanipa changamoto kubwa akisema; Jamani – mkulima maarufu na mcha Mungu akiwa anasali pamoja na mwanae jioni moja alisali hivi; tuombe kwa ajili ya maskini yule pale barabarani ili Bwana amjalie mahitaji yake. Mara moja mwanae akaingilia kati na kumwambia baba yake – baba tusimsumbue Mungu bure. Tunaweza sisi kumpatia mahitaji yake maskini yule. Sisi tuchukue nafasi ya Mungu kwani ametujalia haya tuliyo nayo.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa mwaka huu, Jumapili tarehe 11 Februari 2018 inaongozwa na kauli mbiu “Mama tazama mwanao. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake”. Baba Mtakatifu anataka mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa kuhakikisha kwamba, inazingatia kwanza kabisa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu: wito wa Mama Kanisa wa huduma kwa wagonjwa na maskini; kumbu kumbu endelevu ya historia ya huduma kwa wagonjwa sanjari na nguvu ya uponyaji inayoonesha uhusiano uliopo kati ya utume wa uponyaji na mwamko wa imani kwa wagonjwa wanaokutana na Kristo Yesu, wakiomba huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huduma ya uponyaji inayotekelezwa na Kristo Yesu kwa wagonjwa mbali mbali inahitaji jibu la imani thabiti kutoka kwa wahusika.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linaendelea kupyaisha huduma kwa wagonjwa sanjari na kujikita katika uaminifu kwa amri iliyotolewa na Kristo Yesu mintarafu mng’ao wa mwanga wa utukufu wa Fumbo la Msalaba. Kwani hili ni fumbo la matumaini, huruma na upendo usiokuwa na kikomo. Ikumbukwe kwamba, fadhila ya upendo ni msingi wa maisha ya kila mfuasi wa Kristo na Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Kristo kwa waja wake. Katika hija ya maisha yao hapa duniani, wafuasi wa Kristo watambue kwamba, wanasindikizwa, wanalindwa na kutunzwa na Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Hii ndiyo changamoto ambayo Wakristo wanapaswa kuivalia njuga kwa kumwilisha Injili ya upendo inayowataka kuhudumiana kwa dhati! Kwa njia hii, wakristo wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mama Kanisa katika maisha na wito wake, daima amekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, historia ambayo kwa hakika inapaswa kuwa endelevu. Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yameendelea kutoa huduma kwa wagonjwa hasa vijijini ambako bado huduma za afya zinasuasua. Mashirika haya yamekuwa yakitoa huduma bora, daima mwanadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Hospitali na taasisi za afya zimeendelea kufanya tafiti mbali mbali ili kuboresha tiba na huduma kwa wagonjwa, lakini maadili ya kikristo yamepewa msukumo wa pekee.  Kanisa limeendelea kusimama kidete katika kuchangia maboresho ya afya ya mama na mtoto kwa kupunguza vifo vya watoto wadogo; kwa kukinga na kutibu magonjwa mbali mbali. Kwa maneno mafupi, Kanisa daima limekuwa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano dhidi ya magonjwa kwa kuwasaidia wale waliojeruhiwa katika maisha!

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.