Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Boresheni miundo mbinu na teknolojia daima mkizingatia huduma makini

Papa Francisko analitaka Shirika la Posta Italia kuboresha sera, mikakati na miundo mbinu daima likiendelea kua aminifu kwa lengo msingi ambalo ni huduma makini kwa wananchi wa Italia.

10/02/2018 16:40

Shirika la Posta la Italia lina uhusiano wa dhati kabisa na maisha pamoja na historia ya nchi ya Italia, tangu pale umoja wa kitaifa ulipopatikana nchini Italia. Ni shirika ambalo limeendelea kuziunganisha familia na watu sehemu mbali mbali za dunia; kwa kubadilishana habari, huduma na biadhaa, kiasi cha kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi, yanayohitaji kwa kiasi kikubwa ufanisi na huduma bora zaidi. Shirika limeendelea kujipyaisha kwa kusoma alama za nyakati, kiasi hata cha kuweza kujiingiza katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Italia, kwa kuanzia katika vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya teknolojia hali ambayo imesababisha mabadiliko makubwa katika mawazo na mitindo ya maisha ya watu, kiasi cha kuhitaji ufanisi mkubwa zaidi wa huduma na bidhaa zinazozalishwa. Shirika la Posta, likaliona jambo hili na kuanza kujikita katika uwekezaji unaojielekeza zaidi katika mchakato wa kukidhi mahitaji ya siku zijazo kwa kufanya tafiti na upyaisho wa teknolojia unaozingatia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na matumizi bora ya rasilimali ya dunia!

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 10 Februari 2018 wakati alipokutana na kuzungumza na viongozi pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Posta la Italia. Amekazia umuhimu wa Shirika kujikita katika mafunzo kazini pamoja na kuendelea kuboresha mbinu na mikakati ya kazi, daima wakiwa waaminifu kwa lengo lao asilia, yaani huduma kwa wananchi wa Italia, badala ya kutaka kupata faida kubwa. Utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza kwani watu ndio utajiri mkubwa na rasilimali inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wala si kichokoo cha kuchezea na hatimaye kutupwa nje!

Huduma kwa wateja iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana; kwa wafanyakazi kuhakikisha kwamba wanatoa huduma makini bila kuwatwisha wateja mzigo wa shida na mahangaiko ya majumbani mwao! Wafanyakazi wajenge mahusiano mema na wafanyakazi wenzao, kwa kusikilizana, kuwajibikiana na kuheshimiana; mambo yanayojenga na kukuza tija na ufanisi kazini. Wafanyakazi wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kwa kujenga na kudumisha amani na utulivu.

Shirika la Posta la Italia limekuwa likitoa kipaumbele cha pekee cha huduma kwa wateja wake na kwamba, umefika wakati pia wa kuwaangalia wafanyakazi wake kwa kuangalia mahitaji msingi ya wafanyakazi wanawake wanaonyonyesha watoto wachanga; familia za wafanyakazi na mahitaji yake msingi; mambo msingi sana katika mchakato wa maboresho ya mazingira ya kazi; kwa kuheshimu haki msingi za wafanyakazi pamoja kuwapatia mshahara unaokidhi mahitaji yao msingi.  Bajeti ya kampuni isiwe ni kikwazo cha mchakato wa maboresho ya kazi na huduma inayotolewa. Shirika lijitahidi kuwa karibu zaidi na wateja wake na hasa maskini na wanyonge zaidi, ili kuwa ni mahali pa rejea katika shida na mahangaiko yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

10/02/2018 16:40