2018-02-10 17:44:00

Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu


Zaidi ya asilimia 70% ya wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni wanawake na mabinti, kati yao theluthi moja ni watoto wadogo. Hii hali ya unyonyaji, unyanyasaji, na mateso ya wanyonge hawa kimwili na kiakili ni aibu na kashfa kubwa kwa jamii ya leo inayoonekana hata kutojali kabisa ni nini kinatokea kwa watu hawa. Sauti iliyojaa huzuni ya Kardinali Pietro Parolin wakati ya Omelia yake mnamo tarehe 8 Februari 2018, kumbukumbu ya Mtakatifu Josephina Bakhita, katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati wa kikao cha kikundi cha Mt. Martha Kimataifa, Taasisi dhidi ya biashara haramu ya binadamu.

Ibada ya Misa ilihudhuriwa na wanaume na wanawake wapigania haki, mahakimu, askari wa vikosi vya ulinzi na usalama, na watendaji wa huduma mbalimbali za binadamu, hususani wapiga vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu. Kardinali Parolin amewaalika kutafakari hali ya wahanga wa biashara hiyo haramu, huku wakijiuliza maswali: ni jinsi gani wataweza kuwakomboa wahanga hao kutoka katika utumwa huo?; ni namna gani wataweza kuzuia wasianguke tena katika janga hilo?; na ni kivipi wataweza kuhakikisha janga hili la biashara haramu na utumwa mamboleo linatokomezwa na haliibuki tena?!. Hii ni biashara haramu, ya kinyama na ukatili mkubwa, ambayo ni moja ya pepo waovu wanaotesa na kunyanyasa Familia ya binadamu kwa nyakati hizi (Rej. Marko 7: 24-30). Hali hii haiwezi kufumbiwa macho hata kidogo, na wala waamini wakristo hawakati tamaa kukabiliana na changamoto zozote zinazoibuka duniani, kwani wanafahamu wazi kwamba Kristo amekwisha shinda utumwa wa dhambi na mauti, Naye anawaalika waamini kuwa na matumaini: nimewaambia mambo haya ili mpate kua na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko, lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu (Rej., Yohane 16: 33).

Ni mwaliko wa Kristo kuwahangaikia wanyonge na wale wote wanaonyanyaswa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kiasi cha kuonekana na kutumika kana kwamba ni bidhaa na sio binadamu wanaostahili heshima ya utu wao. Kardinali Parolin anasema ni lazima kupambana kufa na kupona kuhakikisha uovu unapigwa vita, na kutokomeza kabisa tabia chafu na tamaduni za kutojali binadamu kwa kukodolea jicho faida na maslahi binafsi, kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francisko. Hawa wote wanaonyanyaswa na kudharirishwa utu wao, bado machoni pa Mwenyezi Mungu wana thamani kubwa. Ni lazima kila mmoja kutulia na kutafakari kwa kina hali za watu hawa wanaolazimika kuishi maisha yanayodharirisha utu wao, na kisha kujitosa kadiri ya nafasi kuwakomboa kutoka hali hiyo. Kuna wahamiaji wengi wanaokimbia nchi zao kutokana na kinzani za kisiasa, kijamii, vita ghasia na baa la njaa; tumaini pekee wanalokuwa wamebaki nalo ni kutafuta hifadhi katika nchi za kigeni. Cha kusikitisha ni kwamba wanapofika katika nchi wanakotarajia kupata hifadhi na unafuu wa maisha, ndipo wanapopambana na mengine tena.

Baba wa familia wanalazimika kufanya kazi zisizojali utu na heshima yao, na wanalipwa chini ya kiwango au hawalipwi kabisa ujira wanaostahili. Watoto wadogo wanalazimika kuwa omba omba mitaani na wengine kufanyiwa ngono haramu. Wanawake wanajikuta barabarani wakifanyiwa biashara haramu ya ngono ikiwa ni pamoja na filamu za ngono; wakati huo mabinti wengi wanalazimishwa kuolewa na vibabu sukari. Wengi wa vijana wanahadaika na wanachukuliwa viungo vyao vya mwili na vinaingizwa kwenye biashara ya viungo vya binadamu. Hawa wote mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu bado wana thamani kubwa anasema Kardinali Parolin.

Pale ambapo binadamu anakengeuka na kumwacha Mwenyezi Mungu hata kuanza kuabudu miungu mingine kama fedha, madaraka, au tamaa za kimwili, Mwenyezi Mungu bado huinua wanawake na wanaume walio waaminifu kwake na wanaoshirikiana na Neema yake ili kuufanikisha mpango wake wa wokovu wa wanadamu, kwani niĀ  mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwamba viumbe wake waishi kwa furaha. Kardinali Parolin, kawaalika kikundi cha Mtakatifu Martha na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa sehemu ya wanaume na wanawake walio tayari kushirikiana kwa uaminifu na mapenzi ya Mwenyezi Mungu ili kutokomeza biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Hivi karibuni Kardinali Parolin alipata nafasi ya kutembelea kanisa la Masista wa Kanosa huko Schio, Italia, na kusali mbele ya Masalia ya Mtakatifu Josephina Bakhita, ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 70 tangu kufariki kwake. Kardinali Parolin alimalizia Omelia yake kwa kusema: historia ya Mtakatifu Josephina Bakhita ni chemichemi ya matumaini katika kutafuta ukombozi wa wengi wanaoathirika kwa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Clestine Nyanda

Vatican News!.








All the contents on this site are copyrighted ©.