2018-02-09 07:48:00

Wakristo nchini Nigeria bado "ngangari" licha ya dhuluma za kidini


Askofu Oliver Dashe Doeme wa Jimbo Katoliki la Maiduguri, Nigeria, akitoa shukrani kwa misaada inayotolewa na Shirika la kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji anasema, kwa mwezi Januari, 2018 peke yake, jimbo la Maiduguri limekwishapoteza raia 73, wakiwemo watoto wadogo. Hawa ni wanyonge wanaouwawa kutokana na ghasia na kinzani ndani ya nchi ya Nigeria, wakati serikali ya Rais Muhhamad Buhari haionekani kufanya lolote ili kuzuia hali hiyo tete. Jimbo la Maiduguri ni eneo ambalo limeathirika zaidi kutokana na mashambulizi ya kikundi cha kigaidi cha Boko haram, ambacho kilianzishwa kutokea maeneo hayo. Mbali ya maelfu ya watu waliopoteza uhai, kumekuwa pia na matukio ya kuchoma na kuharibu shule takribani 25 na Hospitali 3 zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, makanisa 200 na nyumba za watawa 3 vimefanyiwa kufuru. Kwa masikitiko makubwa, wakati ambapo ilionekana kana kwamba mashumbulio na ghasia za Boko haram vilikuwa vinaelekea mwishoni, sasa yameibuka mashumbulio ya jamii ya wachungaji wa Fulani, wanaoua wakulima na kuwaharibia vibaya mashamba yao.

  

Askofu Oliver Dashe Doeme anasema, kuna uwezekano mkubwa kwamba walikuwa ni hao hao jamii ya wachungaji wa Fulani waliovamia maadhimisho ya mkesha wa Mwaka mpya 2018 katika makanisa 2 ya jimbo la Maiduguri na kuua waamini 17. Waamini wa maeneo hayo wananyanyaswa na kuuwawa sababu ya imani yao, hata hivyo ni jambo la mfano na la kuigwa kuiona imani yao thabiti, ambapo pamoja na mashambulio hayo yote, bado waamini wamesimama imara katika imani yao kwa kuhudhuria kwa wingi katika maadhimsho mbali mbali kanisani. Jimbo la Maiduguri linahudumia takribani watu 100,000 kati yao wajane, yatima na wasio na makazi, waliosababishiwa hali yao kutokana na vifo vya takribani 5,000 vya ndugu na jamaa zao wa karibu, waliouwawa na kikundi cha kigaidi cha Boko haram.

Mwaliko wa Askofu Oliver Dashe Doeme umetolewa siku chache baada ya mwaliko wa Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Abuja, ambaye amesema, mashambulio na hali tete wanayolazimika kuiishi waamini wa Nigeria isichukuliwe tu kuwa ni mashambulizi ya kigaidi ya waislamu dhidi ya wakristo, bali yatazamwe kwa jicho pana zaidi, kwa sababu kuna mashumbulizi dhidi ya misikiti, kuna utekaji nyara kwa kutumia nguvu na silaha, kuna wale wanaolipiza kisasi kwa chuki za ukabila, kuna jamii ya wachungaji wa Fulani wanaowashambulia wakulima, na makundi mengi tu ya uhalifu mwingi unaotapakaa nchini Nigeria. Mpaka sasa serikali haionekani kuchukua hatua zozote madhubuti, hii inaonesha jinsi gani serikali ya Rais Buhari siyo ya kuaminika katika kulinda usalama wa raia wa Nigeria na mali zao. Shirika la kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji linakusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia wajane 500 na yatima 1,000 nchini Nigeria, wakati huo huo Baraza la maaskofu Ujerumani kupitia tume ya misioni inayoongozwa na Askofu mkuu Ludwig Schick wa Bamberg, linahamasisha waamini wa Ujerumani kuonesha pia mshikamano na waamini wanaoteseka nchini Nigeria.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.