Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko: Uongozi bora ni dawa ya mchunguti dhidi ya utumwa!

Papa Francisko: uongozi bora na makini katika vikosi vya ulinzi na usalama, miongoni mwa wanasiasa na mihimili ya uinjilishaji ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

09/02/2018 15:44

Kikundi cha Mtakatifu Martha Kimataifa ni Taasisi ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu kilichozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014. Kuanzia tarehe 8 – 9 Februari 2018, kikundi hiki kimekuwa na mkutano wake mjini Vatican, uliokuwa unasimamiwa na Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 9 Februari 2018 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Kikundi hiki cha Mtakatifu Martha Kimataifa kwa kukazia: uongozi bora katika vikosi vya ulinzi na usalama, miongoni mwa viongozi wa kisiasa na wahudumu wa shughuli za kichungaji ili kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, hili ni janga kubwa katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwapongeza wajumbe wa Kikundi cha Mtakatifu Martha Kimataifa kwa mchango wao makini katika mchakato mzima wa kupambana, ili hatimaye, kuweza kudhibiti biashara ya binadamu na utumwa mamboleo unaoendelea kusababisha mateso na mahangaiko kwa watu wengi duniani. Mikutano kama hii, umekuwa ni muda wa kutafakari na kubadilishana uzoefu na mang’amuzi, kiasi hata cha kushirikishana sera na mikakati kitaifa na kimataifa ili kupambana na janga hili katika maisha ya watu, janga ambalo ni kubwa sana, kuliko hata inavyofikirika kwa wengi. Aibu hii dhidi ya utu na heshima ya binadamu inajionesha hata katika nchi zile zilizoendelea duniani!

Hata leo hii, Mwenyezi Mungu anaendelea kuuliza watu katika ulimwengu mamboleo, Je, Kaini yuko wapi ndugu yako Abeli. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni changamoto pevu kwa walimwengu mamboleo kuendelea kupembua kuhusu mifumo mbali mbali ya biashara na utumwa mamboleo inayojitokeza katika jamii na hatimaye, kufumbiwa macho na jamii husika wakati ambapo utumwa mamboleo kama vile: biashara ya ngono, unyonyaji wa watu, lakini zaidi kwa watoto wadogo wanaofanyishwa kazi za suluba.

Lengo kuu liwe ni kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, ili kuvunjilia mbali mitandao ya uhalifu wa magenge kitaifa na kimataifa bila kusahau maendeleo ya sayansi na teknolojia, kulega lega kwa kanuni maadili, nidhamu, weledi na uwajibikaji mambo yanayochangia waatu wengi kutoa kipaumbele cha pekee kwa faida kubwa kama kielelezo cha ukuaji wa uchumi badala ya utu na heshima ya binadamu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, ana matumaini sana na mjadala uliofanywa na wajumbe hawa katika mkutano wao wa mwaka huu hapa mjini Roma.

Ni majadiliano yatakayosaidia kukuza uelewa na umuhimu wa kuwasaidia waathirika wa matukio haya ya kihalifu pamoja na kuwawezesha kuanza tena safari ya kuingizwa kwenye jamii, ili kukuza na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu. Daima, Mama Kanisa anaonesha moyo wa shukrani kwa jitihada mbali mbali zinazofanywa ili kuwafariji waathirika kwa “mafuta ya faraja ya Mungu” kwani hii pia ni hatua muhimu sana ya kuganga na kuipyaisha jamii katika ujumla wake. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe wa Kikundi cha Mtakatifu Martha Kimataifa kwa moyo wao wa ushirikiano katika sekta hii muhimu sana. Anapenda kuwatia shime pamoja na kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake ili kuweza kutekeleza kinagaubaga dhamana na wajibu huu nyeti katika jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

09/02/2018 15:44