Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Imegota miaka 5 tangu Benedikto XVI alipong'atuka madarakani

Miaka 5 imegota tangu Papa Benedikto XVI alipong'atuka kutoka madarakani na kwenda "Jangwani" ili kusali, kutafakari na kuliombea Kanisa la Kristo! - AP

09/02/2018 17:30

Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, dunia ilipopigwa butwaa na mshangao mkubwa kusikia kwamba, Papa Benedikto XVI ameng’atuka kutoka madarakani, kama kielelezo cha heshima na upendo wake kwa Kanisa la Kristo, ili aweze kupanda kwenda mlimani kwa ajili ya kutafakari, kusali na kuliombea Kanisa la Kristo Yesu ili liweze kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu zaidi, huku likiendelea kujipyaisha kwa kusoma alama za nyakati! Ni tukio ambalo limeendelea kupata umuhimu wake wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua na kuthamini unyenyekevu mkubwa ulioshuhudiwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, miaka mitano iliyopita!

Monsinyo Alfred Xuereb, Katibu mkuu wa Sekretariati ya Uchumi Vatican ambaye kwa muda wa miaka mitano, yaani kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka 2013 amekuwa akifanya kazi bega kwa bega na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, katika unyenyekevu na ukimya wake, Papa Mstaafu Benedikto XVI amewashangaza watu wengi sana. Kabla ya kutangaza uamuzi wake mzito na mgumu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, alisali sana, akatafakari kwa kina na mapana na zaidi sana alipenda kutafakari maisha yake mbele ya Msalaba katika kimya kikuu!

Kwa mshangao mkubwa, tarehe 11 Februari 2013 akaamua kutangaza matokeo ya sala na tafakari zake za kina kwa kung’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu Mstaafu alitumia siku hiyo pia kutangaza mkutano wa Baraza kuu la Makardinali, “Conclave” na akaendelea kuwa mtulivu na mwenye amani ya ndani kwani moyoni mwake, alikuwa tayari ametekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Baada ya kukamilisha mchakato mzima wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, tukio la Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuaga na kuondoka kwenda Castel Gandolfo kuanza maisha mapya, liliwashtua na kuwagusa watu wengi sana!

Ni tukio ambalo lilitangazwa mubashara na vyombo mbali mbali vya habari ndani na nje ya Vatican! Watu wengi wakalishuhudia na kubaki na kumbu kumbu ya kiongozi wa Kanisa aliyelipenda sana na wala hakuwa na sababu ya kung’ang’ania madaraka, kiasi hata cha kuachia nafasi kwa Makardinali kuweza kumtafuta na hatimaye, kumchagua Khalifa Mpya wa Mtakatifu Petro, ambaye kwa sasa ni Papa Francisko, Baba wa maskini na matumaini ya waliokata tamaa!

Monsinyo Alfred Xuereb, anasema, hivi karibuni alibahatika kukutana na Papa Mstaafu Benedikto XVI, wakaadhimisha pamoja Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kupata kifungua kinywa. Alikuwa mdadisi wa mambo mengi katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa hakika, hali yake ya afya inayochangiwa na umri mkubwa, yaani miaka 91 vinaendelea kumdhohofisha sana na anasema, kwa sasa anajiandaa kwenda nyumbani kwa Baba wa milele kwenye usingi wa amani. Uamuzi wa kung’atuka kutoka madarakani uliofanywa na Papa Mstaafu Benedikto XI ni kitendo cha ujasiri na ushupavu wa imani na matumaini, daima akisukumwa na ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo.

Hakujiangalia wala kujitafuta binafsi; hakusikiliza shutuma na makelele ya watu waliotaka kupindisha ukweli kwa kuandika habari za kughushi! Kuna uhusiano mwema kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Papa Mstaafu Benedikto XVI, anayemjali kama “Babu ndani ya familia” amana, urithi na utajiri mkubwa wa Kanisa. Baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko alimpigia simu, Papa Mstaafu Benedikto XVI kumshukuru na kumpongeza kwa uamuzi wake wenye ujasiri, ari na moyo mkuu! Tangu wakati ule, Papa Mstaafu akaahidi utii na sala kwa Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, jambo ambalo ameendelea kulitekeleza katika hali ya ukimya na moyo mkuu. Papa Mstaafu Benedikto XVI kwa sasa anajiandaa vyema kwa sala, tafakari na Ibada mbali mbali kwa ajili ya kwenda nyumbani kwa Baba wa milele! Katika udhaifu wake wa mwili, anamshukuru Mungu kwa yote aliyoweza kumkirimia katika maisha yake kama Padre, Askofu na hatimaye, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Bado anasali kwa ajili ya Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

09/02/2018 17:30