2018-02-08 08:19:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani 2018


Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa mwaka huu, Jumapili tarehe 11 Februari 2018 inaongozwa na kauli mbiu “Mama tazama mwanao. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake”. Baba Mtakatifu anataka mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa kuhakikisha kwamba, inazingatia kwanza kabisa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu: wito wa Mama Kanisa wa huduma kwa wagonjwa na maskini; kumbu kumbu endelevu ya historia ya huduma kwa wagonjwa sanjari na nguvu ya uponyaji inayoonesha uhusiano uliopo kati ya utume wa uponyaji na mwamko wa imani kwa wagonjwa wanaokutana na Kristo Yesu, wakiomba huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huduma ya uponyaji inayotekelezwa na Kristo Yesu kwa wagonjwa mbali mbali inahitaji jibu la imani thabiti kutoka kwa wahusika.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linaendelea kupyaisha huduma kwa wagonjwa sanjari na kujikita katika uaminifu kwa amri iliyotolewa na Kristo Yesu mintarafu mng’ao wa mwanga wa utukufu wa Fumbo la Msalaba. Kwani hili ni fumbo la matumaini, huruma na upendo usiokuwa na kikomo. Ikumbukwe kwamba, fadhila ya upendo ni msingi wa maisha ya kila mfuasi wa Kristo na Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Kristo kwa waja wake.

Katika hija ya maisha yao hapa duniani, wafuasi wa Kristo watambue kwamba, wanasindikizwa, wanalindwa na kutunzwa na Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Huyu, ndiye Mama ambaye upanga ulipenya moyoni mwake, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi. Ni Mama ambaye aliendelea kuandamana na Kanisa katika sala kama inavyojionesha kwenye Siku kuu ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume. Mwinjili Yohane alimhifadhi na kumhudumia Bikira Maria, huku akiendelea kutafakari wito wa umama wake katika maisha na utume wa Kanisa la mwanzo. Mtume Yohane, aliwasaidia wagonjwa wa mwili na roho kukutana na Kristo katika hija ya maisha yao na hivyo wakaonja huruma, upendo, msamaha wa dhambi zao na hatimaye, wakafutwa machozi machoni pao. Hii ndiyo changamoto ambayo Wakristo wanapaswa kuivalia njuga kwa kumwilisha Injili ya upendo inayowataka kuhudumiana kwa dhati! Kwa njia hii, wakristo wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa uinjilishaji na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mama Kanisa katika maisha na wito wake, daima amekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, historia ambayo kwa hakika inapaswa kuwa endelevu. Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yameendelea kutoa huduma kwa wagonjwa hasa vijijini ambako bado huduma za afya zinasuasua. Mashirika haya yamekuwa yakitoa huduma bora, daima mwanadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Hospitali na taasisi za afya zimeendelea kufanya tafiti mbali mbali ili kuboresha tiba na huduma kwa wagonjwa, lakini maadili ya kikristo yamepewa msukumo wa pekee.  Kanisa limeendelea kusimama kidete katika kuchangia maboresho ya afya ya mama na mtoto kwa kupunguza vifo vya watoto wadogo; kwa kukinga na kutibu magonjwa mbali mbali. Kwa maneno mafupi, Kanisa daima limekuwa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano dhidi ya magonjwa kwa kuwasaidia wale waliojeruhiwa katika maisha!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kumbu kumbu ya historia ya huduma kwa wagonjwa ni chemchemi ya furaha, sadaka na ukarimu wa waanzilishi mbali mbali wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yanayoendelea kutekeleza dhamana na utume wao kwa ubunifu na uaminifu mkubwa, kwa kufanya tafiti na kutoa kinga na tiba ya magonjwa mbali mbali. Kutokana na changamoto mamboleo, gharama za uendeshaji na vifaa tiba, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, hospitali zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, hazigeuzwi kuwa na mwelekeo wa kibiashara zaidi, kwani Kanisa linataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa katika mchakato mzima wa huduma na tiba kwa wahusika. Hata Wakristo wanaofanya kazi katika hospitali za serikali na binafsi wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Injili.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwapatia pia mitume na waandamizi wao nguvu ya uponyaji na kwamba, Kanisa linaendeleza huduma hii kwa huruma na mapendo na kwamba, inapaswa kupyaishwa na kumwilishwa kutoka katika familia, parokia hadi kufikia taasisi za huduma ya afya. Wagonjwa wa muda mrefu, walemavu na wazee wanapaswa kuangaliwa zaidi kwa jicho la upendo na kwamba, kuna haja pia ya kuwa na sera makini za huduma kwa wagonjwa. Wadau wa huduma ya afya watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa wagonjwa, changamoto kwao ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kama ushuhuda unaotajirisha huduma kwa wagonjwa.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2018 kwa kumwangalia Bikira Maria, Mama wa huruma na upendo, ili awaombee matumaini wale wote waliokata tamaa; awasaidie waamini kuwa wakarimu kwa ndugu zao wagonjwa, ili waweze kuwahudumia kwa moyo wa Kiinjili. Kanisa linawakumbuka na kuwaombea wagonjwa na wadau wote katika sekta ya afya, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao katika hali ya upendo na huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.