Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Waamini lindeni nyoyo zenu ili msikengeuke!

Papa Francisko anawataka waamini kukesha na kusali ili wasitumbukie kwenye dhambi za mazoea.

08/02/2018 14:41

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 8 Februari 2018 amewataka waamini kukesha na kusali, daima wakiwa macho dhidi ya Ibilisi anayeweza kuwatumbukiza dhambini, kwa kudhoofisha tunu msingi za maisha ya kiroho kama ilivyokuwa kwa Mfalme Sulemani aliyekengeuka katika Amri na Maagizo ya Mwenyezi Mungu na kutopotea katika ukahaba na mmong’onyoko wa maadili na utu wema, kiasi hata cha kutomtii Mungu na hivyo kuwa kweli chukizo mbele yake! Inasikitisha kuona kwamba, Mfalme Sulemani alikengeuka na kushindwa kushika Amri za Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Mfalme Sulemani alikuwa ni mtu wenye hekima na busara ikilinganishwa na Mfalme Daudi, baba yake aliyepitia shida na mahangaiko makubwa; kwa hakika aligeuka na kuwa mdhambi mkubwa. Mfalme Sulemani aliyepata heshima na thamani kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuchagua hekima na busara ya kuwaongoza na kuwahukumu watu wake! Lakini, Sulemani akakengeuka na kutopea katika dhambi, kiasi hata cha kushindwa kuona uovu maisha pake, tofauti kabisa na Mfalme Daudi aliyetambua dhambi zake, akatubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.

Sifa na utukufu uliosimuliwa na Malkia wa Sheba, umegeuka na kuwa ni chukizo mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu ya kukengeuka na kufuata miungu ya kigeni, kiasi kwamba, moyo wake ukawa dhaifu sana! Baba Mtakatifu anakaza kusema, udhaifu wa moyo ulimtumbukiza Mfalme Sulemani katika dhambi za mazoea, kiasi cha kushindwa kuona uzito wa dhambi alizokuwa akitenda katika maisha kwa kukiuka Amri na Maagizo ya Mungu, kwa hakika mazoea yana taabu zake. Matokeo yake, Mfalme Sulemani akaishia kuwa mla rushwa na fisadi mkubwa. Haya ndiyo yanayowapata waamini ambao mioyo yao imekengeuka na kutopea katika dhambi. Hii ni changamoto endelevu katika maisha ya waamini, mwaliko ni kuhakikisha kwamba, wanakuwa waaminifu kwa Amri na Maagizo ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao bila kuudhoofisha moyo!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanakesha na kuulinda moyo wao, ili usitumbukie katika dhambi za mazoea na matokeo yake, ni kutengwa na Mwenyezi Mungu kwa sababu ya ubaya wa moyo. Ni vigumu sana kwa mla rushwa kutubu na kumwongokea Mungu na hatimaye kuwa Mtakatifu. Kumbe, kuna haja ya kukesha daima, ili kuulinda moyo usielemewe na dhambi, kwa kujenga mahusiano mema na Mwenyezi Mungu, ili kufurahia : uaminifu wa uzuri, ukuu na utakatifu wa kukaa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/02/2018 14:41