Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Papa Francisko: Uharibifu wa mazingira ni alama ya kupoa kwa upendo

Papa Francisko anasema, uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira ni dalili za kupoa kwa upendo duniani. - AP

08/02/2018 07:37

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2018 unaongozwa na kauli mbiu! “Na kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa” (Rej. Mt. 24:12) Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu manabii wa uongo, moyo uliopooza kwa ubaridi; umuhimu wa sala, matendo ya huruma na kufunga ili kuwasha moto wa Pasaka kwa kuabudu Ekaristi Takatifu na kujipatanisha na Mungu na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho!

Baba Mtakatifu anasema manabii wa uwongo ni watu wanaoelekeza kama nyoka, wanaofurahia mateso na mahangaiko ya wengine, kiasi hata cha kuwageuza na kuwa watumwa wao. Kuna mamilioni ya watu wanaoishi kwa tamaa ya kupata fedha, hali ambayo inawageuza kuwa ni watumwa wanaotafuta faida kubwa! Hawa ni watu wanaoishi katika upweke hasi, daima wakitafuta watu wa kuwadanganya. Manabii wa uwongo ni wale wanaotoa majibu mepesi mepesi kwa mambo magumu katika maisha! Wanaoweza kuponya magonjwa kwa njia ya miujiza, lakini huu ni ulevi kama ilivyo kwa vijana wanaobwia dawa za kulevya, kiasi cha kutokua na thamani tena katika jamii au kwa kujenga mahusiano legelege!

Ni watu wanaoishi katika ombwe kiasi hata cha kukosa maana ya maisha. Manabii wa uwongo wanatoa majibu mepesi mepesi yasiyoweza kufumbatwa katika tunu msingi za maisha ya binadamu kama vile: utu, uhuru na uwezo wa kupenda. Matokeo yake watu wamekengeuka na kuelemewa na tamaa na wataka kutenda kama anavyotenda baba yao Ibilisi, kwa kuwawekea machoni ubaya kama kitu chema; uongo kama ukweli, changamoto ya kufanya mang’amuzi ya dhati ili kuweza kuwabaini manabii wa uongo, kuna haja ya kuzama zaidi na wala si kuridhika na matokeo ya juu juu na haraka haraka, bali kuangalia ile chapa ya kudumu inayoacha alama zake katika nyoyo za watu kwani hii ni chapa inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya ustawi wa wengi.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, moyo wa mwanadamu unaweza kupoa na kukosa upendo kutokana na uchu wa fedha kwani shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha, hali inayowapelekea kufarakana na imani, kwa kumkataa Mwenyezi Mungu kiasi hata cha kushindwa kupata neema na faraja kutoka katika Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Matokeo yake ni ghasia na mauji kwa wale wote wanaodhaniwa kuwa ni kikwazo cha maendeleo kwa watu kama hawa. Hivi ndivyo vile vitendo vya utoaji mimba, kifo laini, mauaji ya wageni au jirani wasiokidhi vigezo vya matumaini yao.

Papa Francisko anasema, hata mazingira yanashuhudia kupoa kwa upendo kwa kazi ya uumbaji kunakosababishwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira, utupaji wa taka ngumu baharini pamoja na vifo vya wakimbizi na wahamiaji wanaomezwa kwenye tumbo la bahari na makaburi yao kukosa hata alama! Mbingu badala ya kutangaza sifa na utukufu wa Mungu, zimekuwa ni mahali pa kudondosha silaha za maangamizi. Upendo unapooza hata kwenye jumuiya za kikristo na alama kuu ni kukosekana kwa fadhila ya upendo kutokana na: ubinafsi na uchoyo, utambuzi wa nafsi, upweke hasi, mapambano na kinzani; kwa kumezwa mno na malimwengu na yale yanyoonekana wazi machoni pa watu; mambo yanayoharibu ari na moyo wa kimissionari.

Naye Padre  Agapiti Amani anasema, moja ya himizo kubwa la Kanisa ni kwa wanakanisa kutenda kazi za huruma ambazo kimsingi “ni matendo ya huruma ambayo kwayo tunamsaidia jirani katika shida zake za kiroho na za kimwili. Kufundisha, kushauri, kutuliza, kufariji ni kazi za kiroho za huruma, kama kusamehe na kusikiliza kwa uvumilivu. Kazi za kimwili za huruma ni hasa katika kuwalisha wenye njaa, kuwasetiri wasio na nyumba, kuwavika walio uchi, kuwatembelea wagonjwa na wafungwa, na kuwazika wafu” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, n. 2447). Baba Mtakatifu Francisko ameongeza utunzaji wa uumbaji kuwa ni kazi pia ya huruma. “Kama kazi ya kiroho ya huruma, kuyatunza makazi yetu ya pamoja inadai kuitafakari dunia ya Mungu kwa shukrani” (“Laudato si, n. 214). Baba Mtakatifu anasema pia kuwa, “Haitoshi kuionja tu huruma ya Mungu katika maisha yetu. Ni lazima wale wanaoipokea wawe ishara na chombo cha huruma kwa wengine. Si suala la kufanya juhudi kubwa au kutenda kama mwanadamu asiye wa kawaida. Bwana ametuonesha njia rahisi, inayoundwa na matendo madogo lakini ambayo, mbele ya macho yake, yanathamani kubwa kiasi kwamba akasema ni juu ya hayo ndimo ilimo hukumu yetu.

Yesu anasema kwamba, kila mara tunapompatia mtu mwenye njaa chakula na mwenye kiu maji, tunapomvika aliyeuchi na kumkaribisha mgeni, au tunapomtembelea mgonjwa au mfungwa, tunamtendea hayo yeye pia. Kanisa linayaita matendo haya kuwa ni kazi za huruma za kimwili…Kazi za huruma zinaamsha ndani yetu hitaji na uwezo wa kuifanya imani iishi na kutenda kupitia upendo…kwa njia ya matendo haya madogo tunaweza kuleta mapinduzi ya kiutamaduni… kama kila mmoja wetu, kila siku, akifanya moja ya haya, haya yatakuwa mapinduzi duniani!” Hii ni sehemu ya ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2017 iuliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ukiongozwa na kauli mbiu “Furaha ya Injili ya Uumbaji”. Hii ni changamoto endelevu kutokana na madhara makubwa yanayosabaishwa na uchafuzi wa mazingira. Uharibifu wa mazingira una madhara makubwa hata katika maisha ya mwanadamu! Ikumbukwe kwamba, waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi ni maskini na wanyonge. Kumbe, kuna haja ya kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora, ili mazingira nayo yaweze kumtunza mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko, katika Waraka wake wa kitume, “Laudato si”, yaani  “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”,  anakaza kusema utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki, amani na mshikamano kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Anatuambia utunzaji wa uumbaji ni kazi ya huruma na kuitunza nyumba yetu  ya pamoja inadai  au inatupasa kuitafakari kazi ya uumbaji kwa moyo wa shukrani, na katika hili mwanadamu atakuwa amekuwa chombo cha huruma kwa wengine.  Mtakatifu Francisko wa Assisi aliwahi kusema mazingira ya ulimwengu huu pamoja na viumbe vyake ni kama ndugu, yaani hutegemeana na hivyo huitaji upendo na utunzaji, na hili ni jambo linalompa mwanadamu mamlaka ya kutunza mazingira pamoja na viumbe vyote vya angani na majini ila yote yakiongozwa na tanswira ya upendo na mwisho wake ukielekea kwenye upendo wa Mungu.

Ujumbe wa Kwaresima kwa 2017, ukitazama mbele unamkosha mwanadamu kwa kumwambia,  furaha ya pasaka si kwa mwanadamu peke yake bali  ni furaha ya viumbe vyote  vinavyotawaliwa na kuratibishwa na mwanadamu aliyekombolewa na Kristo, kwani ufufuko ndiyo sababu ya furaha, imani na matumaini yetu. Hivyo katika haya  tujifunze kuishi furaha itokayo kwa Mungu ambayo inaletwa na uumbaji, na furaha hii itapata ukamilifu wake katika maisha ya umilele mbinguni. Tukumbuke kuwa kutunza mazingira ni mojawapo ya kuishi katika mapenzi ya Mungu. Sambamba na hilo mwanadamu bado hajaonyesha uwajibikaji chanya katika kujali na kutunza mazingira na hivyo tunashuhudia  matukio mengi  yasabishawayo na  uaribifu wa mazingira yakimwaadhiri mwanadamu, hususani uharibifu wa  vyanzo vya maji, ambavyo vinatuletea ukosefu wa maji na  hudumu nyingi katika jamii. Mito mingi inakauka,  viumbe wa baharini  kama samaki na vinginevyo vinapungua, haya yote ikiwa ni sababu ya uharibifu wa mazingira. Hivyo,  ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2017, ni ujumbe wa kumrudia Mungu, kutafakari na kuchukua hatua katika kupenda na kutunza mazingira. Mwanadamu  akieshimu na kulinda mazingira, nao viumbe pia watakuwa wamekombolewa   dhidi ya utumwa wa uharibifu, kama atuambiavyo Mtakatifu Paulo. Tutunze mazingira na tuendelee kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zetu.

Mimi Pd. Agapiti Amani ALCP/OSS

Vatican News!

08/02/2018 07:37