Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Ratiba

Papa Francisko kutembelea Puglia na Toscana nchini Italia, 2018

Papa Francisko, tarehe 20 Aprili anatarajiwa kutembelea Mkoa wa Toscana na tarehe 10 Mei kutembelea Mkoa wa Puglia, Kusini mwa Italia.

08/02/2018 09:31

Mnamo mwezi Aprili na mwezi Mei 2018, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija mbili za kitume maeneo ya Puglia na Toscana nchini Italia. Taarifa hizi zilizoambatana na ratiba ya hija hizo mbili za kitume nchini Italia, zimetolewa na Mhudumu mkuu wa Nyumba ya kipapa ambapo Baba Mtakatifu atapenda kusali katika makaburi ya Askofu Tonino Bello (1935 – 1993) na Padre Zeno Saltini (1900 – 1981), kisha kukutana na wanajumuiya ya Nomadelfia na Wafokolari wa Loppiano.

Kwa ufupi, Baba Mtakatifu Francisko siku ya Ijumaa tarehe 20 Aprili, atapaa kutoka uwanja wa ndege wa Ciampino, Roma, mpaka uwanja wa ndege wa kijeshi wa Galatina, ambako atachukua helkopta kuelekea makaburi ya Alessano, Puglia, mahali alipozaliwa na kuzikwa Askofu Tonino Bello, baada ya kifo chake mnamo tarehe 20 April 1993 akiwa na umri wa miaka 58. Baada ya sala katika makaburi hayo, atafanya mapumziko mafupi kisha kuonana na wanafamilia wa kifransiskani kwani Askofu Tonino Bello alikuwa mtawa wa utawa wa tatu kisha kuelekea katika viwanja vya  Ugento – Santa Maria di Leuca, ambapo Askofu Vito Angiuli atamkaribisha rasimi ili kusema na waamini. Baadae ataelekea kuadhimisha Misa Takatifu katika kanisa kuu la Molfetta Jimbo Katoliki la Molfetta-Giovinazzo-Ruvo-Terlizzi, ambapo Askofu Tonino Bello aliliongoza tangu mwaka 1982 mpaka mauti ilipomfika.

Siku ya Alhamisi, tarehe 10 Mei, 2018 Baba Mtakatifu atafanya hija maeneo ya Toscana, ambapo ataanzia Nomadelfia akipokelewa na Askofu Rodolfo Cetoloni wa Jimbo la Grosseto, Padre Ferdinando Neri, na Francesco Matterazzo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nomadelfia. Huko atapata nafasi kwenda kusali katika kaburi la Padre Zeno Saltini, na baada ya kuonana na wanajumuiya wa Nomadelfia, na atakuwa na tafrija na vijana wa jumuiya hiyo, ambapo atazungumza nao mawili matatu. Katika kuhitimisha hija hiyo ya kitume, Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kusali katika Madhabahu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Theothokos, na kupokea salamu za shukrani kutoka kwa Askofu Mario Meini wa Fiesole, na Bi Maria Voce, Mwenyekiti wa Wafokolari.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

08/02/2018 09:31