2018-02-08 15:53:00

Papa Francisko asikitishwa na maafa yaliyotokea nchini Taiwan


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Philip Huang Chao-ming wa Jimbo Katoliki Hwalien, lililoko nchini Taiwan, anapenda kutuma salam zake za rambi rambi pamoja na kuonesha mshikamano wake wa upendo kwa njia ya sala na sadaka yake kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na tetemeko la ardhi lililotokea Jumanne, tarehe 6 Februari 2018 huko Mashariki mwa Pwani ya Taiwan.

Taarifa zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 10 wamefariki dunia, wengine 265 wamejeruhiwa vibaya na kwamba, watu 60 hawajulikani mahali walipo! Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwaombea wale wote waliofariki dunia katika maafa haya ili waweze kupata pumziko la milele mbinguni! Anawaombea majeruhi kupona haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime viongozi wa serikali na vikosi vya uokoaji kuongeza bidii ya kuwasaidia waliotharika. Mwishoni, anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wananchi wote wa Taiwana katika kipindi hiki kigumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.