Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Majadiliano ya kidini yakuze tunu msingi za maisha ya kiroho!

Majadiliano ya kidini yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu zinazomwilishwa kuanzia kwenye familia ili kujenga jamii yenye upendo na mshikamano wa dhati. - EPA

08/02/2018 16:14

Kwa mara ya kwanza katika historia, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE , kuanzia tarehe 7-9 Februari 2018 linaendesha majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na waamini wa dini ya Kiislam kuhusu imani na tasaufi, kwa mwaliko uliotolewa na Askofu mkuu Angelo Massafra wa Jimbo kuu la Shkodrè. Anasema, majadiliano ya kidini ni muhimu sana katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kwa mwaka huu, wajumbe wanajadiili zaidi kuhusu masuala ya kitaalimungu, tasaufi na mahusiano na dini mbali mbali Barani Ulaya. Wawezeshaji wakuu wa majadiliano haya ya kidini wanaendelea kujikita zaidi katika mchakato wa ujenzi wa mahusiano mema kati ya mwamini na Mwenyezi Mungu; changamoto za shughuli za kichungaji kati ya Wakristo na Waislam Barani Ulaya; ndoa ya watu wa imani tofauti na kwa kesi hii, ndoa kati ya Mkristo na Muislam. Hapa familia inakuwa ni kiini cha majadiliano ya kidini na mahali muafaka pa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho.

Askofu mstaafu Claude Rault wa Jimbo Katoliki la Laghouat, Algeria ameshirikisha uzoefu na mang’amuzi yake kuhusu majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam, mintarafu tasaufi na maisha ya kiroho. Kardinali Jean Lous Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Monsinyo Khaled Akashek, afisa mwandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini ameelezea shughuli mbali mbali ambazo zimetekelezwa na Baraza hili, lakini kwa namna ya pekee, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri na hotuba yake kwa wajumbe waliokuwa wanashiriki mkutano wa kimataifa kuhusu amani duniani, uliokuwa umeandaliwa na Chuo kikuu cha Al Azhar

mjini Cairo, nchini Misri.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri kuanzia tarehe 28-29 Aprili 2017 iliongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri”. Hii ni hija ya kitume iliyopania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa familia ya Mungu nchini Misri, ili kujikita katika misingi ya haki, amani, maridhiano na uhuru wa kuabudu. Tofauti msingi zinazojitokeza miongoni mwa familia ya Mungu nchini Misri ni utajiri unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kujipambanua kuwa ni kiongozi anayesimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Jean Louis Tauran anakaza kwa kusema, tema ambazo zimechaguliwa na kufanyiwa kazi kwa mwaka huu ni muhimu sana katika kurekebisha mitazamo finyu na maamuzi mbele ambayo wakati mwingine, yanapenyezwa kwa makusudi na vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa malengo maalum, ili kukuza na kudumisha misimamo mikali ya kidini na kiimani, hatari sana kwa mafungamano ya kijamii. Jambo la msingi ni kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki na amani kwa kukataa kishawishi cha kutumia jina la Mwenyezi Mungu kufanya vitendo vya kinyama.

Dini ya Kiislam ina amana na tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili, ambazo zikifuatwa na kuzingatiwa ni msaada mkubwa katika kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kuna haja ya kuheshimiana na kuthaminiana; kukuza na kudumisha upendo, wema na huruma mambo msingi katika maisha ya kiroho kwa waamini wa dini ya Kiislam ambayo pia yanapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko. Wakristo na Waislam wote wanapaswa kuwa ni vyombo vya huruma ya Mungu kwa kuondokana na mambo yote yanayoweza kuchochea na kukuza vita, ghasia na mipasuko ya kidini; kwa kukataa kabisa kishawishi cha ubaguzi na nyanyaso kwa misingi ya kidini, ili kudumisha amani na utulivu! 

Albania ni nchi ambayo imeonja nyanyaso, dhuluma na vita ya kidini, lakini pia ni nchi ambayo iliweza kusimama tena na kuanza mchakato wa haki, amani na maridhiano ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko aliichagua kuwa ni kati ya nchi za kwanza kutembelewa Barani Ulaya. Hapa ni mahali alipozaliwa Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta, chombo na shuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu; dada na mama wa walimwengu wote, lakini zaidi maskini na wale wote wanaosukumizwa pambezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

08/02/2018 16:14