Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maendeleo

Jimbo kuu la Mombasa lazindua mpango mkakati wa kichungaji

Jimbo kuu la Mombasa, Kenya limezindua Mpango Mkakati wa Shughuli za Maendeleo ya Kichungaji katika kipindi cha miaka kumi, mkazo ni majiundo, miundo mbinu na maboresho ya huduma kwa watu wa Mungu. - AFP

08/02/2018 08:30

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, hivi karibuni, amezindua Mpango Mkakati wa Shughuli za Kichungaji Jimbo Kuu la Mombasa unaojikita katika kutangaza na kushuhudia uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya familia ya Mungu Jimboni humo kwa njia ya huduma makini, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali za maisha! Mpango huu unapania pamoja na mambo mengine, kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na matumaini, ili kuharakisha mabadiliko chanya yanayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika kanuni maadili; huruma na upendo wa Mungu; umoja na ushirikiano; haki na usawa katika utekelezaji wake!

Mpango Mkakati wa Shughuli za Kichungaji Jimbo Kuu la Mombasa unatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka kumi kuanzia sasa. Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anasema, ni mpango mkakati unaowajumuisha wakleri, watawa na waamini walei katika utekelezaji wake, daima, wote wakiwa wameshikamana kama ndugu katika Kristo Yesu. Huu ni mpango mkakati ambao umepembua kwa kina na mapana hali halisi ya Parokia, maisha na mahitaji msingi ya kiroho na kimwili kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Kenya. Ni kazi kubwa iliyotekelezwa na Tume ya shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Mombasa kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas, Jimbo kuu la Mombasa. Mchakato huu umefanywa kwa muda wa  miaka mitatu na sasa Jimbo kuu la Mombasa limeibuka na Mpango Mkakati wa utekelezaji wake, unaopaswa kufanyika katika kipindi cha miaka kumi kuanzia sasa anasema Askofu mkuu Martin Kivuva

Musonde. Familia, Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, Parokia na Jimbo katika ujumla wake, ndio wahusika wakuu. Ikumbukwe kwamba, Jimbo kuu la Mombasa linatoa kipaumbele cha kwanza kwa familia kama shule ya utakatifu, haki na amani; mahali muafaka pa kurithishia imani, matumaini, mapendo na msamaha! Nafasi ya pili ni kwa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo, shule ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na mahali pa kushuhudia Injili ya huruma na mapendo ya Kikristo, kielelezo makini cha imani tendaji!

Takwimu zinaonesha kwamba, Jimbo Kuu la Mombasa lina Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zipatazo 1,400 zinazohudumiwa kwenye Parokia 56 zinazounda Jimbo Kuu la Mombasa ambalo kwa sasa linahudumiwa na Mapadre 114. Lengo kwa siku za usoni ni kuhimiza miito mitakatifu ili kuongeza idadi ya waamini wanaofunga na kuishi vyema Injili ya familia; wakleri wanaojisadaka bila kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Neno na Sakramenti za Kanisa bila kusahau mchango wa watawa katika ushuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini ya katekesi, elimu, afya na maendeleo endelevu ya binadamu! Jimbo linapania kuongeza Parokia kutoka Parokia 56 zilizopo kwa sasa hadi kufikia 96 ili kusogeza huduma za kichungaji na maisha ya kiroho kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa. Huu ndio Mpango Mkakati wa Shughuli za Kichungaji Jimbo kuu la Mombasa katika kipindi cha miaka kumi kuanzia sasa anasema, Askofu mkuu Martin Kivuva

Musonde.

Na Sr. Bridgita Samba Mwawasi,SSJ. Mombasa na kuhaririwa na

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/02/2018 08:30