Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Waamini wa dini mbali mbali jitokezeni kwa wingi kuombea DRC & Sudan

Papa Francisko anawaalika waamini wa dini mbali mbali kuungana naye tarehe 23 Februari 2018 ili kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini DRC na Sudan ya Kusini. - AP

07/02/2018 17:00

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4 Februari 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ametangaza kwamba, tarehe 23 Februari 2018, Ijumaa ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wafunge na kusali, kwa ajili ya kuombea amani duniani. Lakini kwa namna ya pekee, kuombea amani huko DRC na Sudan ya Kusini ambako watu wanateseka sana kutokana na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii na kinzani mbali mbali.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika hata waamini wa dini mbali mbali kuungana naye kutekeleza dhamana na wajibu huu wa kimaadili kadiri ya taratibu, sheria na kanuni za dini zao, lakini watu wote kwa pamoja, waweze kumlilia Mwenyezi Mungu ili amani ya kweli iweze kupatikana katika maeneo haya ambayo watu wake wanateseka sana kwa vita. Anasema, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, daima anasikiliza kilio cha watoto wake, wanaomkimbilia kwa machozi na mateso makubwa wakiomba msaada wake, ili kuwaponya waliopondeka moyo na kuzingaga jeraha zao.

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini linasema, Baba Mtakatifu Francisko  anawaalika waamini wa dini mbali mbali duniani kushiriki katika tukio hili, kadiri ya Sheria, kanuni na taratibu za dini zao. Lina amini kwa dhati kwamba, dini zina mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha amani duniani. Kumbe, Baraza hili linapenda kutoa shukrani zake za dhati, kwa ushiriki na mshikamano utakaooneshwa na waamini wa dini mbali mbali duniani kwa ajili ya kuombea amani huko DRC na Sudan ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

07/02/2018 17:00