2018-02-07 07:28:00

Ubaridi wa upendo ni chanzo kikuu cha mateso na nyanyaso za watu!


Waamini wa Kristo wanaoishi maeneo ya Mashariki ya Kati, bado wanaendelea kuteswa sababu ya imani yao kwa Kristo, umaskini unaosababishwa na vita, kinzani na ghasia; ambapo mpaka sasa hazionekani dalili za nia ya kukomesha matukio hayo. Zaidi sana, mateso na mahangaiko ya wakristo hao, yanasababishwa pia na ubaridi wa upendo ambapo wengi wanaonesha kutojali kabisa mateso ya wenzao. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuwaombea ndugu wakristo waishio Mashariki ya Kati, na kwa namna ya pekee walioko nchini Armenia. Mwaliko huo ameutoa alipokuwa akiongoza Ibada ya Misa Takatifu, katika Parokia ya Watakatifu Biagio na Carlo, Jimbo kuu la Roma, wakati parokia hiyo inaadhimisha sherehe ya somo wasimamizi na waombezi, siku ya Jumamosi tarehe 3 Februari 2018.

Mateso na nyanyaso ambazo Kanisa linapitia, kwa macho ya kawaida, vinaonekana kama maumivu yasiyo na faida yeyote na zaidi sana kama ishara ya kushindwa, hata hivyo Mwenyezi Mungu katika hekima yake kuu, hukusanya kila tone la damu na jasho la wafiadini na wenye kunyanyaswa kwa imani, kisha huvigeuza kuwa rutuba kwa ajili ya kukua na kukomaa kwa ukristo na kuzaa matunda mengi ya imani thabiti. Dunia ya leo inahitaji sana waamini wanaohangaikia majadiliano, ukarimu na jitihada za kulinda na kutetea haki na amani, hasa kwa wale wanaonyanyaswa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Sandri, amekumbusha pia umuhimu wa utume kwa vijana. Baba Mtakatifu Francisko, kwa kutilia maanani nafasi ya vijana katika utume na maisha ya Kanisa, kaitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili vijana, itakayofanyika mjini Vatican mnamo mwezi Oktoba 2018, ikiongozwa na kauli mbiu vijana imani, na mang’amuzi ya miito. Siku chache kabla ya maadhimisho ya Pasaka, Baba Mtakatifu atakutana na wawakilishi wa vijana kutoka mabara yote duniani, ikiwa ni mwendelezo wa harakati za kuwasikiliza vijana. Hivyo Kardinali Sandri, anawaalika waamini kuendelea kuliombea Kanisa na kila mmoja kushiriki kwa nafasi yake, ili matukio haya yote yawasaidie vijana wa kizazi kipya kukutana na Mungu na waweze kuzaa matunda mema na yenye kudumu. Utume kwa vijana, uende sambamba na ushuhuda dhahiri wa maisha ya kila siku. Huu ni mwaliko kwa wazazi, walezi, wakleri, watawa na wote wenye nafasi ya kuwahudumia vijana, kuhakikisha kwamba kila wanalolitenda linakuwa na matokeo chanya kama mfano wa kuigwa na vijana. Ushuhuda wa namna hii, utaweza kuwasha matumaini na hamu ya vijana kuwa karibu zaidi na zaidi na Kristo Bwana.

Kanisa la Parokia ya Watakatifu Biagio na Carlo, jijini Roma lilipata misukosuko na kuacha nyufa kutokana na tetemeko la mwaka 2016, na hivyo kupelekea kanisa hilo kufungwa na waamini kuanza kusali kwa kutumia ukumbi wa parokia. Baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu kwa kumbukumbu ya somo wasimamizi na waombezi wa parokia hiyo, siku ya Jumamosi, Paroko, Padre Giovanni Villa, alitangaza kwa matumaini makubwa kwamba: ndani ya muda mfupi, zitaanza kazi za kurekebisha na kuimarisha tena kanisa hilo. Kumbe mbali na waamini wanaonyanyaswa sababu za imani, ghasia, na kinzani, Kanisa linawakumbuka pia waamini wanaoteseka kutokana na majanga asilia kokote duniani.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.