2018-02-07 15:50:00

Papa Francisko: Kristo Yesu ni kiini cha Habari Njema inayotangazwa!


Liturujia ya Neno la Mungu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu inahitimishwa kwa kutangazwa kwa Injili na kabla yake, Shangilio ambalo ni aleluya huimbwa nje ya kipindi cha Kwaresima  na waamini waliokusanyika wanaitikia kwa shangwe ili kumkaribisha Kristo Yesu anayekuja kuzungumza na wafuasi wake kwa njia ya Injili. Kama ilivyo kwamba Fumbo la maisha na utume wa Kristo Yesu linafumbatwa na kung’ara katika Ufunuo wa Maandiko Matakatifu, hivi ndivyo ilivyo hata kwa Liturujia ya Neno la Mungu. Injili ni muhtasari wa Neno la Mungu lililosomwa katika masomo yaliyotangulia kutoka katika Agano la Kale na Agano Jipya na kupata utimilifu wake kutoka kwa Kristo Yesu, kiini cha Habari Njema ya Wokovu!

Huu ni muhtasari wa Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 7 Februari 2018 iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican kutokana na hali ya hewa kuchafuka sana mjini Roma. Liturujia ya Neno la Mungu inatofautisha Injili na masomo mengine na kwamba, inatangazwa kwa kishindo na Mhudumu wa Neno la Mungu aliyewekwa wakfu na anahitimisha Ibada hii kwa kubusu Injili. Baba Mtakatifu anasema, Injili inapotangazwa waamini wanasimama, wanafanya Ishara ya Msalaba; Neno la Mungu linafukiziwa uvumba kama kielelezo cha kumtukuza Kristo Yesu pamoja na kutambua umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya waamini.

Kwa njia ya alama hizi, waamini wanatambua uwepo wa Kristo Yesu kati yao, anayewatangazia Habari Njema inayo ongoa na kumletea mwamini mabadiliko katika maisha. Haya ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Kristo Yesu na waamini wake na kushuhudiwa kwa maneno, “Utukufu kwako Ee Bwana” na “Sifa kwako Ee Kristo”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kusikiliza Neno la Mungu hata kama wamekaa kwa umakini mkubwa kwani Kristo Yesu anazungumza nao kwa wakati huo! Mama Kanisa anatangaza Injili na waamini wanapaswa kusikiliza kwa makini na kwa moyo wazi ili kung’amua na kutambua mambo ambayo Kristo Yesu alitenda na kusema kwa wakati fulani. Hili ni Neno ambalo ni hai kwani ni uwepo endelevu wa Kristo kati pamoja na watu wake. Mtakatifu Agostino anasema kwamba, Injili ni mdomo wa Kristo anayetawala mbingu na dunia na kamwe haachi kuzungumza na waja wake walioko hapa duniani, kwani kwa hakika kwa kutangaza Injili na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu, hatimaye, waamini wanapaswa kutoa majibu muafaka yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao, kielelezo cha imani tendaji. 

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Ujumbe wa Neno la Kristo unahitaji pia kusindikizwa na mahubiri yanayotolewa na Padre baada ya Injili kusomwa. Mahubiri ni mwendelezo wa majadiliano kati ya Yesu na waja wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wamekazia sana umuhimu Mahubiri katika Ibada ya Misa Takatifu kama mwendelezo wa majadiliano kati ya Kristo Yesu na waamini wake. Mahubiri yanapaswa kuandaliwa kwa umakini mkubwa kwani hii ni chemchemi ya utakatifu wa maisha kwani Neno la Mungu linahitimisha safari yake kwa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kama alivyofanya Bikira Maria na Watakatifu. Neno la Mungu linapaswa kuingia masikioni mwa waamini, kuzamishwa katika sakafu ya nyoyo za waamini na kufanyiwa kazi kwa njia ya mikono ya waamini.

Baba Mtakatifu anasema, kuhusu umuhimu wa mahubiri amejadili kwa kina na mapana kwenye Waraka wake wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”: mahubiri hayana budi kuwasaidia watu kupyaisha maisha yao. Maaskofu, Mapadre na Mashemasi wanapaswa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao wa kuandaa na kuhubiri vyema kama sehemu ya huduma makini kwa watu wa Mungu na waamini nao wanapaswa kusikiliza kwa makini pamoja na kutambua kwamba, kila mhubiri anazo sifa na mapungufu yake.

Changamoto kwa waamini hapa ni kuhakikisha kwamba, wanasikiliza kwa makini bila kuweka pingamizi. Wahubiri watambue kwamba, wanamwakilisha Yesu katika huduma hii makini na kwamba, mahubiri yanapaswa kuandaliwa kwa umakini mkubwa. Wahubiri watambue kwamba, mahubiri ni haki ya waamini na ni sehemu muhimu sana ya Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu. Mahubiri yawe mafupi, lakini yaliyoandaliwa vyema kwa njia ya sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu na hatimaye, muhtasari wake kadiri ya mazingira ya watu! Baba Mtakatifu anahitimisha Katekesi yake kuhusu Ibada ya Misa Takatifu kwa kusema kwamba,  Liturujia ya Neno la Mungu ni njia makini ambayo Mwenyezi Mungu anaitumia kuzungumza na kujadiliana na waja wake! Waamini nao wanapaswa kusikiliza kwa makini; Kumwabudu Kristo Yesu anayezungumza pamoja nao, ili waweze kuongoka na kupyaishwa tena katika maisha yao, tayari kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya upya wa maisha unaoshuhudiwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.