Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Diplomasia ya mshikamano ni kikolezo cha maendeleo endelevu!

Diplomasia ya mshikamano, udugu na upendo ni muhimu sana katika ujenzi wa amani duniani. - EPA

07/02/2018 07:45

Tumekutana Washington DC, kwa lengo la kupalilia diplomasia ya urafiki, yaani ule utamaduni wa kukutana ambao Baba Mtakatifu Francisko anausisitiza sana katika utume wake. Mkutano huu hapa Washington DC, ni katika harakati za kunuia kujenga mifano ya viongozi wanaoshiriki kwa pamoja kutafuta mafao ya wengi. Matukio mengi ya kusikitisha kwa enzi zetu hizi, yanayoonekana kana kwamba ni maigizo, yanahitaji kukabiliwa kwa kukoleza zaidi majadiliano. Wake kwa waume sehemu zote duniani, wanatafuta uhuru, amani, haki jamii na kuheshimu utu wa mtu.

Hazina ya utamaduni wa udugu na mshikamano, ndiyo itakayowezesha mafanikio ya maendeleo endelevu ya binadamu. Hakuna taifa au jamii ambayo ni kisiwa, ndiyo sababu mikutano kama huu wa Washington DC, ni muhimu sana katika kufanikisha hayo. Hivyo ndivyo Bwana Salvatore Martinez, Mwenyekiti wa chama cha Uamsho wa Roho na mfuko wa Vatican, Centro Internazionale Famiglia di Nazareth, anavyodadavua kiini cha safari ya utume wake nchini Marekani, kuanzia tarehe 6 – 9 Februari 2018. Bwana Martinez anakutana na wawakilishi wa taasisi za kidini, kisiasa, kitaaluma na  akiwa pia ni mjumbe mwakilishi wa nchi ya Italia kwenye Shirikisho la Ushirikiano wa Kimataifa la Usalama na Maendeleo barani Ulaya, OSCE, katika kutetea haki za binadamu, kwa namna ya pekee mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, hofu isiyo mashiko dhidi ya wageni na unyanyapaaji.

Kwa namna ya pekee, Bwana Salvatore Martinez anashiriki katika National Prayer Breakfast, kifungua kinywa cha 66 kwa ajili ya sala kitaifa, nchini Marekani. Huu ni mkusanyiko mkubwa sana wa viongozi wa dini jijini New York, kutoka madhehebu na dini ambazo zinamtambua Kristo Yesu kama mfano wa uongozi unaojali tunu msingi za Injili, utu wa binadamu, amani, udugu na mshikamano kati ya mataifa. Naye Bwana Salvatore Martinez anashiriki kwa mara ya 17 sasa katika tukio hilo la National Prayer Breakfast, ambapo Rais Donald Trump atashiriki. Wanashiriki pia Maseneta na wajumbe wa Congress, watumishi wa mahakama nchini Marekani na wanadiplomasia wa jumuiya ya kimataifa. Wawakilishi zaidi ya 140 kutoka mataifa mbali mbali duniani wanashiriki tukio hilo, kwa lengo la kujadiliana tema kubwa zinazoikabili dunia leo, na kuboresha zaidi mahusiano na ushirikiano uliopo katika miradi mbali mbali ya mshikamano, maendeleo endelevu na kudumisha utu wa binadamu.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!

 

07/02/2018 07:45