Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Yaliyojiri katika maadhimisho ya Siku ya Watawa Jimbo kuu la Mombasa

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anawataka watawa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha umoja na udugu, upendo na mshikamano katika maisha na utume wao, licha ya changamoto wanazokabiliana nazo kila siku! - ANSA

06/02/2018 16:01

Hivi karibuni wakati wa maadhimisho yua Siku ya XXII ya Watawa Duniani, Baba Mtakatifu Francisko amewaambia watawa kwamba, wanaweza kupyaisha mkutano na jirani zao kwa kuendelea kuzingatia kuandamana kwa pamoja, huku Mwenyezi Mungu akiwa ni kiini cha safari na hija yao ya pamoja. Wazee wanazo funguo za maarifa zinazotakiwa na vijana ili kukua na kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani toba, wongofu wa ndani, upendo, udugu na mshikamano wa kweli. Amewakumbusha kwamba, Unabii unafumbatwa kwa namna ya pekee katika kumbu kumbu ili kuweza kuwakutanisha watu.

Watawa wanapaswa kutambua kwamba, mbele yao kuwa ndugu zao katika Kristo wanaopaswa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini, badala ya kuthamini simu ya kiganjani. Maisha ya kuwekwa wakfu hayana budi kutoa kipaumbele cha kwanza katika ushuhuda wenye mvuto, ili kuendelea kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu, ili hatimaye, kuzaa matunda yanayokusudiwa kwani maisha yao yamejikita katika mizizi ya kweli na wala si kutoa kipaumbele cha kwanza kwa miradi, teknolojia na miundo mbinu kwani kwa kufanya hivi, maisha ya kitawa yatakuwa butu pasi na mvuto wala mashiko! Jirani na mahitaji yake msingi ni muhimu kuliko mambo yote!

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, hivi karibuni, ameadhimisha Siku ya XXII ya Watawa Jimbo Kuu la Mombasa, kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wito wa maisha ya kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa. Watawa ni mhimili, mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Wao ni manukato yanayolipamba Kanisa kwa uwepo na huduma yao makini katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa. Jimbo kuu la Mombasa linahudumiwa na Mashirika kumi na matano ya kitawa na kazi za kitume na kwa pamoja yanashiriki kikamilifu katika maisha na utume kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa.

Askofu mkuu Musonde amewataka watawa kujenga na kudumisha umoja na udugu; upendo na mshikamano katika maisha na utume wao, licha ya changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha yao! Watawa wawe ni mashuhuda na vyombo vya imani, tayari kuitangaza na kuimilisha katika matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji! Kujikwaa, kuteleza na kuanguka ni sehemu ya mchakato wa maisha ya kitawa, kumbe, watawa wanapokumbana na changamoto kama hizi katika safari ya maisha na wito wao, wawe na ujasiri wa kusimama tena na kuendelea na safari kwa kutumia nyenzo zilizowekwa na Mama Kanisa yaani: Sakramenti, ushauri makini, toba na wongofu wa ndani! Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde, amezitaka familia kuwa kweli ni kitalu cha miito mitakatifu, kwa kutoa malezi bora na makini, ili Kanisa liweze kuwapata watawa na mapadre: wema, watakatifu, wachamungu na wachapakazi watakaojitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zao; kwa sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbusha watawa kwamba, maisha yao yanapata chimbuko lake kwa kukutana na Kristo Yesu ambaye ni fukara, mseja na mtii! Hiki ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaohitaji jibu makini bila kumung’unya mung’unya maneno, ili kumfuasa na kumuiga Yesu: fukara, mseja na mtii. Utawa unapania kuyaacha malimwengu na utajiri wake; furaha na anasa zake; ubinafsi na uchoyo wake ili kumwambata Kristo Yesu, Jana, Leo na Daima. Maisha ya kitawa yanasimikwa katika nadhiri ya utii kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha uhuru wa mtu! Ni maisha yanayojazwa kwa amani na Injili ya furaha kwa kuwawezesha wazee kuhitimisha maisha yao kwa furaha inayojikita katika sakafu ya mioyo yao, kwani mikononi mwao, wamemkumbatia Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu anawataka watawa kuhakikisha kwamba, wanamkumbatia Kristo Yesu na kumhifadhi katika ushuhuda wa maisha yao: wakati wa sala, wanapokuwa mezani; wanapokuwa wakizungumza kwa simu; wanapokuwa shuleni wakifundisha na kusoma; wanapowahudumia maskini na wahitaji, yaani, watawa wanapaswa kumkumbatia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kielelezo cha neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao. Ili kuendelea kuwasha moto wa maisha ya kiroho, watawa hawana budi kuhakikisha kwamba, daima wanakutana na Kristo Yesu, kwa kuondokana na litania ya malalamiko yasiyokuwa na “kichwa wala miguu”.

Watawa wajenge utamaduni wa kukutana na Kristo kama vijana na wazee; kaka na dada, ili kuondokana na kishawishi cha kukumbuka daima “masufuria ya nyama na makapu ya vitunguu swaumu” kwa mambo yaliyopita kwani yana madhara makubwa katika moyo wa mtawa! Watawa wajitahidi kuishi siku waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu huku wakiwa na amani na wote! Watawa wajenge utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika ufukara, useja na utii, mambo ambayo kwa walimwengu yanaonekana kana kwamba, yamepitwa na wakati!

Na Sr. Bridgita Samba Mwawasi,SSJ. Mombasa na kuhaririwa na

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

06/02/2018 16:01