2018-02-06 06:57:00

Mwaka wa Mahakama ya Vatican: Umakini na ushirikiano wa kimataifa!


Mji wa Vatican, mbali ya kuwa ni makao makuu ya Kanisa Katoliki ulimwenguni, ni nchi inayojitegemea. Kufuatia umuhimu wa kujiendesha kwa kanuni na taratibu za kisheria, Vatican inao mfumo wa kulinda na kutetea haki. Ingawa mfumo huu haupo kwenye mahusiano ya kimahakama na Jumuiya ya Kimataifa, bado ni mfumo unaotenda kazi katika hali na mazingira yeyote ambapo tunu msingi za amani, haki jamii na utu wa binadamu vinapotishiwa au kutotiliwa maanani. Katika maadhimisho ya uzinduzi wa mwaka wa 89 wa Mahakama mjini Vatican, Professor Gian Piero Milano, Mhamasishaji wa haki wa nchi ya Vatican, siku ya Jumamosi, tarehe 3 Februari 2018, ametoa taarifa yake, ikizingatia pia yaliyojiri ndani ya miaka mitano tangu kupyaishwa kwa mfumo wa taratibu za haki na sheria nchini humo. Upyaisho ulioanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI mnamo mwaka 2013 na kuendelezwa na Papa Francisko.

Kati ya mambo mapya yaliyofanyiwa kazi katika upyaisho huo ni kupenyeza baadhi ya sheria na taratibu za kimataifa katika mfumo wa sheria wa Vatican. Hii imechangia kuthibitisha na kufanya hai tena ule uwepo wa pamoja wa taratibu sheria za kikanisa na za kitaifa katika utendaji wa kutetea haki, amani na utu wa binadamu. Hii inaonesha wazi jinsi gani taratibu sheria za Vatican, pamoja na upekee wake, zipo wazi katika kujadiliana na kuendana na mifumo mingine na hali halisi ya nyakati, historia na mazingira ili kupata suluhu nzuri zaidi na thabiti katika kutetea kanuni na kulinda tunu na mafao ya wote.

Upyaisho wa taratatibu kanuni za nchi ya Vatican umekuwa wa patashika za jasho na muda wa kutosha, miaka mitano sasa, hata hivyo matunda yake yameanza kuonekana, na hata Moneyval, kamati ya kimataifa ya wataalamu wa kutathimini hatua madhubuti za kutokomeza utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi, imethibitisha ubora wa mabadiliko wa taratibu hizo. Mafanikio haya yamefikiwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya watu wa usalama, uchunguzi na mahakama nchini Vatican, amesema Professor  Gian Piero Milano.

Kazi iliyofikiwa mpaka sasa ni nzuri sana, hata hivyo ni lazima kuchukua tahadhari kwa wahusika wote, wasije wakabweteka. Tahadhari hii inaendana na taarifa iliyotolewa na Moneyval mnamo Desemba 2017, katika mkutano mkuu wa tatu katika kutathimini suala la utakatishaji fedha Vatican. Moneyval imekosoa zaidi utaratibu wa kuwashughulikia watakatishaji fedha wa Vatican, hasa kwa sababu walikuwa hawashitakiwi mahakamani. Professor  Gian Piero Milano anatoa jibu kwamba, mfumo wa uendeshaji taasisi za Vatican ni tofauti na mifumo ya uendeshaji taasisi za mataifa mengine, hasa kwenye upande wa benki. Taarifa za uhakika zinazoweza kupatikana na mfumo wa uendeshaji kesi unahitaji umakini mkubwa kabla ya kumshitaki mtu kwa kosa fulani, hasa kwa makosa ya utakatishaji fedha.

Ikumbukwe pia kwamba, uchumi wa Vatican ni wa hadhara na wa upande mmoja; yaani ni uchumi usio maficho na hauna wawekezaji wala wafanya biashara. Wateja wa benki ya Vatican ni wakleri, watawa, taasisi za Kanisa, na wafanyakazi katika taasisi hizo; mfumo unaokwepa kwa kiasi kikubwa nafasi ya utakatishaji wa fedha. Pamoja na kupungua sana matukio ya utakatishaji wa fedha Vatican, kati ya mwaka 2013 na 2017, tayari zimetaifishwa Euro 21,847,983.23; Dolla za kimarekani 4,762,850.25; Pound za Uingereza 1,471,949.59; Dolla za Australia 805,174.45; Frank za Uswiss 650, 275.81. Na kwa mara ya kwanza sasa, kufuatia takwimu hizi, limekwishatolewa ombi la kufungua kesi Mahakama ya Vatican dhidi ya utakatishaji fedha. Katika taarifa yake, Professor  Gian Piero Milano anasema, kuna haja ya kuitazama upya sheria ya mwaka 1987 ya mfumo wa Mahakama wa Vatican. Sheria ambayo imefanyiwa mabadiliko mengi mpaka sasa, hasa kweye upande wa utendaji. Bila shaka sheria hii ingefaa kufanyiwa mabadiliko sasa katika ujumla wake.

Kati ya mambo yaliyotiliwa maanani katika taarifa ya Mhamasishaji wa haki nchini Vatican, ni pamoja na makosa yalitendwa na kushughulikiwa kwa haki mpaka sasa, kwa namna ya pekee makosa dhidi ya watu na makosa ya rushwa, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akisisitiza kupiga vita vikali tabia hizo. Kuhusu makosa dhidi ya watu, hasa unyanyasaji wa watoto wadogo, Professor  Gian Piero Milano ameeleza kwamba, taratibu za kesi hizo zinafanyika kwa uangalifu mkubwa kwa kuzingatia pia haki, heshima na utu wa watu wote wanaohusika katika sakata hizo, lengo likiwa kwanza kabisa kutafuta ukweli wa matukio hayo na uwajibikaji wa watuhumiwa. Shughuli hii ni pevu kwa upande wa utaalamu kisheria, lakini pia kisaikolojia kwa wale wote wanaohusika katika nafasi mbalimbali katika jamii. Kwa sababu hiyo, umakini mkubwa unahitajika katika kushughulika nazo.

Takwimu zinaonesha kwamba, kwa mwaka wa Mahakama 2017, kumekuwa na kesi 7 za makosa mbali mbali; kesi za barabarani 247, kati ya hizo 11 wamepatokana na makosa; kumekuwa na mashitaka 4 kutoka mahakama za kigeni; maombi 123 kutoka kwa Mwendesha mashitaka wa nchi ya Italia, kati ya hayo 7 yamerudishwa kwa sababu Mahakama ya Vatican haikuwa na mamlaka ya kuendesha mashitaka hayo; pia zimesajiliwa ndoa 296, raia wapya 88 na marehemu 20. Kesi zingine zilizokuwapo ni za uharibifu na ugushi sehemu kama Kanisa kuu la Mt. Petro, Maktaba za Vatican na Duka la Dawa. Taarifa za uchunguzi kutoka kwa vyombo vya usalama, zimegundulika tetesi chache za kujihusisha na dawa za kulevya na utekaji, mpaka sasa tuhuma mbili ni za kweli na zimefanyiwa kazi. Ikumbukwe kwamba, nchi ya Vatican, ina raia ambao ni vizazi vya familia kongwe za tangu Nyakati za Kati. Kumbe kesi na tuhuma hizi tajwa, zinahusisha pia raia wa namna hiyo, ingawa wakleri na watawa pia wanaweza kuwemo.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.