Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya latoa tamko kuhusu hali ya Kenya!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limetoa tamko kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, haki msingi za binadamu pamoja na utawala wa sheria kadiri ya Katiba ya nchi ya Kenya. - REUTERS

06/02/2018 15:46

Dhamana na wajibu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya ni kuhakikisha kwamba umoja, amani na uhuru wa kweli vinatawala katika maisha ya familia ya Mungu nchini Kenya. Kanisa linapenda kujikita katika mchakato mzima wa upatanisho wa amani, utulivu na mafungamano ya kitaifa ili kudumisha haki kwa wote! Haya ndiyo mambo makuu yatakayovaliwa njuga na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka 2018.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, matatizo, changamoto na kinzani zinazojitokeza miongoni mwa familia ya Mungu nchini Kenya zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa njia ya amani. Ikumbukwe kwamba, hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani! Kampeni ya Kwaresima kwa Mwaka huu inazinduliwa kwenye Jimbo kuu la Mombasa, tarehe 10 Februari 2018. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika tamko lake, lililotiwa mkwaju na hatimaye kusomwa na Askofu Philip Anyolo, linasikitika sana kutokana na matukio ya uvunjifu wa haki na amani yanayoendelea kujitokeza nchini humo.

Vyama vya upinzani pamoja na serikali iliyoko madarakani, vimeendelea kufanya vitendo vinavyokiuka Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni Sheria Mama! Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitika kusema kwamba, kufungwa kwa baadhi ya vituo vya televisheni wakati Kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Bwana Raila Odinga alipojiapisha kuwa Rais wa wananchi ni kitendo kinachokwenda kinyume cha uhuru wa wa vyombo vya habari na haki ya watu kujieleza kadiri ya Katiba ya nchi. Hatua hizi za serikali ni kutaka kurudisha nyuma maendeleo makubwa yaliyokwisha kupatikana katika mchakato mzima wa utekelezaji wa Katiba mpya ya Kenya mintarafu masuala jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, Katiba ya Nchi na Itifaki za kimataifa zilizoridhiwa na Serikali ya Kenya zinapaswa kuzingatiwa kadiri ya Ibara ya 34 ya Katiba ya Nchi. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinayo dhamana ya kuhabarisha, kuelimisha familia ya Mungu nchini Kenya na kwamba, Serikali inayo wajibu wa kuhakikisha kwamba, habari hizi zinatolewa katika mazingira ya amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linakazia umuhimu wa Mamlaka ya Mawasiliano Kenya kutekeleza wajibu wake katika uhuru kamili bila kuingiliwa na serikali, siasa au masuala ya mafao ya kibiashara, wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wake. Ili Mamlaka ya Mawasiliano Kenya iweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake, haina budi kuzingatia tunu msingi za kitaifa, sheria na kanuni za utawala bora na huduma kwa jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linaitaka Serikali na Upinzani kwa upande mwingine, kuhakikisha kwamba, vinalinda na kudumisha misingi ya haki, amani na mafungamano ya kitaifa, ili kulinusuru taifa kutokana na mpasuko mkubwa ambao umesababishwa kwa kiasi fulani na mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita. Ikumbukwe kwamba, Sheria ni msumeno na hakuna mtu au taasisi yoyote ile ambayo iko juu ya Sheria. Maaskofu wanaitaka familia ya Mungu nchini Kenya kuhakikisha kwamba, inajikita katika misingi ya Katiba ya nchi, kwa kuheshimu na kuthamini haki msingi za binadamu na uhuru wa kujieleza. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, liko tayari kusaidia mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Kenya, ili kukabiliana fika na changamoto zilizoko kwa sasa anasema, Askofu Philip Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

06/02/2018 15:46