2018-02-06 16:21:00

Askofu mkuu Fridolin Ambongo Besungu ateuliwa kuwa Askofu mwandamizi


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Mkuu Fridolin Ambongo Besungu, OFM, Cap. wa Jimbo Kuu la Mbandaka-Bikoro na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Bukungu-Ikela, kuwa Askofu mwandamizi mrithi wa Jimbo kuu Katoliki la Kinshasa, nchini DRC. Askofu mwandamizi mrithi Fridolin Ambongo Besungu alizaliwa tarehe 24 Januari 1960. Baada ya masomo na majiundo yake kitawa, kunako mwaka 1987 akaweka nadhiri zake za daima kwenye Shirika la Ndugu Wadogo Wakapuchini na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1988. Baadaye aliendelea na masomo ya juu na hatimaye, kujipatia Shahada ya Uzamivu wa Taalimungu maadili kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Alfonsiana.

Tangu wakati huo, alibahatika kuwa Paroko usu tangu mwaka 1988 hadi mwaka 1989. Aliwahi kuwa Jaalim la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kinshasa; Mkuu wa Shirika na Makamu Mkuu wa Shirika nchini DRC. Amewahi pia kuwa Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Kitawa Kitaifa nchini DRC, ASUMA na Mkuu wa Wakapuchini Barani Afrika, CONCAU. Akateuliwa na hatimaye kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Bokungu-Ikela tarehe 6 Machi 2005. Baadaye aliwahi pia kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Kole, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani Baraza la Maaskofu Katoliki DRC. Aliwahi kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo kuu la Mbandaka-Bikoro kabla ya kuteuliwa na Papa Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo hilo. Tangu mwezi Juni 2016 amekuwa pia Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.