2018-02-05 15:06:00

Rais wa Uturuki akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 5 Februari 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, ambaye baadaye alibahatika kukutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na Rais wa Uturuki, wamekazia uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Uturuki; hali ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Uturuki; umuhimu na dhamana ya kuwakaribisha na kuwahudumia wakimbizi pamoja changamoto zake. Viongozi hawa wawili wamegusia hali ilivyo huko Mashariki ya Kati na kwa namna ya pekee kuhusu umuhimu wa Mji wa Yerusalemu pamoja na mchakato wa kukuza na kudumisha amani na utulivu huko Mashariki ya Kati kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kuheshimu na kuzingatia haki msingi za binadamu na Sheria za Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.