Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Maparoko wafunzeni waamini wenu kuabudu vyema!

Papa Francisko anawaalika Maparoko kuhakikisha kwamba, wanawafunda vyema waamini wao jinsi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu katika hali ya ukimya na sala.

05/02/2018 15:28

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 5 Februari 2018, katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Agatha, shahidi na bikira, amewataka waamini kutambua historia ya maisha yao, tayari kufanya hija ili kuupanda Mlima wa Bwana, ili kuimarisha Agano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake. Hili ni Agano ambalo Mwenyezi Mungu alifunga na watu wake kwa kuwapatia Amri na Maagizo kama kielelezo cha utambulisho wao.

Mfalme Sulemani alilipandisha Sanduku la Agano na kuliweka mahali pake, yaani Patakatifu pa patakatifu. Waandishi walizinyambulisha Amri za Mungu kiasi hata cha kuwa ni mzigo mkubwa kwa Waisraeli. Yesu anatoa muhtasari wa Amri za Mungu kwa kukazia upendo kwa Mungu na jirani kama muhtasari wa mafundisho yake makuu kwa wafuasi wake! Ndani ya Sanduku la Agano kulikuwemo na Mbao zilizoandikwa juu yake Amri za Mungu. Waisraeli wakapata mahali pa kusali, kutafakari na kumwabudu Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao. Huu ni mwaliko kwa Mapadre  na hasa Maparoko kuhakikisha kwamba, wanafunda waamini wao jinsi ya kusali vyema, kumtukuza, kumwimbia na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa njia ya ukimya, ili kujifunza kujiachilia bila ya kujibakiza mbele ya Mwenyezi Mungu.

Tangu wakati huu, anasema Baba Mtakatifu waamini wanapaswa kufundwa jinsi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu kama itakavyokuwa huko mbinguni, yaani sala katika kumwabudu Mungu. Waamini watambue kwamba, wameteuliwa na Mwenyezi Mungu kutoka katika umati mkubwa wa watu wa Mataifa, watu ambao wamepewa ahadi ambayo imejikita katika sakafu ya moyo wao, tayari kupanda kwa ajili ya kumwabudu Mwenyezi Mungu. Hii ni hija ndefu na ngumu katika maisha, lakini inawezekana kwenda kumwabudu Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mbele ya Mwenyezi Mungu, mwamini anakosa maneno na Mfalme Sulemani anabahatika kusema maneno mawili tu: Kusikiliza na Kusahamehe. Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kuwataka waamini kumwabudu Mwenyezi Mungu katika hali ya ukimya kwa kutambua historia iliyoko mabegani mwao, ili kuomba fadhila ya kusikiliza na kusamehe. Waamini wajitaabishe kutumia muda mrefu kidogo ili kusali sanjari na kujikumbusha hija ya maisha yao ya kiroho, neema ba baraka ambazo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu; neema ya kuteuliwa na Mwenyezi Mungu, ili kushirikishwa katika Agano na Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, kupanda juu mlimani ili kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa kuonesha unyenyekevu ili sala iweze kuhitimishwa na maneno makuu mawili “Kusikiliza na Kusamehe”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

05/02/2018 15:28