2018-02-05 08:14:00

Papa asema, miujiza ya Yesu ilipania kuamsha imani, toba na wongofu


Injili ya Jumapili ya V ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa ni mwendelezo wa maisha na utume wa Kristo Yesu huko Kapernaumu na kwa namna ya pekee, Mwinjili Marko anakazia uhusiano uliopo kati ya utume wa uponyaji na mwamko wa imani kwa wagonjwa wanaokutana na Kristo Yesu, wakiomba huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huduma ya uponyaji inayotekelezwa na Kristo Yesu kwa wagonjwa mbali mbali inahitaji jibu la imani thabiti kutoka kwa wahusika. Hiki ni kiini cha tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 4 Februari, 2018 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Kristo Yesu aliianza Siku ya Sabato kwa kumponya mkwewe Simoni aliyekuwa kitandani hawezi kwa homa na kuhitimisha Siku hii kwa kuwaponya wagonjwa mbali mbali waliofika mahali alipokuwapo. Huu ni umati mkubwa wa watu uliokuwa unateseka kutokana magonjwa ya kimwili na maisha ya kiroho, maeneo muhimu sana katika utume wa Kristo Yesu, alioutekeleza kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo, kwa kuwaganga, kuwaponya na kuwafariji wale wote waliokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Yesu alitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya watu pamoja na watu kwa ajili ya watu wa Mungu na kwamba, sehemu kubwa ya maisha yake ya hadhara daima alikuwa kati ya watu. Hawa ni watu waliokuwa wanaelemewa na shida pamoja na changamoto mbali mbali za maisha: hali inayoonesha umaskini na udhaifu wa binadamu unaoguswa na kupyaishwa na nguvu ya Kristo Yesu, kiasi cha kushinda na watu hawa hadi majira ya jioni. Baba Mtakatifu anasema, hata alfajiri na mapema sana, Yesu akaondoka, akatoka kwenda zake mahali pasipokuwa na watu ili aweze kupata mwanya wa kusali katika ukimya na upweke.

Huu ni ushuhuda kwamba, maisha na utume wa Kristo Yesu, haukufumbatwa katika utukufu na fahari ya miujiza aliyoitenda kutokana na nguvu yake ya Kimungu. Bali,  miujiza ilikuwa ni alama iliyokuwa inahitaji jibu makini la imani; matendo ambayo daima yalikuwa yanaandamana na maneno ili kuamsha imani, toba na wongofu wa ndani, kielelezo cha neema ya Mungu iliyokuwa inamiminika kutoka kwa Kristo Yesu. Yesu aliendelea na utume wake kwa kuhubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya na kutoa mapepo, kielelezo cha uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya watu wake.

Wanafunzi wake, walienda kumtafuta mahali pa faragha, alikokuwa “amejichimbia” ili kusali, ili kujichotea nguvu na ari ya kusonga mbele ili kuwatangazia watu furaha ya Injili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ndio unaopaswa kuwa ni mwelekeo wa hija ya maisha ya kila Mkristo, yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa kutoka kifua mbele, ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Mwishoni, Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, nyota ya uinjilishaji mpya, awasaidie waamini kuwa wazi na wasikivu wa sauti ya Roho Mtakatifu anayelisukuma Kanisa kujichimbia kati ya watu, ili kutangaza na kushuhudia nguvu ya uponyaji na faraja kutoka kwa Kristo Yesu mganga wa roho na mwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.