Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Ushindi wa Kristo Yesu unafumbatwa katika Fumbo la Msalaba!

Ushindi wa Kristo Yesu juu ya dhambi na mauti unafumbatwa katika unyenyekevu, mateso, kifo na ufufuko kutoka wafu na wala hakuna njia ya mkato! - AP

03/02/2018 08:26

Ishara ya Msalaba ni ishara inayotoa muhtasari wa ukombozi wetu. Tumekombolewa kwa njia ya Msalaba; yaani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kwa njia ya msalaba mwanadamu anapokea matunda ya ukombozi na kwa njia ya msalaba anaendeleza duniani kazi ya ukombozi ya Kristo mpaka atakapokuja tena. Ishara hii ya ukombozi ni ishara pia ya ushindi mkubwa wa Kristo kwa njia ya mateso na njia kujishusha mno. Anaeleza Mtume Paulo kuwa Kristo aliyekuwa yuna namna ya Mungu alijifanya hana utukufu akatwaa namna ya utumwa tena alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya Msalaba (rej. Waf. 2:6-11). Maandiko Matakatifu katika dominika ya tano ya mwaka B wa Kanisa yanatualika tuitafakari njia hii ya Kristo: ushindi kwa njia ya mateso na kujishusha. Ni masomo ambayo pia yanatupa nafasi ya kuona na kuupokea mpango wa Mungu katika maisha yetu hasa katika nyakati ngumu za maisha na nyakati zinazotunyenyekesha.

Masomo kwa ufupi

Somo la kwanza (Ayubu 7:1-4,6-7) ni somo linalomwelezea mtu mmoja aitwaye Ayubu. Huyu alikuwa tajiri na machoni pa Bwana alikuwa ni mwadilifu na mwenye haki. Ayubu alipata maafa; mali na wanawe wote wakafa naye pia akapatwa na ugonjwa mbaya mwili mzima. Majirani za Ayubu hawakuamini kabisa kama mtu mwadilifu na mwenye haki machoni pa Bwana anaweza kupata matatizo. Hayo waliamini huwapata wadhambi tu. Katika somo hili la kwanza  Ayubu anatoa malalamiko yake mbele ya Mungu. Anaiangalia hali yake na anaona hana dhambi ila Mungu ameamua tu kumpitisha katika mateso na Ayubu hajui ni kwa sababu gani. Anasema Mungu asingekuwa na sababu ya kumpatia mateso hayo kwa kuwa hata maisha yake duniani ni mafupi “maisha yangu ni upepo, jicho langu halitaona mema tena”.

Somo la Pili (1Kor. 9:16-19, 22-23) Mtume Paulo anaeleza siri za utendaji wa kazi zake za kitume. Huyu ndiye Mtume ambaye huenda amefanya kazi kubwa kuliko wengine katika kuinjilisha watu wa mataifa. Alifanya safari nyingi za kitume na barua alizoandika zinabeba karibu nusu ya vitabu vya Agano Jipya.  Siri hizo ni kwamba kwanza alijizuia kutumia uhuru aliokuwa nao ili afungwe na kazi moja tu ya kuhubiri injili. Pili, alijifunza kuwachukulia watu kadiri ya hali zao na kuwafikishia Habari Njema ya wokovu kadiri ya hali zao. Kama anavyosema “nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu”. Ni mtendaji anayejitahidi kuyaingia mazingira ya watu anaowahudumia ili ayaelewe na kisha kuyaelewa anakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuwahudumia. Kwa maneno ya Baba Mtakatifu Francisko huyu ni mchungaji asiyeogopa harufu ya kondoo katika kuwalisha!

Somo la Injili (Mk. 1:29 - 39) linaonesha kazi anazozifanya Kristo kutangaza ufalme wa Mungu; kazi za uponyaji wa wagonjwa, utoaji mapepo na kuhubiri. Yesu anafika nyumbani kwa Simoni na Andrea anamponya mkwewe Simoni. Kisha anaendelea na kuwaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali na wenye mapepo ambao waliletwa kwake. Tunaona pia kuwa Kristo anawakataza pepo wasiseme kuwa yeye ni nani; “...wala hakuwaacha pepo kunena kwa sababu walimjua”. Hata watu walipozidi kumfuata hakupenda kuendelea kukaa kwao bali aliondoka kwenda mahali pengine ili ahubiri na huko nako. Miujiza na maajabu aliyokuwa akiyafanya Yesu yalimtambulisha kuwa ndiye Masiha na yaliashiria mwanzo wa ufalme wa Mungu na kushindwa kwa enzi ya yule mwovu shetani. Lakini Yesu anataka kuonesha kuwa hajaja kumshinda shetani kwa njia za kimiujiza, za umaarufu au ushujaa katika vipimo vya ulimwengu. Anataka kuonesha kuwa amekuja kumshinda shetani kwa njia nyenyekevu, njia ya mateso na kifo msalabani.

Tafakari

Mateso ya Ayubu yanatupa nafasi ya kuyaangalia upya mateso ya ubinadamu wetu. Tangu mwanzo historia ya mwanadamu imeambatana na mateso mbalimbali. Haya yamemwijia mwanadamu kwa njia ya magonjwa, ugumu wa maisha, migogoro, vita, mauaji na njia nyingine nyingi kadha wa kadha. Na mateso haya mwanadamu ameyapokea kwa mitazamo tofauti tofauti. Ipo mitazamo inayoona kuwa mateso ya mwanadamu yanaletwa na mwanadamu mwenyewe. Ni katika namna anavyochagua na kufanya maamuzi, katika vipaumbele vyake na matendo yake kwa ujumla anajikuta au amejisababishia mateso ama amewasababishia wengine mateso. Katika mtazamo huu utatuzi humtegemea mwanadamu pekee. Hawa hufungamanisha maisha katika hekima, busara, kazi, maarifa na kadhalika kama namna ya kuepuka kuteseka maishani na namna pia ya kujikwamua katika mateso.

Ipo pia mitazamo inayoona kuwa mateso ya mwanadamu ni matokeo ya nguvu iliyo nje ya binadamu. Wapo wanaoona mateso yanaletwa na shetani na ni matokeo ya ubaya wake kwa mwanadamu. Na wapo wanaoona yanaletwa na Mungu kwa au kwa sababu ya dhambi za watu ama ili kuwajaribu. Mtazamo huu huona kuwa ili mwanadamu aepuke mateso anapaswa kutumia nguvu zilizo nje yake. Katika kundi hili ndio tunawapata wanaotumia waganga wa kienyeji na mbinu mbalimbali za kishirikina ili kujikinga. Kwa bahati mbaya baadhi ya wahubiri na viongozi wa madhehebu huangukia kundi hili hasa pale wanaposisitiza injili ya raha na utajiri, uponyaji wa hadhara na utatuzi kimiujiza wa mateso yote ya mwanadamu kwa kuwa na imani na kutoa sadaka nzuri. Wapo pia wanaomkimbilia Mungu kwa dhati wakiomba ulinzi na msaada wake katika nyakati za mateso.

Kanisa hutufundisha kuwa mateso katika maisha ni sehemu ya ubinadamu wetu, ubinadamu ambao ni dhaifu na unaotegemea daima kuimarishwa na kukamilishwa na Mungu pekee. Mt. Augustino anasema Mungu ametuumba kwa ajili yake na kwamba mioyo yetu haitotulia hadi inapotulia kwake.  Mateso sio hali inayomtenga mtu na Mungu. Kinyume chake mateso ni nafasi ya mtu kuzidi kumkaribia Mungu. Mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu hauko kimahesabu hivi kwamba wenye haki machoni pake watakingwa na mateso ilhali wasio haki machoni pake ndio tu watakaopata mateso. Tumemwona Ayubu katika somo la kwanza akikiri kuwa anateseka si kwa sababu ya dhambi alizofanya bali ni Mungu tu ameruhusu ateseke. Kwa nini Mungu ameruhusu hivyo, Ayubu hajui!

Kuyaona mateso kama kitu kilicho ndani ya uwezo wa mwanadamu peke yake hakufikii ukomo alioufunua Kristo na kuuthibitisha kwa kifo chake msalabani pale alipoyageuza mateso kuwa njia ya wokovu. Kwa ufunuo huu mwanadamu haalikwi tu kutumia hekima, akili na uwezo aliopewa na Mungu kukabiliana na mateso maishani bali pia anaalikwa kuyaunganisha mateso hayo na mateso ya Kristo msalabani kwa ajili ya kujipatia matunda ya wokovu na kwa ajili ya kuendeleza kazi ya ukombozi ya Kristo.

Tunadhani hakukuwa na njia nyingine ya kumwokoa mwanadamu isipokuwa njia inayonyenyekesha ya msalaba? Kwa miujiza mingi aliyofanya Yesu alionesha kuwa angeweza kumwokoa mwanadamu kwa njia hizo ila kwa mapenzi yake ameamua kutumia njia ndefu, ngumu na inayonyenyekesha. Njia ya msalaba. Ndivyo anavyotukumbusha kuwa katika mateso hakuna njia ya mkato. Tunapaswa kusimama imara katika imani na kuweka kwake tumaini kuomba mapenzi yake yatimizwe katika maisha na hasa katika hayo anayoruhusu tuyapitie. Neema ya Mungu ituimarishe katika nyakati za mateso maishani mwetu na kwa njia hiyo tuufikie uzima wa milele.

Bikira Maria malkia wa Mateso, utuombee.

Pd. William Bahitwa,

VATICAN NEWS.

03/02/2018 08:26