2018-02-03 16:45:00

Mahakama zitambue na kuheshimu utu wa binadamu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 3 Februari 2018 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Bikira Maria, Mama wa familia kwa ajili ya kuzindua Mwaka wa 89 wa Mahakama ya mji wa Vatican. Katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa wadau katika utekelezaji wa sheria na haki kutambua kwamba, daima mbele yao kuna binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anayepaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Kwa upande wake, Professa Gian Piero Milano, Mhamasishaji wa amani mjini Vatican amepembua kwa kina na mapana shughuli mbali mbali za utekelezaji wa haki mintarafu: kanuni maadili, kanuni na sera za kisiasa kimataifa; Mafundisho Tanzu ya Kanisa pamoja na Sheria za Kanisa kama vyanzo vya utekelezaji wa haki mjini Vatican. Vatican katika utekelezaji wa dhamana hii, inaendeleza utume wake katika maisha ya kiroho kwa kukazia, ukweli, uwazi, uaminifu na uwajibikaji makini unaofumbata dhana, ari na moyo wa kisinodi, ili kupanga, kuamua na kutekeleza kwa pamoja! Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika sheria za Kanisa, kielelezo cha mchakato wa ushirikiano na mshikamano wa kitaifa na kimataifa unaotekelezwa na Vatican, ili kupambana kikamilifu na uhalifu wa kifedha kwa kutunga sheria inayopambana na utakatishaji wa fedha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Mambo yote haya ni sehemu ya usalama wa mji wa Vatican unaosimama kidete pia kulinda na kudumisha uhuru, haki na amani. Hapa mkazo ni umakini, ukweli na uwazi na taarifa za kifedha, pamoja na kushirikiana na wadau mbali mbali wa kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha kwamba, kanuni maadili, ukweli na uwazi vinazingatiwa kikamilifu, ili fedha na mali ya Kanisa visaidie katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Professa Gian Piero Milano katika hotuba yake elekezi anasema, uhalifu na uvunjaji wa sheria, kanuni na tunu msingi za kimaadili ni mambo yanayohitaji kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kwa kujizatiti katika kujenga na kukuza tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kimaadili. Ametumia fursa hii kuorodhesha shughuli mbali mbali zilizotekelezwa na Mahakama ya Vatican kwa kipindi cha mwaka 2016/ 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.