Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Ufafanuzi kuhusu makosa makubwa ya uhalifu, "Delicta graviora"

Kuna makosa ya uhalifu mkubwa "Delicta graviora" yanayoshughilikiwa moja kwa moja na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. - EPA

02/02/2018 08:08

Mama Kanisa katika kuendeleza Utume wake wa kutaka kudhibiti uhalifu unaoweza kutendwa na waamini: lengo likiwa ni kumrekebisha mhalifu; kutenda haki kwa waliokosewa; na kuondoa kashfa (Rej. CIC, c. 1341). Kati ya makosa ya uhalifu, yapo yale ambayo yanatambuliwa kuwa ni makosa makubwa ya uhalifu, Delicta graviora, na yametengwa ili kushughulikiwa, sio tena na Askofu Jimbo wala Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume, bali na Mahakama maalumu ya Baba Mtakatifu.

  

Mahakama hiyo ni Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Makosa husika yanayoshughulikiwa na Mahakama hiyo ni makosa dhidi ya Sakramenti ya Kitubio, dhidi ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na dhidi ya Amri ya sita ya Mungu. Kuhusu Sakramenti ya Kitubio, makosa ambayo mchakato wake umetengwa ili kushughulikiwa na Kiti Takatifu, yaani Mahakama ya Baba Mtakatifu ni: makosa ya padri kuvunja siri ya kitubio, kumtongoza kimapenzi kwa maneno au ishara mwamini anayekuwa katika kitubio, au kutumia kwa namna yeyote maongezi ya kwenye kitubio kwa kumuumiza aliyetubu kwake.

Kwa upande wa Ekaristi Takatifu, ni kukejeli au kutoweka heshima kwa Sakramenti hiyo kwa nia ya kukufuru. Kosa hili laweza kutendwa ama na waamini walei ama na wakleri. Makosa dhidi ya Amri ya sita ya Mungu, yanawahusu wakleri wanaojihusisha na masuala ya ngono dhidi ya watoto wadogo hata kama ni kwa njia ya mtandao, pedopornographia (CIC, c. 1395§2)

Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo mwaka 2001 kwa Barua binafsi Motu proprio, Sacramentorum sanctitatis tutela, yaani Ulindaji wa Utakatifu wa Sakramenti, alitoa taratibu za mchakato wa kuendesha kesi hizo katika Mahakama za Kanisa. Mnamo mwaka 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa Tamko, Reformatio Normae gravioribus delictis, juu ya marekebisho ya kanuni za makosa makubwa ya uhalifu, aliziboresha taratibu hizo kwa baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa havikueleweka barabara!

Na Padre Celestine Nyanda,

Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana.

Vatican News!

02/02/2018 08:08