Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Siku ya XXII ya Watawa Duniani: Matumaini, Changamoto na Ushuhuda!

Siku kuu ya watawa ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa zawadi kubwa ya miito ndani ya Kanisa, kutathmini matatizo na changamoto zake ili kuzitafutia ufumbulizi wa kudumu. - AFP

02/02/2018 15:03

Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa watu wa Mungu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na Kanisa lake katika maisha na utume wao, ili kweli Yesu aweze kuwa kati pamoja na watu wake, ili kuwakirimia matumaini na furaha tele katika maisha! Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza mapadre na watawa katika maisha na utume wao, kwa njia ya sala na sadaka zao za kila siku, ili kweli watu hawa waweze kujitosa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa njia ya karama za mashirika yao ambayo kweli ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, uaminifu kwa wito na maisha ya kitawa pamoja na uaminifu kwa karama ya Shirika ni kati ya changamoto kubwa zinazowakabili watawa katika maisha na utume wao! Bado kuna kinzani na migogoro kati ya watawa na wakleri hasa kutokana na uelewa finyu wa taalimungu ya kikanisa! Kuna changamoto za kitamaduni na kimalezi, lakini watawa wakumbuke kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, matumaini, huruma na upendo kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia! Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya kuwekwa wakfu ndani ya Kanisa.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la asilimia 20% ya miito katika Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Barani Afrika, mambo ambayo wachunguzi wa mambo wanasema, yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na masuala ya: kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni. Lakini, jambo la msingi ni kwa walezi kuhakikisha kwamba, wanakuwa makini katika kuwachagua vijana wanaotaka kujisadaka katika maisha ya kitawa, waaminifu kwa karama za mashirika yao sanjari na kuzingatia kanuni, taratibu, sheria na miongozo ya malezi, ili kweli Kanisa liweze kupata watawa na mapadre: wema, watakatifu, wachamungu na wachapakazi.

Vijana wa kizazi kipya wasaidiwe kukuza wito wao, ili kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa: mtii, fukara na mseja kamili, tayari kushiriki katika maisha na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Katika maisha na utume wa kitawa kuna changamoto, magumu na raha zake, jambo la msingi ni kukuza na kudumisha umoja, udugu, upendo na mshikamano wa dhati; mambo yanayorutubishwa kwa: Sala ya Kanisa, Sakramenti za Kanisa, Tafakari na Maisha ya kidugu! Kwa njia hii, watawa wataweza kupata utimilifu wa maisha yao na hivyo kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na furaha inayomwilishwa katika huduma makini kwa familia ya Mungu! Watawa na mapadre watambue na kuthamini useja kama alama ya matumaini kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake.

Uongozi ndani ya Mashirika ya kitawa na kazi za kitume uwe ni ushuhuda wa huduma na sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti kutokana na sababu mbali mbali katika maisha yao! Watawa na mapdre watambue kwamba wao ni alama ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Watawa waoneshe kwamba, inawezekana kuishi kwa amani, upendo, umoja na mshikamano wa kidugu licha ya tofauti za makabila, mahali anapotoka mtu, uwezo wa kielimu na hata pengine kiuchumi! Yote haya ni kwa ajili ya sifa, utukufu na heshima ya Mwenyezi Mungu, asili ya miito yote ndani ya Kanisa.

Padre Timothy Radcliffe kutoka Shirika la Wadominican anasema, maisha na utume wa kitawa ni changamoto inayowataka watawa wenyewe kuhakikisha kwamba, wanajikita katika ukamilifu wa maisha kwa kuzingatia mambo msingi yanayoweza kuwapatia furaha ya kweli, amani na utulivu wa ndani. Changamoto za kitamaduni zishughulikiwe kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, mashirika ya kitawa yanajitamadunisha katika mazingira ya watu wanaowahudumia, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Ili kufikia lengo hili katika maisha ya kitawa kuna haja ya kuwa na “moyo wazi kabisa” “latitudo cordis” ili kupokea na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Mashirika mbali mbali ya kitawa yawe na utambulisho wake unaopata chapa ya kudumu kutoka katika karama na huduma kwa watu wanao wahudumia, kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Padre Pascual Chavez Villanueva katika makala ya maadhimisho ya Siku ya XXII ya Watawa Duniani kwa Mwaka 2018 anakazia zaidi umuhimu wa kuwafunda walezi, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kurithishwa uzuri, utakatifu na sadaka ya maisha ya kitawa kwa watu wa nyakati hizi. Utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ukarimu na ushuhuda wa furaha ya Injili ni mambo msingi ambayo walezi wanapaswa kuwarithisha vijana wao katika malezi. Jumuiya ya malezi iwe ni shuhuda wa furaha, matumaini, upendo, mshikamano na udugu.

Haya ni mambo msingi yanayofumbatwa katika ile sanaa kufundisha kwa njia ya maisha, kutafuta ukweli na kuwafunda vijana kuwa kweli ni watu wenye furaha moyoni! Vijana wafundwe barabara kuthamini Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, wasaidiwe kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu, kwa kuwa na vipaumbele ambavyo vinapaswa kuvaliwa njuga! Vijana wafundishwe kuona na kutatua matatizo na changamoto za maisha ya kitawa katika mwanga wa Injili ya matumaini, kwa kuheshimu na kuthamini uhuru wa mtu binafsi, dhamiri nyofu kwani hapa ni mahali patakatifu ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake.

Vijana wa kizazi kipya wasindikizwe katika mchakato wa safari ya maisha na wito wao, ili waweze kufanya maamuzi mazito katika maisha. Hapa kuna haja ya kuwa na mwelekeo chanya katika maisha, ujasiri na mang’amuzi thabiti katika maisha. Wingi wa miito upate chimbuko lake katika utume na ushuhuda wa watawa sehemu mbali mbali za dunia! Kwa njia hii, hata vijana wa kizazi kipya wanaweza kuwa na ndoto ya kushiriki katika maisha ya kitawa na kipadre. Vijana wawe tayari kujitoa bila ya kujibakiza ili waweze kufundwa hatua kwa hatua katika maisha na utume wa Mashirika ya kitawa, tayari kushiriki katika mchakato wa kulipyaisha Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Fadhila ya upendo na udugu ni muhimu sana katika mchakato wa mageuzi ndani ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

02/02/2018 15:03