Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Mama Kanisa anainjilisha, ana ganga na kuwatakasa watu wa Mungu!

Mama Kanisa ni ushuhuda wa uwepo wa Mungu. Anatumwa kuwaondolea watu dhambi zao, kuwaganga na kuwaponya magonjwa na udhaifu wao wa mwili, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

02/02/2018 07:26

Mpendwa msikilizaji wa Vatican News! Tungo moja ya nyimbo za dini inakwenda namna hii: “Nikitazama juu angani nikiomba msaada, mateso yananizidi, hakuna anayekuja, nainua mikono yangu naleta sala yangu, Ee Mungu nisaidie, Mungu unihurumie”. Ni tungo inayotupatia taswira ya mwanadamu aliye kwa upande mmoja katika hali ya mateso na kwa upande mwingine inamwonesha akiweka tegemeo lake kwa Mungu. Shida, mahangaiko na taabu huandamana na maisha ya kila siku ya mwanadamu. Wengine huimarishwa katika imani yao lakini wengine huweweseka na kuiacha imani. Pamoja na hayo yote tunapaswa kujiuliza chanzo chake ni nini? Kama Mungu aliumba vyote na akasema kuwa ni vizuri wapi yanapotokea haya? Ninawaalika katika Dominika hii kutafakari juu ya dhana hii.

Tuanze kwa kujiuliza: Je, ipo wapi imani yangu na utegemezi wangu kwa Mungu pale ninapokumbwa na matatizo fulani? Je, ninapokimbilia kwa nguvu nyingine na kumwacha Mungu ni suluisho kwa shida ninazozipata? Je, matatizo niliyonayo yamesababishwa na yeye? Maandiko matakatifu yatuonesha wazi ni wapi unapotokea uovu dhidi ya mwanadamu; si kutoka kwa mwenyezi Mungu bali ni husuda na nia mbaya ya mwovu shetani. Ibilisi ndiye alimpatia Ayubu maswahibu yaliyompata (Rej Ayu 1:9-12). Hivyo chanzo cha uovu hakiwezi kutoka kwa Mungu. Hata katika jamii ya mwanadamu leo hii tunaona hivyo. Ni husuda, wivu, majigambo na chuki za kibinadamu ndizo ambazo zinauharibu ulimwengu huu na kumfanya mwanadamu daima kuwa katika hali ya mahangaiko. Katika ujumla wake tunaweza kuona hali hii katika tendo la mwanadamu kumweka pembeni Mungu na kujitwalia utawala wake binafsi, jambo ambalo linazaa ubinafsi na kuua undugu kati ya watu.

Simulizi la Ayubu katika somo la kwanza ni kielelezo kwetu na jawabu kwa mwitikio wetu wakati wa kukabiliana na maswahibu katika maisha. Imani yake kwa Mungu haiyumbishwi na haya yanayompata. Daima anauona wema wa Mungu na anayachukulia hayo yanayomsibu kuwa hayatoki kwake na mwishoni yatapita na yeye kuendelea kuuonja wema wa Mungu. Anaonesha wazi kwamba mwanadamu kupitia katika maswahibu ni jambo la kawaida na wakati mwingine linakatisha tamaa. Hali hii haimuondoi katika kuweka tumaini lake kwa Mungu. Ayubu aliyekirimiwa mali nyingi na umaarufu mkubwa alipitia katika wakati mgumu sana. Ni kipindi cha majaribu ambacho kilinuia kuipima imani yake. Wote waliomzunguka walimshawishi hata kumtukana Mungu. Lakini yeye aliyaangalia yote katika jicho la imani na kuungana na mzaburi na kutualika akisema: “Msifuni Bwana, huwaponya waliopondeka moyo”. Anakuwa mithili ya Kristo pale juu msalabani katika hali ya mateso makubwa alijikabidhisha kwa Mungu akisema: “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu” (Lk 23:46).

Uasi wa mwanadamu ulimwondoa Mungu katikati ya watu na kuwa chanzo cha mivurugano na taabu nyingi. Uasi huu uliiharibu kazi ya uumbaji na kumfanya mwanadamu kupitia katika hali ya shida. Ujio wa Kristo ulimwenguni unahuisha tena uwepo wa Mungu na hivyo kuwa sababu ya furaha na auheni kwa mwanadamu. Hili linajidhihirisha katika somo la Injili ya leo pale Kristo anapowaponya watu mbalimbali walioletwa mbele yake kwa ajili ya uponyaji. Mama mkwe wa Petro ni mmoja kati ya hawa wanaoponywa na tunaambiwa baada ya kupokea uponyaji “homa ikamwacha, akawatumikia”. Tendo hili linatufundisha jambo muhimu sana juu ya nini kinacholetwa na Kristo na matokeo yanayotegemewa kutoka kwetu sisi. Mama mkwe wa Petro na hawa wengine wanaoponywa wanauwakilisha ubinadamu unaogaragazwa na taabu za ulimwengu huu. Ujio wa Kristo ambao ni utambulisho wa uwepo wa Mungu unaleta auheni. Ujio wa Kristo ulimwenguni ulinuia kumkomboa mwanadamu. Uumbaji wote ambao umekuwa katika hali ya kuvurugika umerudishwa katika uwiano.

Zaidi ya hapo ujio wake unafanya uumbaji uendelee katika hali yake njema. Mama mkwe wa Petro alipoponywa aliwahudumia. Alirudi katika nafasi yake ya kawaida kama mama wahuduma Bila shaka kabla ya kuponywa wageni waliofika wakisongwa na uchovu na njaa kidogo walipoteza matumaini na pia kuugua pamoja naye. Hii ndiyo hali ya ulimwengu wetu pale ambapo bado haujaonja uwepo wa Mungu. Ni mahali ambapo panabaki kutokuwa na matumaini na furaha kwa wenye uhitaji. Uwepo wa Mungu hurejesha furaha na kutoa fursa kwa kila mwanajamii kutimiza wajibu wake kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Haya ni matibabu kwa jamii ya mwanadamu inayogawanyika na inayomwachia kila mmoja ajitafutie auheni yake mwenyewe na matokeo yake ni magomvi, chuki na husuda ambazo kuendelea kumwachia mwanadamu mateso maishani mwake.

Ujio wa Kristo ni uumbaji mpya. Ujio huu mpya unatufanya kuwa wapya na pia kutuweka kuwa vyombo vya kuieneza habari hii njema kwa wote. Hayo tuyaonjayo kwa ujio wake na mwanzo huu mpya yanatusukuma kuwapelekea na wengine ili kwa huduma zetu nao wauone mkono wa Mungu. Mtume Paulo anatuhasa kutumia nafasi hizo na kutenda kwa busara ili kuwafikia wote katika hali zote. “Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu”. Hii ni kuwa mithili ya Kristo ambaye ameitwaa hali yetu ya kibinadamu ili apate kutukomboa. Mwenyezi Mungu anakutuma kwenda kuitangaza Habari Njema na kumrejeshea mwanadamu atesekaye matumaini huku ukimwendea kwa hali yake, lugha yake na namna yake na hivyo kukuelewa vizuri.

Mkristo ni kiumbe kipya. Sakramenti ya Ubatizo inampatia cheo hicho na kwa Sakramenti ya Ekaristi takatifu anaungana kwa karibu zaidi na upendo wa Mungu na hivyo anatarajiwa kutoa miale upendo huo na kuangaza kote. Wapo wanadamu ambao bado wanateseka lakini hawajapoteza matumaini kwa Mungu; wapo ambao ni wagonjwa, wapo waliopoteza wapendwa wao, wapo waliopoteza mali zao. Wote wanamlilia Mungu na wanategemea uponyaji wa ndani. Tunapaswa sisi kuwa vyombo vya kuwarudishia matumaini na kuyapokea yote katika imani. Tutende hayo kwa maneno yetu na mfano wa maisha yetu yanayoakisi ukweli wa Injili kwani Kristo aliye Injili yetu “aliutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu”.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha,

Vatican News!

02/02/2018 07:26