2018-02-01 10:19:00

Vatican inapania kujenga umoja wa waamini na Khalifa wa Mt. Petro!


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuatilia kwa karibu sana maisha na utume wa Kanisa nchini China na mara kwa mara anahabarishwa yale yanayojiri katika maisha na utume wa Kanisa kupitia Sekretarieti kuu ya Vatican. Kumekuwepo na majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya Vatican na Serikali ya China. Huu ni ufafanuzi ambazo umetolewa hivi karibuni na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican kufuatia taarifa zilizokuwa zinataka kuchafua mahusiano kati ya Vatican na Serikali ya China! Katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, umefika wakati wa kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini China kwa kutambua na kuheshimu dhamana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa katika kuteuwa na kuwasimika Maaskofu kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa Katoliki.

Lengo anasema Kardinali Parolin ni kutaka kukuza na kudumisha majadiliano yatakayoondoa dhana ya utengano wa viongozi na waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kwani viongozi wanaoteuliwa na Baba Mtakatifu hawatambuliwi na Serikali ya China na kwamba kuna baadhi ya waamini wa Kanisa Katoliki wasiotambuliwa rasmi na Serikali ya China. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya majadiliano kati ya Vatican na Serikali ya Watu wa China na hatima ya mazungumzo haya ni maisha ya kiroho, yanayoliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato mzima wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo makini cha imani tendaji!

Kumekuwepo na malumbano ya muda mrefu kati ya Kanisa na Serikali ya Watu wa China kutaka Kanisa lipewe nafasi katika mchakato wa maendeleo endelevu ya wananchi wa China: kiroho na kimwili, lakini jitihada hizi bado hazijazaa matunda yanayokusudiwa. Badala yake anasema Kardinali Pietro Parolin, kumekuwepo na madonda na sadaka kubwa ambayo imetolewa, lakini hii haiwezi kuhesabiwa kuwa ni sehemu ya mchakato wa makubaliano ya kisiasa! Pengine, hata kuliko sehemu nyingine yoyote ya dunia, waamini wa Kanisa Katoliki nchini China wamethubutu kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya matatizo, mahangaiko na mateso wanayokumbana nayo kila kukicha!

Kifungu cha umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu mahalia nchini China ni nguzo muhimu sana ya umoja wa Kanisa! Vatican inapenda kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano ili kweli umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu mahalia nchini China uweze kujengwa na kudumishwa mintarafu: Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Mama Kanisa. Ni mchakato unaopania kujenga na kuimarisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji pamoja na miundo mbinu ili kuharakisha mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda makini.

Vatican inatambua na kuthamini mchango, sadaka na mateso ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini China; uaminifu na ukarimu wao kwa Injili ya Kristo ni mkubwa zaidi. Ikumbukwe kwamba, kati ya mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza katika mahusiano kati ya Vatican na Serikali mbali mbali duniani ni kuhusu uhuru wa kuteua Maaskofu mahalia. Hatua hii bado haijafikiwa kati ya Vatican na China, kumbe, kuna haja ya kuvuta subira, kwani kutoelewana bado kutaendelea kuwepo, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kwa subira na uvumilivu.

Changamoto hii itakapokuwa imepatiwa ufumbuzi wa kudumu, hakutakuwepo tena na haja ya kuweka vizuizi vya umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa mahalia. Kanisa litaendelea kukumbuka na kuenzi shida, matatizo na changamoto ambazo waamini wa Kanisa Katoliki nchini China, wamekumbana nazo na kwamba, daima Kanisa litaendelea kushikamana pamoja nao wakati wote katika sala pamoja na kuwasindikiza katika hija ya umoja kamili na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwaandikia barua waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kwa kuwakumbusha kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kanisa linaamini kuhusu uwepo wa nguvu ya Mungu inayotenda kazi kati ya watu wake. Kanisa Katoliki nchini China, linataka kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu na wala si kuwa mbadala wa Serikali ya watu wa China anasema Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Bwana Gianni Valente wa Vatican Insider na kuchapishwa tena na Gazeti la L’Osservatore Romano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.