Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Kifo ni tukio la maisha, urithi na kumbu kumbu hai!

Papa Francisko asema, kifo ni sehemu ya maisha ya binadamu, ni urithi na kumbu kumbu endelevu!

01/02/2018 15:14

Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe Mosi, Februari 2018 ametafakari kuhusu Fumbo la Kifo; wosia wa Mfalme Daudi kwa mwanaye Sulemani na hatimaye, kifo chake, akamtaka ashike mausia ya Bwana, atembee katika njia na Amri zake. Hapa waamini wanakumbushwa kwamba, wanapaswa kuondokana na kishawishi cha kujisikia kwamba, wao ni watawala na wamiliki wa zawadi ya maisha na muda na hivyo kusahau kwamba, wao hapa duniani ni wapita njia na wala hawana makazi ya kudumu.

Kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbu kumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili waweze kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Kifo kitakuja tu kwa wakati wake, kinaweza kuwahi au kuchelewa, lakini mwanadamu akumbuke kwamba, iko siku atakufa tu na hivyo kuungana na wahenga kwenye usingizi wa amani. Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki.

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kufariki dunia, Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

01/02/2018 15:14