2018-01-31 15:18:00

Papa Francisko: Sikilizeni, hifadhini na kumwilisha Neno la Mungu!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uwepo wa Kristo katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu yanajionesha kwa namna ya pekee katika Sadaka ya Misa Takatifu, katika nafsi ya Kasisi na kwamba, anajitoa tena kuwa Sadaka Altareni kwa njia ya huduma ya mapadre na Yupo hasa katika Ekaristi Takatifu; katika Sakramenti ya Ubatizo. Yupo katika Neno lake, kwa kuwa ni Yeye anayesema wakati Maandiko Matakatifu yanaposomwa katika Ibada ya Misa Takatifu. Yupo Kanisa linaposali na kuimba Zaburi na yupo wakati waamini wanapokusanyika kwa ajili yake!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 31 Januari 2018 amefafanua umuhimu wa Liturujia ya Neno la Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu kuwa ni mahojiano kati ya Mwenyezi Mungu na watu wake. Neno la Mungu ni hai linapotangazwa na kusikilizwa kwa imani. Roho Mtakatifu aliyezungumza kwa njia ya Manabii ndiye aliyewawezesha waandishi wa Neno la Mungu kuandika kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, ili kwamba, Neno la Mungu linapotangazwa liweze kusikika katika nyoyo na masikio ya waamini, ili hatimaye, waweze kumwilisha kile walichosikia katika uhalisia wa maisha yao.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa watulivu, wanyenyekevu na wasikivu wakati Neno la Mungu linapotangazwa Kanisani, daima wakiwa tayari kufungua akili na nyoyo zao, ili kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza nao, ili hatimaye, Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha yao. Lakini, inawezekana kwamba, si wakati wote Neno la Mungu linaweza kueleweka mara moja, Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika mazingira kama haya, bado Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na waja wake. Waamini wajenge utamaduni wa ukimya na utulivu wakati maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, kwani Neno hili ni chemchemi ya uhai na maisha mapya; ni mkate wa uzima wa milele na amana ya utajiri kutoka katika Maandiko Matakatifu na kwamba, huu ni utambulisho wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Agano la Kale, Injili na Nyaraka mbali mbali ni utajiri mkubwa unaofumbata Neno la Mungu. Zaburi, Wimbo wa katikati na nyimbo zote zile zinazotumika kupamba Liturujia ya Neno la Mungu ni muhimu sana katika kuwasindikiza waamini kuliishi Neno la Mungu. Wakati wa Liturujia ya Neno la Mungu, si muda muafaka wa kusoma magazeti au habari za udaku! Neno la Mungu lipewe heshima, kwani hapa ni majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake. Mimbari ipewe heshima inayostahili na kwamba, wasomaji wa Neno la Mungu waandaliwe vyema na wafanye mazoezi, ili Neno liweze kusomwa na kusikika vizuri zaidi. Kwa njia hii, kweli Neno la Mungu linakuwa ni taa ya miguu ya waamini na mwanga katika njia zao, wanapokuwa katika hija ya maisha ya hapa duniani. Neno hili lisikilizwe kwa makini na kuzamishwa katika sakafu ya nyoyo za waamini, ili hatimaye, liweze kuzaa matunda yanayokusudiwa na kwamba, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kutoa majibu kadiri ya nafasi ya uwezo wa mwamini mwenyewe.

Roho Mtakatifu anahitaji nyoyo za waamini zenye udongo mzuri, mahali ambapo ataweza kupandikiza mbegu ya Neno la Mungu, ili Neno hili liweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Neno la Mungu anasema Baba Mtakatifu linapaswa kutembea katika maisha ya waamini yaani kwa kulisikiliza, kulizamisha katika sakafu ya moyo na hatimaye, kulifanyia kazi. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuthaminiwa katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, pale Mwenyezi Mungu anapofanya majadiliano na waja wake! Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa Kitaifa  na Watawa wa Shirika la Yesu na Maria. Wote hawa amewatia shime ya kuhakikisha kwamba, wanaishi utume wao katika ukweli, huku wakionesha na kushuhudia Injili ya huduma na uwakilishi uliotukuka! Majiundo makini ya watu, yawasaidie kutumia vyema karama zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.