2018-01-31 07:02:00

Papa Francisko: Kipaumbele cha Kanisa Perù: Uinjilishaji wa Amazonia


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Umoja wa Matumaini” Jumapili, tarehe 21 Januari 2018, baada ya kutoa hotuba yake kwa Maaskofu, alipata tena muda wa nusu saa ushee! kujibu maswali na dukuduku za Maaskofu Katoliki Perù. Amekazia kwa namna ya pekee, Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia; umuhimu wa Maaskofu kuwa karibu sana na wakleri wao; kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kiutu, kijamii na kimaadili kutokana na kukithiri kwa saratani ya rushwa Amerika ya Kusini. Mambo yote haya yamezungumzwa na Baba Mtakatifu Francisko katika ukweli na uwazi, kwa kuheshimu na kuthamini umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, tema Ambayo ameivalia njuga katika Waraka wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” inagusa umuhimu wa utunzaji wa ekolojia, unaotaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu na kwa namna ya pekee, haki za watu mahalia huko Amazonia, ambako ukoloni mamboleo unaofumbatwa katika nguvu ya kiuchumi unatishia usalama, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amefurahi sana moyoni mwake kutembelea eneo la Puerto Maldonado ambako amekutana, amezungumza na kusikiliza shuhuhuda mbali mbali za watu mahalia ambao zinazofumbata nguvu ya kitamaduni, urithi mkubwa hata kwa vijana wa kizazi kipya.

Mama Kanisa katika mazingira ya Amazonia, anapaswa kuiga mfano wa Mtakatifu Turibius Mogrovejo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lima, Msimamizi wa Maaskofu wa Amerika ya Kusini, aliyejisadaka kwa ajili ya ujenzi wa umoja wa Kanisa, akathubutu kupiga kasia hadi kuvuka ng’ambo ya pili ya mto! Nyuma yake kulikuwepo na umati mkubwa wa watu uliokuwa unamfuata kama kiongozi katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika utamadunisho, ushuhuda wa imani tendaji, huduma makini ya Injili ya upendo na majadiliano katika ukweli na uwazi kama sehemu ya mchakato mzima wa maendeleo endelevu ya binadamu.

Inasikitisha kuona, anasema Baba Mtakatifu, eneo la Amazonia linatumiwa kama “kichwa che mwenda wazimu” kwa ajili ya kuwanufaisha watu wachache. Makampuni ya kimataifa yanataka kuchimba madini kwa fujo na kukata miti ovyo, ili kupata faida kubwa, lakini kwa hasara ya maisha, utu na heshima ya wananchi mahalia. Hawa ni watu wanaotumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Majiundo makilini na endelevu kwa vijana wa kizazi kipya ni muhimu ili kuwasaidia kulinda, kudumisha na kuendeleza mila na tamaduni zao njema!

Huu ndio mchakato wa utamadunisho, unaopania kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inakita mizizi yake kwenye akili, nyoyo na maisha ya watu, tayari kuganga na kuponya yale mambo yanayosigana na tunu msingi za Kiinjili. Eneo la Amazonia linahitaji mihimili thabiti ya Uinjilishaji, hawa ni wakleri, lakini zaidi Mashemasi wa kudumu, watakaokuwa na dhamana ya kuwatangazia watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu na kuwagawia Mafumbo ya Kanisa kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa. Majiundo awali na endelevu kwa Mashemasi wa kudumu ni muhimu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanapata posho ya kujikimu maisha.  Mashemasi wa kudumu wajengewe uwezo wa kutafsiri Injili na nyaraka mbali mbali za Kanisa, ili kuwa kweli ni wahudumu wa Neno la Mungu na Injili ya upendo, kielelezo makini cha imani tendaji Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia, pamoja na mambo mengine, itapaswa kupembua kwa kina na mapana umuhimu, utume na dhamana ya Mashemasi wa kudumu katika maisha na utume wa Kanisa huko Amerika ya Kusini.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu Katoliki nchini Perù kuwa karibu sana na wakleri wao, kwa kujenga na kudumisha moyo na huduma ya kibaba; kwa kukuza na kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kushirikiana na kusaidiana kiutu na kikanisa; kwa kujali na kukidhi mahitaji ya wakleri wao: kiroho na kimwili. Maaskofu kwa kuwekwa wakfu, wanapewa dhamana na wajibu wa kulea watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao! Bila huruma na upendo wa kibaba, Maaskofu wanapoteza dira na mwongozo wa maisha yao katika kufundisha, kuongoza nakuwatakatifuza watu wa Mungu.

Bila fadhila ya ubaba, wema, ukarimu na msamaha, wakleri wengine wanapoteza ile hamu ya maisha na wito wao wa kipadre. Maaskofu wawe karibu na mapadre wao, ili kuwatia shime katika maisha na utume wao; kuwakaripia pale wanapoanza kukengeuka na kutopea katika malimwengu; Maaskofu daima wawe ni mashuhuda na wahudumu wa Injili. Maaskofu wasiwe na uchu wa mali na fedha, kwani haya ni mambo yanayoweza kuwatumbukiza katika aibu na fedheha kubwa. Wajitahidi kuwatendea haki wakleri wao, kwa kuwaonya, kuwasikiliza na kuwapatia nafasi ya kutubu na kuongoka. Maaskofu wawe na busara, unyenyekevu na uvumilivu, kabla ya kutoa maamuzi ya hatima ya maisha na wito wa mapadre wao.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kujenga upendo na mshikamano; kwa kuwathamini na kuwajali wakimbizi na wahamiaji ambao wana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa hasa katika Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda, kielelezo cha imani tendaji. Wakimbizi na wahamiaji, wamekuwa ni wahudumu wa Injili ya upendo kwa njia ya huduma kwa wazee na watoto; wako mstari wa mbele kurithisha imani na matumaini kwa wale wanaowazunguka. Ni waamini ambao wanasaidia kulipyaisha Kanisa la Kristo. Kumbe, hata wakimbizi na wahamiaji wanao mchango mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu Francisko. Sehemu kubwa ya Amerika ya Kusini inakabiliwa na saratani ya rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya umma, kielelezo kikubwa cha kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha adili na utu wema. Kutokana na mwelekeo huu, siasa haina tena mvuto, changamoto na mwaliko wa kuwainjilisha tena na tena wanasiasa, ili waweze kujikita katika uaminifu; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu; ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Uinjilishaji wa wanasiasa ni changamoto pevu kwa Mama Kanisa, lakini ni jambo linalowezekana kabisa anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Ushawishi wenye mvuto na mashiko pamoja na majiundo makini kwa wanasiasa ni mambo msingi yatakayowawezesha wanasiasa kutekeleza dhamana na wajibu wao mimtarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Amerika ya Kusini inaendelea kuongoza kwa watu wake kushindwa kulipa kodi halali kwa maendeleo ya watu. Baadhi ya watu wametumbukia katika sera za kibepari zisizoheshimu wala kuthamini utu na heshima ya binadamu. Kuna uvunjifu mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu za nchi na matokeo yake, wafungwa wamejaa magerezani na huko utu na heshima yao kama binadamu vimewekwa rehani kutokana na kufurika kwa magereza. Lakini magereza inaonekana ni kwa ajili ya wanyonge kwani wala rushwa na wafanyabiashara haramu ya dawa za kulevya na utumwa mamboleo, wako nje na “wanaendelea kuponda mali. Siasa Amerika ya Kusini imeoza! Maaskofu waivalie njuga changamoto hii katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anahitimisha mahojiano maalum na Baraza la Maaskofu Katoliki Perù kwa kuwataka kuanzisha sera na mikakati makini kwa ajili ya wafanyakazi katika vikosi vya ulinzi na usalama, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani, upendo na mshikamano wa kitaifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.