Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Mama Kanisa anashiriki katika mchakato wa uinjilishaji wa kina!

Miujiza, maajabu na ishara ni alama za uwepo wa Ufalme wa Mungu zinazodhihirisha kwamba, kweli Yesu Kristo ni Masiha na Mkombozi wa ulimwengu. - AFP

31/01/2018 17:03

Ndugu mpendwa, tukumbuke kuwa katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu, yaani sehemu hii ya Neno la Mungu toka Injili ya Marko, swali kubwa toka kwa watu waliokuwa wanamsikiliza ni kuwa Yesu ni nani? Domenika iliyopita tumeona wasiwasi huo toka kwa Wayahudi – huyu ni nani? Leo swali elekezi ni kuwa Yesu alikuja kufanya nini?  Katika Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tunaona mambo mengi yakifanywa na Bwana. Tumeweza kuona pia jinsi siku ya Yesu ilivyo, yaani mpango kazi wake kwa siku na utekelezaji wake. Alipotoka katika sinagogi – alienda nyumbani kwa mkwewe Petro, anaponya, watu wanamletea wagonjwa, anawaponya, anajitenga kwa ajili ya sala na baadaye anafundisha kuhusu ufalme wa Mungu. Huu ndiyo mpango kazi wa Yesu kwa siku.

Jambo kuu na la msingi ni kuwa Yesu alikuja kutangaza kwanza habari njema za ufalme wa mbinguni. Ni vizuri nasi pia leo tukatafari kuhusu hilo. Amekuja kutangaza habari njema kwa maskini – Lk. 4:18-19 – Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenipaka mafuta niwahubirie maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafunga kufunguliwa, vipofu kuona tena, kuwaletea wafungwa uhuru, na kutangaza mwaka uliokubalika kwa Bwana. Hapa twapata jibu kwa nini Yesu asubuhi ile, katika somo la injili – hata baada ya kuambiwa kuna umati mkubwa, aliwaagiza wanafunzi wake waondoke, waende miji jirani, kuhubiri habari njema pia huko. Katika Barua Evangelii Nuntiandi, Papa Paulo VI – anasema wazi – uinjilishaji kwa hakika ni neema na wito kabisa wa kanisa, ndiyo utambulisho wa kanisa. Somo la pili la leo latupatia msingi wa somo letu la Injili la leo – kuinjilisha ni sawa na kupumua. Uinjilishaji ndiyo pumzi ya Kanisa. Namna hii ya ufahamu unatuchanganya wengi wetu. Yaani ni upi hasa utume wa Yesu? Hapo juu tunapata jibu. Kwamba kwanza Yesu amekuja kutangaza ufalme wa Mungu. Mengine yote hutokana na hilo. Hebu tuongeze majibu zaidi ili kusaidia ufahamu huu. Katika Mt. 6:33 – tunaendelea kupata majibu – Basi tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na uadilifu wake, na hayo yote mtaongezewa.

Lengo la Yesu kuutangaza ufalme wa Mungu ni kutoa nafasi kwa wanaoamini, watawaliwe na roho ya Mungu kwanza. Mahangaiko yetu katika sura ya dhambi, utengano, magonjwa, mateso n.k yanaingia katika hali yetu ya udhaifu. Tukielewa vizuri mapenzi yake Mungu, haya yote yataponywa na tutajikuta katika hali ya kupokea neema na baraka yake Mungu. Tatizo ni kuwa tunataka kutatua matatizo yetu kadiri tunavyofikiria sisi. Sisi tunataka kumweka punda nyuma ya mkokoteni. Wakati kazi ya punda ni kuvuta mkokoteni.

Lile kundi lililokuja asubuhi ile ni aina ya watu tuliona nao sasa. Walimtafuta Yesu kwa ajili ya shida zao tu. Na ndivyo tunavyoishi imani yetu. Angalia kwa mfano mahudhurio yetu katika ibada na shughuli mbalimbali za kanisa na zinazomhusu Mungu. Pengine tunapotaka kutatua au tukiwa na maombi fulani tu ndiyo tunaonekana kanisani. Mfano tukiomba misa kwa ajili ya marehemu wetu, familia nzima hufika kusali siku hiyo. Lakini siku nyingine za wiki, za jumapili ambapo tunajiona hatuna shida, basi na Mungu hapewi nafasi yake. Tunaishi na Mungu au tunafanya mambo ya Mungu kimatukio tu. Tukio fulani na hasa linalotutisha likishapita, basi na Mungu hatumhitaji tena kwa wakati huo. Kwa kweli haya ni mahusiano hatarishi na Mungu. Hatari ya kumtumia Mungu kama mganga wa kienyeji.

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S

31/01/2018 17:03