2018-01-30 09:43:00

Rais Paul Kagame ndiye mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika


Umoja wa Afrika, umemchagua Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwa ni Mwenyekiti mpya wa umoja huu katika mkutano wake wa 30 umeliohitimishwa huko Addis Ababa, nchini Ethiopia. Anasema, kipaumbele chake cha kwanza ni ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika na kwamba, ataendelea kutumia diplomasia katika kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazojitokeza Barani Afrika. Waafrika wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa katika medani za kimataifa na wala si watu wa kubezwa na kudharauwa. Rais Donald Trump wa Marekani, aliyekutana na kuzungumza na Rais Paul Kagame wa Rwanda huko Davos, Uswiss ameonesha nia ya kutaka kushirikiana na Umoja wa Afrika katika kukuza na kudumisha ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika. Bwana Rex Tillerson, Katibu wa Nchi wa Marekani, anatarajiwa kutembelea nchi kadhaa za Kiafrika mwezi Machi, 2018 ili kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia.

Kati ya mambo yaliyopewa uzito wa pekee ni kadiri ya Kamishna mkuu wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ni masuala ya ulinzi na usalama Barani Afrika  hasa katika maeneo ambayo bado yana vita, kinzani na misigano ya kijamii. Nchi ambazo kwa sasa zinakabiliana na hali tete ni pamoja na DRC ambako kuna uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu na utawala wa sheria; Sudan ya Kusini ambako sasa imegeuka kuwa tena uwanja wa vita na malumbano ya kisiasa wakati maelfu ya watu wanapoteza maisha kutokana na vita, njaa na utapiamlo wa kutisha, bila kusahau Mali na jirani zake. Umoja wa Afrika umeridhia utekelezaji wa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya viongozi wa Sudan ya Kusini. Kwa mara ya kwanza, viongozi wa Umoja wa Afrika wameamua kushirikiana kwa karibu zaidi katika masuala ya usafiri wa anga, kwa kuhamasisha uwekezaji na vitega uchumi miongoni mwa nchi za Kiafrika. Makubaliano haya yanakwenda sanjari na ukuaji wa soko huria ili kukuza na kudumisha uchumi Barani Afrika.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa viongozi wa Afrika wakati wa mkutano wao wa mwaka, anapenda kwa namna ya pekee, kuwahimimiza viongozi wa Umoja wa Afrika kuhakikisha kwamba, wanajikita katika utekelezaji wa Azimio la Malabo, ili kuwakomboa wananchi wa Bara la Afrika kutoka katika lindi na baa la njaa na umaskini. Wadau mbali mbali wa maendeleo, kwa kutambua dhamana yake katika mchakato mzima wa mapambano haya, hawana budi kushikamana na Bara la Afrika ili kutokomeza baa la njaa!

Viongozi wa Umoja wa Afrika waoneshe kwa vitendo dhamana ya kupambana na baa la njaa Barani Afrika kwa kurekebisha sera na mikakati ya kilimo ili kweli sekta hii iweze kuwanufaisha watu wengi zaidi. Ili kuweza kufikia lengo hili anasema Baba Mtakatifu kuna haja ya kujenga na kudumisha majadiliano katika ngazi mbali mbali kwa kuwahusisha wadau wa ndani na nje ya nchi katika mapambano dhidi ya baa la njaa. Kumbe, hapa kuna haja ya kukazia zaidi uwajibikaji wa pamoja, mshikamano na umoja.

Wakati huo huo, Bwana Kuang Weilin, Mwakilishi wa China kwenye Umoja wa Afrika amekanusha taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba, China ilikuwa inapeleleza Makao makuu ya Umoja wa Afrika tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2017 na kwamba, taarifa hii ililenga kuchafua uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Nchi za Kiafrika.

Na habari zaidi kutoka Addis Ababa, Ethiopia, zinasema kwamba, Waziri mkuu wa Ethiopia Bwana Hailemariam Desalegn, Rais Abdel Fattah El Sisi wa Misri na Rais Omar Al Bashir wa Sudan Kongwe, wamekutana na kuamua kuanzisha Mfuko wa Ushirikiano wa pamoja kati ya Mataifa haya matatu, ili kukuza na kudumisha ustawi na maendeleo ya wananchi wao. Kwa sasa Ethiopia inajenga bwawa litakalogharimu kiasi cha dola za kimarekani bilioni 4.8 hadi litakapokamilika, jambo ambalo limezua hofu kubwa kwa Misri kwa kuhofia kina cha maji kuweza kupungua na athari zake katika ukuaji wa maendeleo yake. Hadi sasa ujenzi wa bwawa hili umekwisha kukamilika kwa asilimia 63%. Ethiopia inasema, bwawa hili ni muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya wananchi wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.