Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Wakleri ambataneni na watu wenu ili kuwahudumia vyema

Papa Francisko anawataka wakleri kuwa kati pamoja na waamini wao ili kuwahudumia vyema zaidi.

30/01/2018 14:51

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakleri kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwiga Kristo Yesu, Mchungaji mwema, kwa kuwasindikiza watu wao katika shida na mahangaiko yao: kiroho na kimwili; kwa kuwa karibu, ili kuwaonjesha huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kamwe, viongozi wa Kanisa wasiwe wenye mioyo migumu na wepesi katika kuwahukumu watu wao. Kristo Yesu katika Injili ya Marko 5: 21 - 43 anaonesha jinsi ambavyo Yesu alivyojitahidi kutekeleza dhamana na utume wake kati ya watu wake. Siku yake ilisheheni matukio mbali mbali yaliyomwezesha kuwatembelea watu waliokuwa wanateseka, kuwa kati ya watu waliokuwa na kiu ya kutaka kumwona pamoja na kuwasaidia katika shida na mahangaiko yao: kiroho na kimwili!

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema haya wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 30 Januari 2018. Umati mkubwa wa watu ulikuwa ukimfuata Yesu na wala hakuwa na ofisi maalum ambako alijiwekea ratiba na muda wa kufuatwa na watu walikuwa na shida mbali mbali, hakuwadai watu malipo kwa huduma alizokuwa anawapatia, bali Yesu alikuwa daima kati pamoja na watu, ili kuwatangazia furaha ya Injili. Huu ndio mfano bora wa mchungaji mwema, unaopaswa kuigwa na wakleri ndani ya Kanisa, Wajisadake bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu, ili inapofika jioni, wawe wamechoka sana na hivyo kupumzika kama watoto wachanga kifuani pa mama zao!

Injili ya Marko ambayo ndicho kiini cha tafakari ya Baba Mtakatifu kwa siku hii, inamwonesha Kristo Yesu alivyomponya mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili! Mwanamke aliyethubutu kugusa upindo wa vazi la Yesu na imani yake, ikamponya kweli! Yesu alikuwa daima akizungukwa na umati mkubwa wa watu. Wakleri, wawe na ujasiri wa kuwatembelea watu wao, ili kuwamegea huruma, upendo na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yesu alitenda daima kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wake; akajinyenyekesha hata wakati mwingine kudhihakiwa na kutemewa mate!

Baba Mtakatifu anawakumbusha Wakleri kwamba, wamepakwa mafuta ya Krisma ya Wokovu na hivyo kuwekwa wakfu katika Madaraja mbali mbali ya huduma kama: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu, lakini Krisma ya kweli ni ile ambayo inaacha chapa katika sakafu ya mioyo wa waamini wanaopata huduma kutoka kwa Wakleri wao; kwa kuonesha uwepo wao wa karibu, kwa kuguswa na mahangaiko na mateso yao; kwa kuwamegea huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Wakleri wasiwe na mioyo migumu wala wepesi kuwahukumu watu wao, wawe na huruma, upendo, faraja na uvumilivu, kama kielelezo makini cha huruma na uwepo wa Mungu kati ya waja wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwaombea wakleri wao, ili kweli waweze kuandamana na watu wao, kwa kuonesha ukaribu, huruma na upendo wa Mungu. Kwa njia hii, kweli watu wa Mungu wataweza kufurahia na kufarijika na huduma makini inayotolewa na wakleri wao, kiasi cha kushikwa na mshangao mkuu kama anavyosimulia Mwinjili Marko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

30/01/2018 14:51