2018-01-30 14:30:00

Papa Francisko: Shikamaneni ili kupambana na baa la njaa Barani Afrika


Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kuungana, kushikamana na kushirikiana kwa dhati ili kupambana na balaa la njaa na utapiamlo wa kutisha miongoni mwa watoto unaoendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa sehemu kubwa ya Bara la Afrika. Hiki ni kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa Rais Alpha Condè, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika aliyemaliza muda wake wakati huu ambapo, Umoja wa Afrika ulikuwa unafanya kikao chake cha thelathini kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO.

Baba Mtakatifu anaunga mkono jitihada za utekelezaji wa Azimio la Malabo lililotiwa sahihi kunako mwaka 2014 huko Malabo, Equatorial New Guinea, ambapo Umoja wa Afrika (AU), uliziagiza nchi wanachama kutenga angalau asilimia 10%  ya bajeti kwa ajili ya sekta ya kilimo. Mkwamo wa utekelezaji yakinifu wa Azimio la MAPUTO la mwaka 2003 na baadaye MALABO, 2014 katika nchi nyingi za Kiafrika, kumetajwa kuzorotesha mpango wa uwekezaji katika kilimo na usalama wa chakula, hali ambayo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa umaskini Barani Afrika bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, vita, kinzani na migogoro ya kisiasa na kijamii ni kati ya mambo yanayoendelea kusababisha baa la njaa Barani Afrika.

Mambo mengine msingi katika Azimio la MALABO ni pamoja na Afrika kutokomeza baa la njaa ifikapo mwaka 2025, kuongeza fursa za ajira kwa angalau asilimia 30% ya vijana kupitia mnyororo wa ongezeko la thamani kwa mazao ya kilimo. Azimio la Malabo anasema Baba Mtakatifu Francisko linapania kuboresha tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo, ili kuleta mageuzi na maboresho ya katika maisha ya wananchi wengi, hasa wale wanaoishi vijijini. Changamoto za maendeleo Barani Afrika zinahitaji kwa namna ya pekee, dira na mwelekeo mpya kwa kujikita zaidi katika ushirikiano, ili kuweza kukidhi kwanza kabisa mahitaji msingi ya binadamu, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, daima haki, amani na maridhiano vikipewa msukumo wa pekee. Umoja wa Afrika kwa kushirikana kwa karibu zaidi na FAO kunaonesha kwamba, baa la njaa linapaswa kushughulikiwa kwa dharura na wala hakuna tena nafasi ya kusubiri zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kwa namna ya pekee, kuwahimimiza viongozi wa Umoja wa Afrika kuhakikisha kwamba, wanajikita katika utekelezaji wa Azimio la Malabo, ili kuwakomboa wananchi wa Bara la Afrika kutoka katika lindi na baa la njaa na umaskini. Wadau mbali mbali wa maendeleo, kwa kutambua dhamana yake katika mchakato mzima wa mapambano haya, hawana budi kushikamana na Bara la Afrika ili kutokomeza baa la njaa! Viongozi wa Umoja wa Afrika waoneshe kwa vitendo dhamana ya kupambana na baa la njaa Barani Afrika kwa kurekebisha sera na mikakati ya kilimo ili kweli sekta hii iweze kuwanufaisha watu wengi zaidi. Ili kuweza kufikia lengo hili anasema Baba Mtakatifu kuna haja ya kujenga na kudumisha majadiliano katika ngazi mbali mbali kwa kuwahusisha wadau wa ndani na nje ya nchi katika mapambano dhidi ya baa la njaa. Kumbe, hapa kuna haja ya kukazia zaidi uwajibikaji wa pamoja, mshikamano na umoja. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwapatia baraka zake za kitume wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Afrika, kama sehemu ya mchakato wa kupambana na baa la njaa na umaskini, ili hatimaye, familia ya Mungu Barani Afrika iweze kufurahia rasilimali na utajiri uliomo Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.