2018-01-29 15:08:00

Papa Francisko: Mahakama za Kanisa heshimuni dhamiri ya Kikristo!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 29 Januari 2018 amezindua Mwaka wa Mahakama ya Rufaa ya Kipapa, “Rota Romana”, kwa kukazia umuhimu wa wadau wakuu wa Mahakama kuhakikisha kwamba, wanaheshimu “Dhamiri”, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo vinavyotekeleza utume wa amani ya dhamiri, ambayo kimsingi ni jambo jema linalofumbata hukumu zao. Katika hukumu inayohalalisha au kutengua ndoa ya Kikristo, Mahakimu na Majaji wanatekeleza dhamana na wajibu wao kama mabingwa katika dhamiri ya Wakristo, dhamana inayowataka kumwomba daima Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa moyo wa unyenyekevu mintarafu ukuu wa utume waliokabidhiwa na Mama Kanisa, daima wakijitahidi kuunganisha kanuni maadili ambayo Hakimu anapaswa kuitumia anapotekeleza utume wake mintarafu dhamiri nyofu.

Ni kwa njia ya mwanga wa Roho Mtakatifu, Majaji na Mahakimu wamepewa dhamana ya kuweza kuingia katika dhamiri za waamini, ndiyo maana Mababa wa Kanisa kwa kutambua udhaifu wao wa kibinadamu, daima walianza maadhimisho ya Mtaguso mkuu na Sinodi kwa kuomba uwepo wa Roho Mtakatifu kwa njia ya sala ya “Adsumus”. Mababa wa Sinodi anasema Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu kuhusu ndoa na familia wamekazia umuhimu wa kuheshimu dhamiri, dhana ambayo imesisitiziwa pia kwenye Wosia wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Hii inaonesha kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro akiwa ameungana na Mababa wa Sinodi wameona umuhimu wa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza viongozi wa Kanisa, ili kujibu kwa ufasaha matumaini ya waamini walioweka kadiri ya dhamiri , bila kulazimika kusubiria kwa muda wa miaka mingi na kwamba, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na katika changamoto za maisha wameweza kuona mwanga ndani ya Kanisa ili waweze kupata amani katika dhamiri zao! Dhamiri nyofu ni muhimu sana kwa wanandoa watarajiwa wanaotegemea kujenga familia kadiri ya mpango wa Mungu.

Mama Kanisa mwingi wa huruma na mapendo kwa kutambua dhamiri za waamini wake wenye kuhitaji ukweli, amewaonya wale wote wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika shughuli za kichungaji katika masuala ya ndoa na familia kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wanandoa watarajiwa kujenga na kulinda “madhabahu ya dhamiri zao ya Kikristo”. Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika barua zake binafsi kuhusu mchakato wa mabadiliko katika masuala ya ndoa na familia amekazia umuhimu wa kuanzisha uchunguzi wa kijimbo, utakaosaidia kuwa na mchakato wa haraka unaosimikwa katika haki kwa kuangalia chanzo na sababu za kuvunjika kwa ndoa.

Kwa upande mwingine, Wosia wa kitume “Furaha ya upendo ndani ya familia” unabainisha mikakati ya shughuli za kichungaji zinazoweza kutumika kwa ajili ya kuwasaidia wanandoa watarajiwa kuanza mchakato wa mang’amuzi na hatimaye, uamuzi wa kuchagua maisha ya ndoa na familia. Sura tano za mwanzo wa Wosia huu zinafumbata kwa namna ya pekee kabisa utajiri wa Agano kati ya Bwana na Bibi mintarafu Mpango wa Mungu kadiri ya Maandiko Matakatifu yaliyomwilishwa na Mama Kanisa katika historia na utume wake. Hapa kuna haja ya kuendeleza fadhila ya: imani, matumaini na mapendo, ili vijana wa kizazi kipya waanze tena kurejea, huku wakiwa na dhamiri hai na yenye utulivu kuamua kufunga ndoa inayoheshimu zawadi ya uhai wa watoto ambao kimsingi ni chemchemi kubwa ya furaha kwa Mungu, Kanisa na binadamu. Wosia huu pia unatoa mbinu mkakati wa kuwasaidia vijana kufanya maamuzi magumu katika maisha yao ili kuwa na mwelekeo chanya zaidi kwa ajili ya ustawi  na mafao ya binafsi na wengi zaidi kwa kuzingatia dhamiri nyofu.

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa haina budi kujielekeza katika kugundua tena na tena umuhimu wa kutunza na kudumisha dhamiri njema ya Kikristo inayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili. Hii ni changamoto kubwa inayowataka wakleri kufanya kazi usiku na mchana ili kuangazia , kutetea na kuenzi dhamiri nyofu ya Kikristo. Hapa Mababa wa Sinodi wamekazia“Regula fidei” yaani: “uaminifu kwa Kanisa”  na Mafundisho tanzu kuhusu Ndoa na Ekaristi pamoja na kuendeleza mchakato wa Ukatekumeni wa maisha ya ndoa na familia unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayowapatia wakristo chapa ya kudumu na neema inayopaswa kulindwa na kutunzwa na wanandoa.

Ulinzi wa roho zao ni muhimu sana kwa Kanisa pamoja na viongozi wa Kanisa. Huu ni utume pia kwa Wakristo wote kuhakikisha kwamba, wanalinda na kutunza dhamiri nyofu kwa kuondokana na misimamo mikali ya maisha ya ndoa na familia kama anavyokazia Mwenye heri Paulo VI ili kuepuka kabisa tabia ya baadhi ya waamini kutokuwa na utii kwa Kiongozi mkuu wa Kanisa na Mtaguso wa Kanisa, kiasi cha baadhi ya watu kujiondoa kwenye Mafundisho halali ya Kanisa, kielelezo cha kutopea kwa imani na hivyo kuacha madhara makubwa kwa Kanisa ambaye ni Mama na Mwalimu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, imani inaangazia hali ya sasa na ile ijayo kuhusu masuala ya ndoa na familia, Kanisa na Jamii katika ujumla wake, hali inayohitaji ukatekumeni endelevu ili dhamiri za Wakristo ziweze kuwa wazi kwa mwanga wa Roho Mtakatifu na kujielekeza kwa kile ambacho Kristo na Kanisa lake wanataka, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ushirikiano mkubwa miongoni mwa familia ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna uhusiano mkubwa kati ya dhamiri na mchakato wa ndoa, kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, kusiwepo na mazoea na kishawishi cha kuifanya haki kuwa ni sehemu ya ukiritimba, kwani kufanya hivi ni kusaliti dhamiri ya Kikristo. Ndiyo maana maamuzi ya Askofu mahalia pamoja na wahusika wote wa mahakama za Kanisa katika ngazi ya kijimbo wanapaswa kushirikiana ili kukamilisha mchakato wa kutengua ndoa ya Kikristo. Dhamiri ya wanandoa wanaoteseka, kamwe isizimishe safari ya neema, ndio maana kuna haja ya usindikizaji baada ya ndoa kuvunjika na talaka kutolewa, daima kwa kutafuta ukweli, ili kweli hukumu iliyotolewa iweze kuweka huru dhamiri za wanandoa husika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.